Mahusiano yako na Mungu ni ya Muhimu zaidi kuliko Mahitaji yako Kujibiwa, naye na Mungu hutumia sana uhitaji wetu kuimalisha mahusiano yake nasi


Carlos Ricky Wilson Kirimbai
 Swala la mahusiano yako na Mungu ni la muhimu zaidi kwa Mungu kuliko swala la kujibu maombi yako kwa hiyo Mungu anapenda sana kama una uhitaji au changamoto, wewe mwenyewe uende mbele zake na hitaji lako kuliko kuwaambia wengine tu wakuombee. Ukienda mbele za Mungu na uhitaji wako itatoa fursa ya vitu viwili vikubwa kutokea.

1. Kuimarika kwa mahusiano yako na Mungu maana siku zote mazungumzo kati ya wawili huimarisha mahusiano kati yao.

2. Uhitaji wako kujibiwa na Mungu na hivyo kukufanya wewe kukua katika kumjua kwako Mungu.

Zaburi 103: 7

7Alimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake.

Usiwe mtu tu wa kutamani kuyajua matendo ya Mungu uwe mtu anayetamani kuzijua na njia zake pia.

Wana wa Israeli waliyajua tu matendo ya Mungu maana kila wakipata changamoto walikuwa wanamfuata Musa. Utakuwa mpendwa anayejua tu matendo ya Mungu kama kila unapopata changamoto wewe ni mbio kwa mchungaji wako, au mtumishi fulani wa Mungu au watu wengine wao wakuombee.

Musa alijua njia za Mungu kwa sababu kila akipata changamoto alikuwa akienda kwa Mungu na hakuwa na mtu wa katikati wa kumwendea.

Tamani kuwa kama Musa na sio wana wa Israel.

Ayubu anatuambia kwenye Ayubu 22: 21.

21 Mjue sana Mungu, ili uwe na amani;
Ndivyo mema yatakavyokujia.

Ukimjua sana Mungu utakuwa na amani. Amani ni neno Shalom linalomaanisha hakuna kilichopungua na hakuna kilichovunjika. Ukimjua Mungu hakuna kitakachopungua na hakuna kitakachokuwa kimevunjika maishani mwako na mema yatakujia.

Kwanini usitamani kumjua Mungu ili uwe na amani na mema yakujie? Kwanini Mchungaji wako amjue Mungu zaidi kupitia changamoto zako wewe?

Daudi anatuambia kwenye Zaburi 34: 10.

10Wana-simba hutindikiwa, huona njaa;
Bali wamtafutao BWANA hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.

Tafuta kumjua Mungu. tafuta kumsogelea wewe na sio mwingine amsogelee kwa niaba yako.

No comments:

Post a Comment