Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal: Udini usitugawe


Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewataka Watanzania kukataa kugawanywa kwa misingi ya udini.Akizungumza katika Baraza la Eid El Fitr mjini Tabora jana, Dk. Bilal, alisema ni busara waumini wa dini na madhehebu kujenga utamaduni wa kuvumiliana hasa  zinapotokea hitilafu miongoni na kati yao.Pia, Dk. Bilal alikemea ubaguzi unaotokana na kabila, rangi, jinsia au mahala mtu alipo au anapotoka.

“Kaeni pamoja na kutafuta muafaka kwa njia ya majadiliano ya amani na upendo, pasipo kutawaliwa na jazba wala chuki. Tukumbuke kauli na angalizo la Rais Jakaya Kikwete kwamba vita ya dini haina mshindi,” alisema.Dk. Bilal, alisema Tanzania imekuwa kisiwa cha amani na utulivu, jambo lisilompendeza kila mtu kutokana na kuwapo wanaotutazama (nchi) kwa jicho la husda na kuiombea mabaya.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal



“Wanatuombea tufike mahali tuharibikiwe ili wao wafurahi. Lakini wakumbuke kuwa dua la kuku halimpati mwewe," alisema. Alisisitiza kuwa amani katika taifa au jamii yoyote ni sharti la kwanza katika mchakato wa kuleta maendeleo.

Alisema anaamini viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kujenga maadili mema katika taifa hili na kwamba watu wakishiba imani ndani ya nafsi zao, wakaelewa na kuzingatia mafundisho ya dini zao, maovu yataondoka kati yao.

Alisema, uwapo wa amani na utulivu unaifanya serikali kupata ahueni, kwamba badala ya kutenga bajeti   kubwa kupanua magereza, kugharamia wafungwa na mahabusu na uendeshaji wa mahakama, rasilimali hizo zitaelekezwa katika mipango mingine ya maendeleo.

Dk. Bilal alisema katika siku za hivi karibuni, yameibuka matukio kadhaa yanaoashiria kutaka kuvuruga amani na utulivu wa taifa na kwamba hujuma hizo zinafanywa na watu wachache wasiolitakia mema taifa kwa maslahi yao binafsi.

Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ipo madhubuti na itahakikisha inapambana kwa nguvu zote kudhibiti hujuma zote zenye nia mbaya ya kuchafua sifa njema ya amani na utulivu wa Tanzania.
“Watanzania tumeishi kama ndugu na taifa moja kwa muda mrefu na kamwe hatutakubali tunu hii njema ivurugwe kwa kisingizio chochote kile,” alisema.

Aliongeza kuwa kamwe serikali haitakuwa tayari kuona Mtanzania anaishi kwa hofu na mashaka ndani ya nchi yake kutokana na vitendo vya wahuni wachache.

“Kila itakapobidi, tutawasaka, tutawakamata na kuwakomesha kwa rungu la mkono wa sheria. Nawahakikishieni kwamba Tanzania yetu itabaki nchi salama ya amani na utulivu na ya kupigiwa mfano daima.“

Alisema uhuru wa kuabudu katika taifa hili umejengewa misingi ndani ya katiba na kutokana na ukweli huo, kila mmoja anapaswa kuheshimu imani au dini ya mwenzake pasi kujiona kwamba imani au dini yake ni bora zaidi.

“Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia mwamko mkubwa kwa taasisi hizi kuanzisha shule za msingi, vyuo hadi vyuo vikuu jambo ambalo sisi katika serikali tunaridhishwa nalo na kuhamasisha kasi zaidi ya kuimarisha sekta ya elimu," alisema.

Alihimiza kuongeza kasi zaidi katika kuboresha sekta ya elimu na kuongeza kuwa uhai wa taifa hili na lolote lile duniani utategemea ubora wa elimu inayotolewa leo

Source: NIPASHE 

No comments:

Post a Comment