Mauaji ya mtoto wa Mchungaji Mwimbaji

Utata mkubwa umegubika vifo vya mtoto wa Mchungaji mmoja wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), na muumini mwingine wa kanisa hilo, vilivyotokea hivi karibuni na kuacha maswali mengi, yaliyoacha mguno mkali kwa familia na hata jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, marehemu hao Utukufu Stefano na Yassin Pascal, walikutwa kwenye bwawa la  kubatizia  wakiwa uchi wa nyama, huku nguo zao na simu zikiwa pembeni.
Mchungaji Stefano Bugele, wa Kanisa la TAG, wilayani Sikonge, mkoani Tabora, akiongea na Jibu la Maisha, katika mahojiano maalumu; alisema kuwa siku ya tukio Mei tatu, mwaka huu, kijana wake huyo aliondoka nyumbani akichukua bomba la kupigia dawa akaenda kwenye bustani yao iliyopo umbali wa nusu Kilometa hivi.

Alisema kuwa baada ya kijana wake kwenda bustanini, yeye  aliongozana na Pascal kwenda kwenye msiba wa jirani na walipomaliza alimuuliza ikiwa ananafasi aungane na mwenzake kwenye kazi ya bustani.
“Unajua huyu Pascal ni muumini wangu wa kwanza nilipokuja kufanya umisheni hapa, na alipookoka alikaa nyumbani kwangu akawa kama mtu wa nyumbani, pia akapendana na mdogo wangu akamuoa hivyo akawa ni shemeji yangu. Na kwa kweli bado alisalia kuwa kijana wangu,” alisema na kuongeza:

“Nilipomwambia habari ya bustanini aliniambia kuwa hata yeye alipanga kunisaidia, nikachukua piki piki nikampeleka mpaka bustanini nikamkuta kijana wangu Utukufu anendelea na kazi, nikawaacha nikaondoka kwenda mjini kumpeleka kijana mmoja ambaye alipata ajali mbaya na kuumia mkono.”
Mchungaji huyo alisema kuwa, baada ya kumpeleka kijana huyo hospitali aliendelea na kazi zake kama kawaida na ilipofika saa  saba aliwapigia simu wakamwambia kuwa wanaendelea vyema na kazi.

“Mimi niliendelea na shughuli zangu na ilipofika saa mbili usiku nilipigiwa simu na kijana mmoja aliyekuwa na matatizo, nikaenda kumsaidia, ilipofika saa  tatu na dakika kadhaa mke wangu alinipigia simu akiniarifu kuwa mke wa Pascal alikuwa nyumbani akimsaka mumewe na wote walikuwa hawajarejea nyumbani hadi wakati huo,” alisema Mchungaji.

Alisema kuwa aliporejea nyumbani alijaribu kupiga simu lakini haikupatikana na alimuaga mkewe kuwa anaenda bustanini kuwatafuta, lakini mkewe akasema kuwa ni vyema waende wote, na kwa pamoja wakatembea hadi bustanini ambapo walistaajabu kukuta nguo zao na ndala na yebo yebo walizokuwa wamevaa, ingawa wenyewe hawakuwaona.

“Nilimwambia mke wangu twende kijijini kwa mke wa katibu wa kanisa tumuulize labda ana taarifa zao. Tulienda tukamgongea mama huyo na kumuelezea, akatuambia kuwa  majira ya  mchana alienda bustanini hapo kwa kuwa bustani yake nayo ilikuwa ikipuliziwa dawa na akawasifu  vijana hao kwa uchapaji kazi,”alisema Mchungaji na kuongeza:

“Mama huyo alituambia kuwa majira ya saa 11, jioni alipita tena hapo bustanini akitokea kwenye semina kanisani, akakuta nguo za vijana hao zikiwa zenyewe na hawakuwepo, kwa kuwa yeye ni msichana aliona kuwa pengine wamekwenda kuoga hivyo si vyema kuwasubiri kwani wanaweza kurejea wakiwa hawajavaa na akaondoka.”

Mchungaji Stefano, alisema kuwa baada ya maelezo hayo waliamua kurejea tena bustanini ambapo walichukua simu za vijana wao na kurejea kijijini ambapo walitoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji na hapo watu walianza kumiminika nyumbani kwake.
“Saa 12, alfajiri tuliondoka na kundi kubwa la watu kwenda bustanini kuwatafuta na tulipofika tu, tulistaajabu kuwaona wote wawili wakiwa ndani ya bwawa wakielea na huku wakiwa wameshafariki dunia. Nilipoona vile nilianguka na sikujua kilichotokea, hata walivyotolewa sikujua; nilipopata fahamu nilikuwa nyumbani na Polisi walishafika,” alisema  Mchungaji huyo  na kuongeza:

“Awali madaktari na Polisi waliwaangalia tu kwa mbali na kusema kuwa wamekufa maji tukazike, lakini alipofika Askofu wa TAG, Tabora akiwa na Afisa Upelelezi wa Mkoa waliambiwa warejee kwenye uchunguzi upya na wakafanya na kutoa taarifa ya kuruhusu mazishi yaendelee.”

Alisema ingawa inaelezwa kuwa walikufa maji lakini mimi nina mashaka kwa kuwa Utukufu alivuja  damu nyingi na hata walioosha maiti walisema wazi kuwa alikuwa na majeraha kichwani  ya kupondwa pondwa.
“Kwa kweli bado nafuatilia kwa makini tikio hili kwa kuwa kuna watu wamerusha habari mbaya za kunichafua. wametoa habari zao bila hata kuniuliza ,” alisema.

Mama mzazi wa Utukufu, Bi. Leah Amoni (Mama Mchungaji), akisimulia tukio hilo kwa uchungu alisema kuwa, wanamuachia Mungu aliye hakimu wa haki, lakini haamini kuwa kijana wake ambaye alikuwa akitegemewa kanisani kwa kazi ya Mungu alikufa kwa kuzama kwenye maji machache yasiyoweza kumzamisha hata mtoto wa miaka 10.

Mama huyo, anasema kuwa tukio hilo ni pigo kwao na kanisa, kwani licha ya mwanaye Utukufu kuwa mpiga vyombo na mwimbisha sifa, mwenzake waliyeuawa pamoja (Pascal) alikuwa Mwenyekiti wa Kwaya ya Kanisa.

“Wakati mmoja alikuwa akitoka damu nyingi mwingine alikuwa amekabwa shingo ikavimba, hali ambayo inaashiria kuwepo kwa mkono wa mtu. Hata hivyo tunamuachia Mungu yeye ndiye hakimu wa haki,” alisema.
Makamu Askofu wa Kanisa la TAG, Jimbo la Tabora, Sadoki Bukuri, alisema kuwa wamelipokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa, lakini kwa kuwa Polisi walishafanya kazi yao na kutoa kibali cha kuwazika marehemu wameliacha na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Mimi nami nilikuwa eneo la tukio, yaani kwenye bwawa wakati wa kuwatoa nilishiriki pia, lakini kweli niliona utata kwa kuwa, walikuwa wakitoka damu jambo ambalo ni ajabu kwa mtu aliyekufa kwa kunywa maji (kuzama),” alisema na kuongeza:
“Kanisa linaendelea na taratibu zake kama kawaida, ila mchungaji amepeleka maelezo yake kituoni na nadhani watafuatilia kujua ukweli wa jambo lenyewe.”

Utata zaidi wa tukio hilo unasababishwa na mfululizo wa matukio ya kuuawa kwa watumishi wa Mungu na kushambuliwa kwa makanisa Tanzania wakati huu.
Baadhi ya wakazi wa Tabora wanaeleza kutolewa hasa ukweli kuhusu hali hii na wanahitaji uchunguzi wa kweli ufanyike kama yanavyofanyika matukio mengine.

No comments:

Post a Comment