Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG Dk. Barnabas Mtokambali asifu Njombe kuonyesha Mfano

Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dk. Barnabas Mtokambali, ametoa rai kwa maaskofu nchini, kuiga mfano wa ujenzi wa chuo cha kupanda makanisa kilichopo Njombe ili kutimiza mpango mkakati wa “Miaka Kumi ya Mavuno Tanzania kwa Yesu.” Dk. Mtokambali alitoa nasaha hizo wakati wa mahafali na uzinduzi wa chuo cha kupanda makanisa kilichopo Mkoa wa Njombe, chini ya Askofu wa Jimbo hilo, Patrick Luhwago, sanjari na semina elekezi ya viongozi iliyomalizika Juni 28, 2013. Askofu huyo alinasihi watumishi kujituma na kukamilisha ujenzi wa vyuo vyao vya kupanda makanisa, vilivyomo majimboni mwao ili kupata watenda kazi wengi walioandaliwa kiufanisi katika shamba la Bwana. Akihutubia katika uzinduzi huo, Dk. Mtokambali alieleza sababu za msingi za kuanzisha vyuo hivyo vya kupanda makanisa kote nchini kuwa ni pamoja na Kanisa kuongezeka kiidadi kupitia watendakazi wengi walioandaliwa vya kutosha na vyuo hivyo.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni Kanisa la TAG kukua kijografia, kiasi cha kufikia maeneo ambayo hayajafikiwa na injili, hivyo kulifanya kukua kwa kasi kama ilivyokuwa enzi za kanisa la Matendo ya Mitume ambalo Yesu aliliacha duniani. “Kuna ulazima mkubwa kwa kanisa letu kukua kijiografia hata kuwafikia watu ambao hawajawahi kufikiwa na injili,” alisema Dkt. Mtokambali. Alieleza sababu zingine za kuanzisha vyuo hivyo kuwa ni pamoja na kuliwezesha kanisa kukua kiufanisi na kwa ubora kama Neno la Mungu linavyoagiza. “Mshirika yeyote wa kanisa la mahali pamoja, mwenye wito wa kufanya kazi ya Mungu ni vema akapitia chuo cha kupanda makanisa na kupata cheti cha utendakazi, huku akiwa na elimu nzuri na mafunzo sahihi. Itamrahisishia kutenda kazi kiufanisi wakati wa huduma mahali popote tofauti na hapo awali,” alisema Dkt. Mtokambali na kuongeza: “Watu walikua wanaenda kutumika kabla hata ya kupata mafunzo ya utumishi na hatimaye kupata watu ambao wanaenda kinyume na misingi ya Neno la Mungu.” Kutumia vema rasilimali ya Kanisa la TAG, ni miongoni mwa sababu aliyoitaja huku akiongeza kuwa, kwakua kila kanisa la mahali pamoja hutoa asilimia 5, kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kutegemeza vyuo hivyo vya Biblia. Aliongeza kuwa, asilimia 75 hutoka makao makuu kwaajili yakutegemeza vyuo hivyo, na kusema TAG imewekeza kwa watumishi wake wote wanaopitia vyuo vya Biblia nchini Tanzania; huku akisisitiza kwa wale ambao wanasoma vyuo hivyo na kutoingia shambani kwaajili ya utendaji kazi, hawawatendei haki washirika wa TAG wanaojitoa kwa mali zao. Sanjali na hayo, Dkt. Mtokambali aliongeza sababu zingine kuwa ni kufanya jimbo kuwa na kituo chake kwa ajili ya shughuli za kijimbo, hapo ndipo patakua sehemu sahihi ya kufanyia mikutano, semina, makambi na mambo yote yahusianayo na jimbo kuliko kukodisha kumbi sehemu zingine. Aidha Askofu alisisitiza kuwa kuna vijiji vingi ambavyo bado havijafikiwa na injili, huku kanisa la Bwana likiwa limeridhika kwa kazi za pale kanisani tu, bila kupeleka injili mahali ambapo bado hapajafikiwa ambapo alihoji: “Kwanini vinywaji vya soda kama vile cocacola, pepsi na vinginevyo vimefika?. Hata vyama vya siasa huko ambapo injili bado haijafika vyenyewe tayari vimeshafika, kwanini kanisa tumelala na kutokuthamini kusudi la Mungu alilotuokoa kwalo?” alihoji kwa uchungu na kuongeza: “Kama vinywaji vimefika pamoja na vyama vya siasa, basi Yesu wetu ni zaidi ya hivyo vyote, jina lake lastahili pekee kusikika Tanzania yote.” Kwa upande wa mgeni kutoka nchini Marekani, Mch. David Willington aliwaasa watumishi kutokukata tamaa, kuvunjika moyo, kujikinai kwa yale wanayopitia na badala yake watambue kuwa katika changamoto zote wanazozipitia bado Mungu yu pamoja nao, na kuwa vita vya huduma zao si wao watakaopigana bali Mungu aliyewaita.

No comments:

Post a Comment