Waziri Nchimbi aliangukia Kanisa

Majanga yanayoonekana kuchipuka kila iitwapo leo, katika taifa la Tanzania na inayosababisha vifo kwa raia wasio na hatia, imeelezwa kuwa, suluhisho lake kubwa ni Kanisa kwani linamamlaka ya kimungu ya kutokomeza.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alitoa rai hiyo, hivi karibuni jijini Dar es Salaam, na kukazia kuwa endapo kila mkristo atasimama  katika nafasi yake kumtafuta Mungu ataliponya taifa linaloandamwa na vurugu za hapa na pale.  

Alisema, kwa sasa taifa limeanza kulegalega kimachafuko na kulifanya kuwa na sifa mbaya kitu ambacho ni tofauti na awali lilipokuwa likijulikana kama kisima cha amani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi

 “Kanisa ni kitu cha muhimu sana katika nchi yoyote duniani, maana lina nguvu ya kimungu na uwezo wa kukomesha mambo yanayolikabili taifa ikiwa watakatifu watamuomba Mungu kwa kumaanisha,” alisema Dk. Nchimbi.

Mbali na hilo, alisema lazima kanisa kwa kushirikiana na Serikali, wakemee wale wote wanaotaka kuharibu amani ya nchi ya Tanzania, ambayo ilikuwa mfano wa kuigwa katika mataifa mengine duniani, hivyo kufanya nchi kuwa na watalii wa kutosha.

“Kuna watu wanania mbaya ya kutaka kuharibu amani ya nchi yetu, hao lazima tuwawajibishe ili tuzidi kudumu katika amani, tuwakatae kwa njia yoyote, hao ndio maadui wa taifa letu, sisi wenyewe serikali hatutaweza bila kanisa kuingilia kati,” alisema Waziri nchimbi.

Waziri Nchimbi huku akionekana kuvaa sura ya huzuni ghafla alisema kuwa, amani iliyokuwepo awali sasa inavuja damu, na kuweka wazi kuwa ili kuindoa hali hiyo wakristo wakae vizuri kwa Mungu na kumsihi ainusuru Tanzania.

Hakusita kukemea wale wote wanaojihusisha na vitendo viovu kwa lengo la kuleta mtafaruku nchini, kuacha mara moja, huku akiahidi kushughulikiwa ikiwa hawataacha nia mbaya waliyonayo kwa taifa.

Akizungumzia suala la maadili, alisema hivi sasa maadili kwa vijana yameshuka hali inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya taifa, hivyo akawasihi wazazi kuwafundisha watoto wao maadili mema.

“Hivi sasa taifa linapoteza nguvu kazi kutokana na kushuka kwa maadili, kitu pekee ni wazazi kujikita kuwafundisha watoto wao kumpenda Mungu ili kukomesha hali hii ya watoto wetu kupotelea duniani,” alisema Waziri Nchimbi.

Sambamba na hilo, aliwataka watumishi wa Mungu kujikita kuwafundisha waumini wao kudumisha amani, na kukemea migogoro isiyo na tija kwa taifa.

“Nawaomba watumishi wa Mungu na viongozi mliopo hapa mjikite kuwafundisha waumini wenu kudumisha amani, na kukemea migogoro ya hapa na pale isiyo na tija kwa taifa,” alimalizia Waziri Nchimbi.

No comments:

Post a Comment