BAKWATA yachangia ujenzi wa Kanisa Geita

Kiongozi mmoja wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), mkoani Mwanza, kwa kushirikiana na waislamu wapenda amani wamechangia kiasi cha shilingi milioni moja kwenye harambee ya ujenzi  wa kanisa la African Inland Church, Dayosisi ya Kalangalala Mkoa wa Geita.

Kiongozi huyo, Sheikh Salum Bala, pasi na kujali umoja na ushirikiano miongoni mwa viongozi wa dini nchini, aliongoza Waislamu wenzake kuchangia Kanisa la AICT katika harambee iliyofanyika Jumapili iliyopita.

Alipopata wasaa wa kutoa mawaidha kwenye kusanyiko hilo, lililokusanya watu kutoka maeneo kadhaa mkoani Geita, Sheikh Bala, alinukuliwa akiweka wazi kuwa Waislamu hawana uadui na Wakristo.

Sheikh huyo akikazia hilo, kwenye harambee hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa zamani, Mhe. Edward Lowasa, alisema Viongozi wa BAKWATA Mwanza wameanzisha umoja wao na kanisa kwajili ya kuendeleza amani na utengamano.

Dhumuni kubwa la kuanzisha umoja wetu na kanisa ni kuondoa chembe chembe za udini zenye kuleta chokochoko Mkoa wa Mwanza na Geita na kwa kudhibitisha Waislamu hawanachuki na Wakristo, tumeamua kuchangia ujenzi wa kanisa hili,” alisema Katibu huyo wa BAKWATA na kuongeza:

“Nimshukuru Waziri Lowasa kwa juhudi wa kuondoa udini, amekuwa mstari wa mbele kuangamiza roho chafu zenye kuibua  migogoro isiyokuwa na kichwa wala miguu.

 Akiongea na na chanzo cha habari hii moja kwa moja kutoka Geita, Mchungaji Simoni Masanyiwa wa African Inland Church, Dayosisi ya Kalangalala alisema ujenzi wa nyumba ya Mungu ulianza mwaka 2008 na unatarajiwa kufikia mwisho Desemba 2013.

Mtumishi huyo wa Mungu alisema, gharama za kukamilisha ujenzi huo zilihitajika jumla ya shilingi Mil. 600 lakini kwa sasa wanamshukuru Mungu kwani kiasi kilichobaki ni Sh. milioni 91 ambacho wanaamini hadi kufika Desemba watakuwa wamekamilisha.

“Watu wengi wamekuwa wakijitoa kuchangia jengo la kuabudia,  hatuna pingamizi na aina ya mtoaji au dini yake,  ikiwa kaguswa kuchangia kanisa sisi hatuna upinzani na hilo,” alisema mtumishi huyo na kuongeza:

“Kabla ya harambee ya Jumapili iliyopita, tulitoa kadi kwa waumini wetu na tuliwapa zingine za kuwagawia ndugu, jamaa na marafiki zao ili kuwaalika kuhudhuria siku ya changizo katika kukamilisha ujenzi wa kanisa.”
Kwa namna nyingine, Mchungaji Masanyiwa alisema Katibu wa BAKWATA Mwanza, alikuwa miongoni mwa waumini wengine wa kanisa hilo, na Mbunge wa Monduli Lowasa kuchangia ujenzi.

Hata hivyo, alimshukuru Katibu huyo wa BAKWATA kwa moyo kwake wa kuondoa tofauti za dini na kuungana nao akiambatana na waislamu kadhaa, kwenye harambee kuonyesha upendo na umoja ulioonekana kutaka kuyeyuka siku za hivi karibuni kwa sababu za uchinjaji.

“Najua anaweza asieleweke kwa waislamu wengine, lakini ninaloweza kueleza hapa ni kuwa, alichofanya Sheikh Bala ni jambo la kawaida kabisa, sisi hatujafikia kiasi cha mafarakano;
chokochoko zozote ni kazi ya Shetani,” alisema na kuongeza:

“Shetani  yuko duniani, sasa unataka kazi zake azifanyie wapi, hapa Geita Kanisa linashirikiana  na wao vizuri, hatukuwa na wasiwasi. Tatizo ni serikali kushindwa kutoa majibu ya hapo hapo inapoibuka migogoro.”

Source Jibu la Maisha.

No comments:

Post a Comment