Afisa wa Zimbabwe afariki ziara ya Obama Maaskofu, wachungaji jijini Dar wamlilia

Afisa wa Serikali ya Zimbabwe, Bw. Amos Mushanyinga, aliyetua nchini kushuhudia ziara ya rais wa Marekani, Barack Obama kwa mwaliko maalum na serikali ya Tanzania, amefariki baada ya kuugua ghafla na kukimbizwa katika Hospital ya Aghakhan ambapo madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake bila mafanikio.

Afisa huyu aliyefariki Julai pili mwaka huu, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali nchini humo, na alikuja nchini Tanzania akiwa na wazimbabwe kadhaa kushiriki ujio wa Rais Obama.

Akizungumza na chanzo cha habari hii, Askofu Mkuu msaafu wa Kanisa la TAG, Dk. Ranwell Mwenisongole, ambaye ni Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Upanga, City Christian Centre (CCC), lililotumika kumuaga afisa huyo alisema kuwa marehemu alifikwa na mauti Jumanne iliyopita jijini Dar es Salaam.
Askofu Mkuu msaafu wa Kanisa la TAG, Dk. Ranwell Mwenisongole, ambaye ni Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Upanga, City Christian Centre (CCC)
Aliongeza kuwa, marehemu Mushanyinga aliwasili nchini Tanzania akitokea nchini Zimbabwe, akiwa mzima kwa lengo la kushiriki mkutano wa Rais Obama na wafanyabiashara, katika ziara yake nchini Tanzania.

Mchungaji huyo aliongeza kuwa, hali ya   Mushanyinga ilibadilika ghafla hivyo kukimbizwa katika hospitali ya Aghakhani ya jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya matibabu, ambapo ili bainika kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la inni.

Mbali na hilo alisema, jitihada za madaktari hospitalini hapo, hazikuzaa matunda ambapo mauti ilimfika wakati akihudumiwa.

Dk. Mwenisongole alisema, ni jambo la kusikitisha kuona marehemu alifika nchini akiwa mzima lakini akarudi akiwa katika sanduku,  akawataka watanzania na Wakristo kwa ujumla, kukaa vizuri kwa Mungu na kuacha michanganyo kwani wakati wowote historia inaweza kufungwa.

Mtumishi huyo wa Mungu, Dk. Mwenisongole aliendelea kubainisha kuwa, kifo cha Mushanyinga kinapaswa kuwa fundisho kwa watu wote, kwa kile alichosema kwamba hakuna ajuae lini Bwana atahitaji roho yake, hivyo kuwa tayari wakati wowote, ili kuwa na maishi milele mbinguni.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uanafunzi na Maandiko ya kanisa hilo, Mchungaji Elingarami Munisi, ambaye alikuwa rafiki wa marehemu wakati wa uhai wake, akizungumza alisema kuwa amesikitiswa na kifo cha mheshimiwa huyo.

Mbali na hilo, aliwataka watanzania kudumisha upendo na mshikamano, huku akiwashukuru kwa kujitokeza kumuaga na kumsindikiza marehemu kusafirishwa kwenda nchini Zimbabwe kwaajili ya kuupumzisha mwili wake.

Sambamba na hilo, aliwasihi wakristo kuzidi kumpenda Mungu na kumtumikia, ikiwa ni pamoja na kuiandaa mioyo yao kwa habari ya maisha yao.

Ibada hiyo maalumu ilihudhuriwa na Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, ambapo alisema Marehemu alikuwa kiongozi bora nchini Zimbabwe katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchumi.

Habari zingine zinasema kuwa Afisa huyo alizungumza na Mchungaji Munisi siku mbili kabla ya kufariki dunia na aliahidi kuwa angeenda kuonana naye katika kanisa la TAG Kawe, Faith and Miracle Centre jumapili iliyopita, lakini hakupata nafasi hiyo baada ya kuugua.

Siku chache zilizopita Mchungaji Munisi alienda Zimbabwe kufundisha katika semina maalumu iliyoandaliwa na kansia ambalo marehemu alikuwa akisali na walipata nafasi ya kuzungumza na akamhudumia kiroho, mtumishi huyo wa umma ambaye pamoja na mambo mengine alikuwa mchumi.

No comments:

Post a Comment