“Naweza kukumbuka vyema siku ya msiba wetu, ilikuwa ni usiku wa manane tulipovamiwa chuoni na kulazimishwa kutoka nje ya vyumba vyetu. Wauaji wakiwa na bunduki za kivita AK 47, sumu, mishale na visu vikali, walianza kuwahoji wanafunzi majina yao, wale waliokuwa na majina ya Kikristo walipigwa risasi na wengine kuchinjwa kwa kisu. Miili yao ilipangwa mistari nje ya majengo ya chuo. Wanafunzi waliokuwa na majina ya asili walitakiwa kutaja baadhi ya aya za kuran, walioweza walipona na walioshindwa waliuawa hapo hapo.”
Hiyo ni sehemu ya maelezo ya Bw. Elkanah Sardauna, mwanafunzi aliyenusurika kimiujiza kuuawa katika mauaji yanayofanana na mateso ya Mpinga Kristo, yaliyotokea mwezi uliopita katika Chuo Kikuu kimoja kilichopo Kaskazini mwa Nigeria na kuistaajabisha dunia.
Akielezea mkasa mzima kwa machozi huku akiwa amelazwa katika hospitali ya Mubi, Sardauna alisema kuwa njia ya kuepuka kifo ilikuwa ni kuukana Ukristo na kutaja jina tu kulitosha kuwafahamisha wauaji kuwa ni Mkristo, alienda mbali zaidi na kuwaambia wazi jina lake na kuwa yeye ni Mkristo.
Hata pale alipopigwa hadi kuanguka chini na kisha kuonywa kutotaja tena jina la Yesu aliendelea kusisitiza kuwa ni Mkristo. Na kwa kweli alikuwa tayari kwa lolote, lakini si kumkana Yesu.
Mwanafunzi huyo akiwa na maumivu makali alitanabaisha: “Walipotoka nje kila mtu alishikwa na bumbuwazi kwa kile kilichokuwa kikiendelea. Ilikuwa kama sinema na hakuna aliyejua nini kitatokea, ghafla ikatolewa amri ya kutoka nje na kila mtu kutaja jina lake, huku mauaji yakiendelea.”
Alieleza kwamba kila mmoja pasipo kujiandaa alianza kueleza anaitwa nani, na hapo sasa ikajulikana nani ni Muislamu na nani ni Mkristo, kwa waliokuwa na majina yasiyoeleweka (Kilugha) alitakiwa kutaja vifungu flani vya kuran.
Hata hivyo wanachuo wengi walishindwa mtihani wa kutaja aya hizo za Kuran na wakaangukia mikononi mwa mauti wakiaminika kuwa ni Wakristo waliojifanya Waislamu ili kukimbia kifo cha kuchinjwa.
“Walipofika kwangu waliniuliza jina langu, niliwaambia mimi ni Mkristo naitwa Elkanah, baada ya kusikia hivyo walinisukuma chini na kupaza sauti zao wakisema ‘Allahu Akbar.’ Nililia na kumwita Yesu pale pale chini. Walinitaka ninyamaze nisitaje jina hilo tena, lakini niliendelea na hapo wakanipiga risasi mkononi na kunichinja sehemu ya shingo yangu.
“Kabla ya kunikata sehemu ya shingo yangu walinitaka nilikane jina la Yesu na imani yangu ya Kristo, kwa kweli nilikataa. Walisema kuwa kila atakayekubali kufanya kile walichokuwa wakitaka basi uzima wake uko mikononi mwao. Kweli walikua na chuki kali dhidi ya Ukristo.”
Baada ya tukio hilo, Sardauna anaeleza kwamba walimtupa chini na wakadhani amekwisha fariki, wakamwacha na kuondoka zao.
“Ni Mungu tu aliyeniokoa kwani walipokuja kwenye bweni letu tukulikuwa wanafunzi wanne ambao tunalala chumba kimoja, sisi wote tulikuwa na majina ya kikristo, wanafunzi wenzangu watatu waliuawa mbele ya macho yangu,” alisema kwa majonzi.
Niliokotwa na kupelekwa hospitali na Mwandishi wa habari ambaye alibaini kuwa bado nilikuwa hai na nilihudumiwa na hapa naendelea na maisha. Nadhani Mungu ameuhifadhi hai uhai wangu kwa kusudi lake,” alisema kijana huyo.
Kiongozi mmoja wa kikristo nchini Nigeria, Mchungaji Gideon Para Mallam, ambaye pia ni Katibu wa Shirikisho la Kimataifa la wanafunzi wanaotoka katika makanisa ya kiinjilisti, ‘International Federation of Evangelical Students,’ aliliambia Shirika la Habari la Open Doors kuwa si tu kwamba vifo hivyo vinasikitisha, lakini pia wanaua taifa la kesho."
Afisa mmoja wa usalama aliliambia Shirika hilo la Habari kuwa, kundi la Boko Haram ni mchanganyiko wa watu wenye mafunzo ya kivita kutoka sehemu mbalimbali za dunia walihamia jimboni humo. Mpaka sasa wanachama wa kundi hilo waliokamatwa kutokana na matukio hayo ya mauaji ni 154 na 30 kati yao waliuawa kabla ya tukio la kuwaua wanafunzi huko Mubi.
Alisema kwamba miongoni mwa silaha ambazo polisi walizikamata katika msako baada ya mauaji hayo zikiaminika kuwa zilitumika kuua wanafunzi hao ni pamoja na AK47, Sub Machine gan, sumu, mishale na visu.
Siku mbili tu kabla ya mauaji hayo, Chuo hicho kilikuwa na uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi na wengi wao waliuawa tena wakitajwa kuwa walikuwa Wakristo.
Shirika la Habari la ‘The Christian Association of Nigeria (CAN) limebainisha kwamba wauaji hao ‘jihadists’ kabla ya kufanya tukio hilo walisambaza barua kwa waamini katika eneo hilo wakiwataka kuikana imani ya Kikristo ndani ya wiki mbili au wasubiri maumivu, huku wakiwakataza kuonyesha onyo hilo kwa watu wa usalama kwa kuwa kufanya hivyo kungemaanisha kujihukumu kifo.
CAN ilisema wanaamini kuwa Boko Haram wanahusika moja kwa moja na tukio hilo ingawa Waislamu nchini humo wanakataa. Hata hivyo Shirika la Utangazaji la BBC lilieleza kwamba katika uchaguzi uliofanyika shuleni hapo walimchagua rais wa serikali ya wanafunzi ambaye ni Mkristo, ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliuawa.
Rais wa CAN, Mchungaji Ayo Oritsejafor, alisema kuwa amesikitishwa na mauaji ya wanafunzi wasiokuwa na hatia na kwamba wamelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa linawakamata wote waliohusika na kuwaachia wasiohusika.
"CAN tunaamini katika umoja na kwa namna hiyo tunawaomba wanawake na wanaume wenye mapenzi mema kujitokeza kuungana na serikali kutafuta wauaji,” alisema.
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilikamata wanafunzi wengine waliosalimika ambao walieleza kwamba miongoni mwa wanafunzi hao wapo ambao ni sehemu ya mtandao wa Boko Haram.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Anglican, Gideon Adamu anaeleza kwamba inawezekana kuwa ni mambo ya kisiasa, huku akibainisha kwamba kaka yake naye aliwahi kupigwa risasi begani na mwisho wa siku alifariki.
Kiongozi mmoja wa kanisa dogo eneo hilo la Mubi, akiongea na Open Door, alisema kuwa licha ya mambo yote yaliyotokea, lakini kwa imani yao hawawezi kulipiza kisasi.
“Hatuwezi kuonyesha udhaifu wa kukimbia kutoka katika eneo hili, hapa ndipo Bwana alipotuita, tutakaa na kutimiza wito wetu kwa Mungu,”
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan akiongea na ndugu wa wanafunzi waliofariki alisema kutokana na tukio hilo maswali yamekuwa mengi kuliko majibu, huku akiongeza kwamba Boko Haram wamekuwa wakitumia nguvu za majeshi yao.