Jumapili iliyopita Wachungaji wengi wa makanisa ya Tanzania Assemblies of God, TAG, jijini Dar es Salaam, na hata wale wa mikoani walishtushwa na jumbe za kutatanisha zilizokuwa zikiandikwa kuomba fedha huku mwombaji akijifanya mchungaji/muandishi.
Mtu huyo mwenye kuvaa ngozi ya kondoo wakati uhalisia ni ‘mbwa’ mwitu, alivaa uhusika wa mchungaji na kudai mchungaji huyo anaumwa yuko Hospitalini hivyo atumiwe fedha kwa njia ya mtandao.
Miongoni mwa jumbe hizo zilizoelezwa kuwachanganya wachungaji wengi zilisomeka hivi: “Bwana Yesu asifiwe Mch. Sheyo mimi ni Mch. Paulo Mulokozi, simu yangu ina matatizo kdg upo wapi muda huu nina shida na wewe, naomba unijibu kwa meseji nipo hospitali . Mungu akubariki.”
Baada ya ujumbe huo, ambazo baada ya uchunguzi mdogo ilibainisha zilikuwa zikitumwa kwa simu iliyokuwa na jina la Zuhura Kambangwa, na hata hivyo alituma ujumbe wa pili unaosomeka: “Samahani naomba uniazime elfu 40 nitakuona jioni saa 1 nina mgonjwa amelazwa.”
Uchunguzi wa chanzo cha habari ambacho ni gazeti la
Jibu la Maisha umebaini kuwa, Mtu huyo aliyetumia namba za simu, 0716494277, alijibiwa na Mchungaji Seiko Sheyo wa Kanisa la TAG, Sinza, kuwa hajasajili namba ya tigo hivyo ampatie namba ya Voda.
Akajibu hivi: “Nitumie kwa namba 0758863991, line yangu wameifungia.”
Hilo lilikuwa moja ya majaribio ya mtu huyo kujipatia fedha bila jasho ambayo aliyafanya kwa wachungaji zaidi ya 30, na watumishi wengine wa gazeti hilo la Jibu la Maisha pamoja na wafanyakazi wa Makao Makuu ya TAG.
Aidha imebainika kuwa akitumia jina la Mhariri wa Gazeti la Jibu la Maisha, Bw. Singo Mgonja, tapeli huyo aliandika ujumbe kuomba fedha kwa wachungaji kadhaa wa jiji la Dar es Salaam, na mikoani na akafanikiwa kupata shilingi 30,000 kwa mtu anayejulikana kama Mwangomwango, mkazi wa Mbeya, ambaye bila kudadisi kasoro kadhaa katika ujumbe huo alituma fedha.
Katika jaribio lingine la kipuuzi, Mtu huyo alijaribu pia kumtapeli Mhariri wa mwingine wa Gazeti hilo
Bw. Mgonja, akijifanya ni Joseph Ongong’a hata hivyo baada ya majibizano marefu ya jumbe za simu Mhariri alimtaka mhusika kutuma mtu achukue fedha taslimu kwa kuwa hana fedha kwenye mtandao na mwisho aliishia kuingia mitini.
Mbali na kufanikiwa kujipatia fedha kidogo zoezi hilo la udanganyifu lilisababisha usumbufu mkubwa kwa Wachungaji waliokuwa wakipokea jumbe hizo.
Kwa mujibu wa Uchunguzi wa gazeti hilo jaribio la kwanza likuwa ni kwa Mhariri wa Habari wa Jibu la Maisha, Ms. Flora Matara, ambaye alitumiwa ujumbe unaosomeka: “Bwana Yesu asifiwe dada Flora, mimi ni Kaka Samweli Thomas simu yangu ina matatizo kidogo, upo wapi muda huu nina shida na wewe, naomba nijibu kwa SMS nipo hospitali. Mungu akubariki. Ujumbe huo kutoka simu namba 0716494277, ujumbe huo ulitumwa Jumapili Septemba 9, saa mbili asubuhi.
Inaelezwa kuwa Mhariri huyo wa habari baada ya kupokea ujumbe huo akiwa karibu na kanisani, alishtuka kwa kuwa Samweli aliyetajwa ni mmoja wa maripota wa gazeti hilo, hata hivyo alipojaribu kumpigia mtumaji hakupokea na badala yake alituma ujumbe akisema atume SMS kwa kuwa yuko wodini kaka yake anaumwa kisha akaomba Sh.35,000.
Akionesha msisitizo aliandika: “Naomba utume ili punguze deni jioni nitakupa ibada njema.”
Ujumbe kama huo ulitumwa kwa kubadilisha majina ya watu na kutumwa kwa Emiliana Kalinga, Grace Luhombo, Joseph Ongong’a, Rehema Abbasi, Laston.
Mwingine aliyejaribiwa katika utapeli huo ni Mchungaji Elingarami Munisi, ambaye alitumiwa ujumbe ukionesha unatoka kwa Mch, Mulokozi wa kuomba shilingi elfu 45,000 kwa madai kuwa anamgonjwa.
Uhalifu huo uliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Urafiki, jijini Dar es Salaam, na kufunguliwa jarida la Uchunguzi namba URP/RB/7227/2012.
Wapelezi wa jeshi hilo wanaendelea kumsaka mhalifu huyo ambaye inadhaniwa kuwa alikusudia kulishambulia kanisa tena siku ya ibada wakati watu wakiwa kanisani kumwabudu Mungu.
Uchunguzi zaidi wa Gazeti hilo umebaini kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la utapeli wa kutumia mitandao ya simu ambapo watu waovu wamekuwa wakitumia simu za mkononi kutapeli watu.
Mbali na kutumia majina ya watu mbali mbali matapeli wamekuwa wakitumia ujanja unaobadilika badilika kujipatia fedha kwa njia isiyo halali, huku wakidanganya watu kuwa watawapatia ajira na kuwaelekeza katika makampuni kadhaa.
Mbali na utapeli huo, kuna utapeli mwingine wa kutumia kadi za ATM, ambapo wenye akaunti hujikuta katika mkanganyo mkubwa baada fedha kuchukuliwa huku kumbukumbu zikionesha kuwa zilitolewa na kadi halali ya mteja.
Katika moja ya matukio mabaya mmoja wa wafanyakazi wa Idara ya Elimu ya Kanisa la TAG, Bw. Thadeus Mbutta, alitapeliwa kiasi cha shilingi 800,000 na katika tukio la kutatanisha kwenye benki moja kubwa ya kibiashara nchini (jina tunalihifadhi kwa sasa).
Uchunguzi wa gazeti hilo ulibaini kuwa wakati Bw. Mbutta akiwa mkoani Lindi kwa shughuli za kikazi, akiwa na kadi yake ya ATM, fedha zake zilichukuliwa katika mashine iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Jambo la kustaajabisha ni kuwa benki wanashikilia madai kuwa kadi iliyotumika ni ya mteja, lakini walipotakiwa kutumia picha za CCTV Camera, zilizopo kwenye mashine hizo kumtambua mhusika walidai kuwa zoezi hilo litachukua muda hadi mwezi mmoja kukamilika.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa utapeli wa kutumia teknolojia umekuwa ukitesa mabenki kadhaa nchini, japo matukio mengi hayatangazwi kutokana na hofu ya kukimbiwa na wateja.
Kipidi cha nyuma wageni kadhaa walikamatwa kwa tuhuma za kutumia mitambo maalumu kuiba fedha za wateja katika mabenki na madai hayo yamesababisha baadhi ya watu kutoa fedha zao katika mabenki na kutumia njia mbadala.
Source : Gazeti la Jibu la Maisha