Kwaya ya Shalom yapeleka Albam sokoni

Kwaya ya Shalom ya Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania, (EAGT) Magomeni, linaloongozwa na Mchungaji Imani Mwakyoma, siku chache zimepita imezindua albam yake  ya nyimbo za injili yenye nyimbo nane iitwayo USILIELIE ambayo sasa iko sokoni ikipeleka habari njema za Injili hata kwa wale wasiofika kanisani wala kuhudhuria mikutano ya Injili.

Uzinduzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa CCM Mkwajuni, Kinondoni Dar es Salaam, ambapo watu wengi walijitokeza kushuhudia tukio hilo, uliosindikizwa na Kwaya mbalimbali wakiwemo waimbaji binafsi wa nyimbo za injili.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la wakimbizi Tanzania, Bi. Judith Mtawali ambaye aliwakilishwa na Bw. Fredrick Mwakalukwa kutoka ofisi za wakimbizi Kigoma.Bw. Mwakalukwa akiongea kwenye uzinduzi huo, aliipongeza Kwaya ya Shalom kwa juhudi kubwa ya kuandaa albamu nzuri na iliyojaa nyimbo zenye upako na zenye kuleta mabadiliko makubwa katika jamii.

Akisoma risala maalum mbele ya mgeni rasmi, iliyoandaliwa na Kwaya ya Shalom, mmoja wa wanakwaya hao, alisema hitaji lao kubwa kwa sasa ni vyombo vya injili pamoja na basi ndogo (costar) ambalo litasaidia kufanya huduma na kusafiri kwa urahisi kwenda kuhubiri Neno la Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Mbali na hilo alisema kuwa, wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufika hapo walipofikia kwa kuwa, baadhi ya wanakwaya hawana ajira na ndiyo sababu inayowafanya washindwe kufanya maendeleo ya Kwaya kwa kasi kubwa,  aliongeza kwamba gharama za ununuzi wa vyombo hivyo vya injili pamoja na basi ndogo vitagharimu Tsh. milioni 49.

Aidha kwa upande wake mwakilishi wa mgeni rasmi, Bw. Mwakalukwa aliwataka wanakwaya kuongeza juhudi ya kumtafuta Mungu na kufanya kazi kwa bidii, kwani hawana haja ya kuajiriwa sehemu nyingine, kama watafanya bidii katika miradi yao ya Kwaya.

“Miradi ya Kwaya inaweza kumlipa kila mtu mshahara wake kila mwezi, endapo mtafanya bidii, tena mkifanya kwa bidii wala hatakuwepo miongoni mwenu ambaye hatakuwa na maendeleo katika familia yake na mtafanya kazi ya Mungu kwa bidii,” alisema na kuongeza:

“Watu watastaajabu ukuu wa Mungu juu ya maisha yenu ya mwilini na rohoni.”
Bwana Mwakalukwa alimshukuru Mungu kwa ajili ya Kwaya hiyo na kumuomba Mungu aendelee kuwatumia wanakwaya hao katika maisha yao yote.

Wakionekana kujawa na furaha, Mchungaji wa Kanisa la EAGT Magomeni, Mwakyoma, pamoja na mkewe Salome Mwakyoma, walisema wanamshukuru Mungu kwa huduma aliyoweka ndani yao, pia kwa ajili ya kwaya ya Shalom ambayo wameweza kuizindua albamu yao ya kwanza ya nyimbo za injili.
“Mungu awafanikishe mipango yenu yote, pia awape umoja miongoni mwenu, pia namshukuru mgeni rasmi kwa kuhudhuria uzinduzi huu, sitalisahau kutambua uwepo wenu watu wote mliohudhuria uzinduzi huu na nawaombea baraka kwa Mungu,” alisema

No comments:

Post a Comment