Maaskofu: Watawala heshimuni maoni ya wananchi Katiba mpya |
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya, amewataka Watanzania kuilinda amani kama mboni ya jicho ikiwa ni pamoja na kuitii mamlaka ya Mungu iliyopo.
Akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa waumini wa kanisa hilo pamoja na Watanzania katika ibada iliyofanyika Dayosisi ya Mpwapwa mkoani hapa,
Askofu Chimeledya alisema kuwa mwaka 2013, ulikuwa na changamoto mbalimbali, hivyo Watanzania wajifunze kusamehe ili kuwa na amani ya kweli.
Alisema kuwa katika mataifa mbalimbali, watu wenyewe kwa wenyewe wanapigana kwa tatizo la kutosamehe wakati hayati Nelson Mandela, ni mfano mzuri na amefundisha kusamehe.
"Hakuna namna yoyote itakayofanya bila kusameheana ili kuwa na amani ya kweli," alisisitiza Askofu Chimeledya.
Aliwataka Watanzania kuwa na chachu ya ukombozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
"Pia nawasihi mjenge moyo wa uzalendo ili kulisimamia taifa kwa uadilifu...wazee wa makanisa waendelee kuhubiri ukombozi," alisema Askofu Chimeledya.
Akizungumzia suala la tatizo la dawa za kulevya, Askofu Chimeledya aliomba serikali kuongeza nguvu kusimamia jambo hilo kwa kuwa lina watu fulani wanaojihusisha na inawezekana wanafahamika.
"Serikali ichukue hatua thabiti ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwani vijana wanaathiriwa sana," alisema Askofu Chimeledya
Aidha, alisema kuwa ni jambo jema kumshukuru Mungu kwa kuuona Mwaka Mpya wa 2014. Hata hivyo, alisema kumekuwapo na mafanikio katika taifa kwa mwaka 2013 ikiwa ni pamoja na mchakato wa Katiba mpya ambao umeleta historia. Pia alisema ugunduzi wa gesi, madini ya uranium, ni neema ya mwaka 2013 ambapo sasa kunahitajika kuwa na sera na usimamizi mzuri kwa manufaa ya Watanzania wote.
Kuhusu maandamano na migomo, Askofu Chimeledya alisema kuwa watu wapewe nafasi ya kusikilizwa ili kusiwapo na migomo wala maandamano yanayosababisha athari kwa taifa.
"Niwaombe sasa Watanzania kutafuta haki kwa kuandamana kwa amani bila kuleta vurugu...kuandamana kwa kutafuta haki lakini yasiwe ya kuvunja amani iliyopo," aliasa Askofu Chimeledya.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment