Afukuzwa kazi kwa kukutwa na shuhuda za BwanaYesu Asema yupo tayari hata kufa akimtetea Yesu

Mtaalamu mmoja wa utafiti katika Chuo Kikuu cha Ubelgiji amefukuzwa kazi kwa kosa la kukutwa na shuhuda za watu walioponywa na Bwana Yesu baada ya kuombewa katika makanisa ya kipentekoste.

Jambo la kustaajabisha zaidi ni kuwa mtaalamu huyo, Bw. Fernando Pauwels, alifukuzwa bila kupewa hata onyo, licha ya kufanya kazi kwa uaminifu kwa miaka 11, mfululizo.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika Habari la CBN (CBN News) Bw. Pauwels, alikuwa mtumishi mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Katoliki kiitwacho  Leuven, ambacho ni miongoni mwa vyuo  vile vya kale kabisa kikiwa kimeanzishwa katika miaka ya 1,400.

Habari za kiutafiti zinaonesha kuwa tofauti ya kiimani kati ya makanisa ya kipentekoste na katoliki nchini humo, imechangia kwani baadhi wanaamini katika uponaji wa kimiujiza na wengine hawaamini  hivyo japo ni Wakristo.

Inadaiwa kuwa viongozi wa utawala katika Chuo hicho walifanikiwa kuufungua mtandao wake na kushtushwa na picha na matukio ya miujiza na alichukuliwa kama muasi wa imani, hivyo akachukuliwa hatua kali za kumtimua kazi.

Alipoulizwa na Shirika la CBN, kuhusu mkasa huo alisema: “Watu wanaruhusa ya kuamini imani nyingi yoyote, tena ya kishenzi, lakini wasifutwe kazi, mimi niliyefanya kazi kwa uaminifu kwa miaka 11, nafukuzwa kwa kumuamini Yesu na kazi zake.”

Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vikongwe zaidi nchini Ubelgiji  kikiwa kimethibitishwa na makao Makuu ya Kanisa hilo yaliyopo Vatican. Lakini kwa sababu Ulaya ya kisasa ina mfumo unaofanana unaosimamia vyuo vikuu, suala la imani limekuwa changamoto kubwa.

Alisema: "Kama ungeniuliza unataka upate mkataba mpya?,” Ningesema  `ndiyo`.  `Una tatizo lolote na wafanyakazi wenzako? Ningesema hapana, kila kitu kiko vizuri kwa hiyo hakukuwa na tatizo na juma moja baadaye nikatimuliwa, nikabaki  najiuliza, `nini kimetokea?."

kilichotokea ni chuo kikuu hicho kutofurahishwa na huduma ya kwenye mtandao ya Fernando yenye kuamini katika nguvu na uwezo utokanao na upendo. Hii ni pamoja na shuhuda za watu mbalimbali walioshuhudia kuponywa kwa uweza wa Mungu kupitia huduma hiyo.

Pauwels alisema,"Chuo kikuu kilikuwa kimeona baadhi ya vipande vya picha za video zinazoonesha watu wakiponywa na kisha kutoa shuhuda ambapo kwa mtazamo wa chuo watu hao waliitwa kuwa siyo wanasayansi.

Msemaji wa Chuo hicho katika mahojiano na CBN alisema: "Mtafiti wa mambo ya kisayansi  anaporuhusu dini kuchukua nafasi ya sayansi, anakiuka taratibu na kushusha hadhi ya chuo na vilevile anaondosha imani ya uongozi kwake kwamba ataweza kuwafundisha watu imani badala utafiti."

Hata hivyo, alisema: "Kama nimefukuzwa kazi kwa sababu ya kuamini kitu kisicho cha kisayansi kama hicho, kwamba Yesu Kristo bado anaponya, najisikia vizuri, lakini walichonifanyia siyo sahihi."

Msemaji wa chama cha kidemokrasia cha Kikristo, ambaye anafanya kazi katika Bunge la Flemish, Bw. Ward Kennes aliiambia CBN: "Nilishangazwa sana kwamba chuo kikuu cha kikatoliki, ambako nami ndiko nilikosoma, kinafanya mambo kama haya."

Rik Torfs, mfanyakazi katika kitivo kimojawapo chuoni hapo ambaye pia ni mwanahabari aliliambia  gazeti la Flemish la Standard: "Uhuru wa kidini una maanisha kuwa kila mtu yuko
huru kuamini kitu chochote apendacho au kinachomvutia."

Siku za hivi karibuni, Torfs aliteuliwa kuwa mkuu wa kitivo kimoja chuoni hapo na mapema kabla ya uteuzi wake   alipohojiwa na CBN alisema endapo atashika nafasi hiyo, angemrejesha Fernando Pauwels kwa kumkodisha kama mtaalamu mwalikwa.

Pauwels, ambaye ana moyo wa kujitoa kwa ajili ya Kanisa la Mungu, alisema anajisikia vizuri anapoteswa kwa ajili ya Kristo, lakini pia anataka wakristo wenye itikadi kama yake walindwe kutokana na ubaguzi kama huo.

"Siku moja nitasimama mbele za Bwana na atasema, umefanya vema, Hicho ndicho kinachotakiwa," alisema.

No comments:

Post a Comment