Athuman Hamisi aweka mkakati mzito wa kuleta watu kwa Yesu!

“Njooni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea.” (Yn.4:29). Maneno haya ya mwanamke msamaria aliyekutana na  Yesu ndiyo yaliyojaa ndani ya moyo wa Athumani Hamisi, na sasa ameanza mkakati wa kushuhudia nyumba kwa nyumba na kuwaleta kwa Yesu.

Katika kuendeleza mpango mkakati wa ushuhudiaji wa shabaha, uliobuniwa na mchungaji kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Magomeni, Mch. Dustan Kanemba, umeendeleza kuungwa mkono na jamii na hata Serikali ikiwa ni baada ya Athuman Hamisi (shoga) ambaye alikutana na Yesu na sasa anaitwa Amosi, kudhamiria kupanda jukwaani kuhubiri  mikutano ya injili kwa lengo la kuwaleta watu kwa Yesu.

Athumani ameamua kuianza kazi rasmi ya kumtumikia Mungu, chini ya Mchungaji wake Kiongozi, Dustan Kanemba na sasa ataanza kupanda jukwaani kushuhudia matendo makuu ya Yesu jinsi alivyombadilisha kutoka katika matendo maovu ya ushoga  alikomtumikia shetani kwa kipindi cha zaidi ya miaka 16 bila faida na sasa yuko huru.

Akiongea na chanzo cha habari, Mchungaji kiongozi wa Kanisa hilo, Dustan Kanemba, alisema kuwa wameanza mkakati maalum wa kuhubiri injili kwa njia ya mikutano ili kumkomoa ibilisi, na kukamata masalia aliowaficha katika ufalme wa giza.
wa kwanza Kushoto Athuman Hamisi
Aliongeza kusema kuwa, wanataka kuhubiri ili Magomeni yote iweze kumgeukia Mungu,na kuleta tumaini la kweli la amani itokayo kwa Bwana kwa kuwa matendo wayafanyao kwa sasa yanamchukiza Mungu kwa kiasi kikubwa ambayo pia yanahatarisha maisha yao.
“Tumeshuhudia wezi, vibaka, walevi na wazinzi wakiokoka, sasa ni wakati wa mashoga kuokoka na kumrudia Yesu”alisema Mch. Kanemba.

Aidha, alimsifu kijana Athuman  kwa uamuzi wa kujitangaza hadharani, ya kwamba ameachana na matendo machafu ya kishoga, na kumrudia Yesu, na kubatilishwa katika utu wa kale na kufanywa kiumbe kipya katika Kristo Yesu, jambo alilosema ni ujasiri wa ajabu ambao Mungu amempa baada ya kuokoka.

Anasema kijana huyo, hapo awali alitenda uovu uliokithiri, kwani ibilisi aliutumia mwili wake vibaya wala hakujali  madhara ambayo yangemkuta nyakati hizo, sasa Yesu amemfanya kuwa kiumbe kipya na kifaa kifaacho katika kazi yake ya injili.
Waumini wa  Kanisa la TAG Magomeni, wakimpongeza Athuman Hamisi kutokana na uamuzi wake wa kuachana na Ushoga na kumpokea Bwana Yesu
Kwa upande wake kijana huyo, ambaye kwa sasa ni jemedari wa Yesu, aliyejivikwa utu wa Kristo, amesema kuwa, atamtumikia Yesu katika kipindi chake chote cha uhai wake, na kumtangaza duniani kote ili kuhakikisha watu wanaachana na matendo maovu ya shetani.

“Nimekusudia kushuhudia watu wote matendo ya Yesu, na kumtumikia Kristo katika maisha yangu yote, ili shetani apate hasara katika ufalme wa kuzimu,”alisema na kuongeza:
“shetani akae chonjo, kwa kuwa tupo tayari kumvaa ili aachie mateka wa Mungu, na mimi nitapanda jukwaani kuonesha namna Mungu alivyoweza kuniokoa, na kunifanya tofauti na kuwa mtu mpya kutoka Ushoga, Uislamu, mpaka kuokoka na kuitwa Amosi,” alisema Athuman.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG Magomeni, Mch. Dustan Kanemba akilishwa keki na Athuman Hamisi

No comments:

Post a Comment