‘Mikutano ya Injili ruksa’ Askofu Dk. Bruno Mwakibolwa


Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania PCT, Mkoa wa Dar es Salaam, limetegua kitendawili kilichokuwa vichwani mwa watanzania wengi siku zimepita, juu ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara mara baada ya kutoa tamko lao juu ya suala hilo, hivi karibuni na kuzua sintofahamu, huku viongozi wa kisiasa nao wakizidisha utata.

Akisoma tamko hilo la Baraza la Maaskofu wa PCT, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Askofu Dk. Bruno Mwakibolwa, alisema kuwa, Serikali haijazuia mikutano ya hadhara japo kuna vyombo vilivyoandika  hivyo.

“Mnamo tarehe 7-8 Mei Mwaka huu, kulifanyika mkutano wa viongozi wa dini za Kikristo na  Kiislam chini ya uongozi wa serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, ambao hata sisi tulishiriki,” alisema Askofu Mwakibolwa na kuongeza.

“Katika kikao hicho yalijadiliwa mambo mengi yaliyohusu amani, usalama na ustawi wa jamii. Aidha mwisho wa mkutano huo tulifikia maazimio 16, na kati ya maazimio hayo hakuna azimio lililositisha au kuzuia uenezaji wa dini kwa njia ya mikutano ya hadhara.

Bali kilichoafikiwa ni mihadhara ya kidini kufanyika kwa namna ambayo haisababishi uvunjifu wa amani, kuwabugudhi watu au kuingilia uhuru wa kuabudu wa watu wengine.

Kwa sababu hiyo, Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Mkoa wa Dar es Salaam, limependa kuujulisha umma kwamba taarifa zilizoenezwa kwamba mikutano ya hadhara ya injili imepigwa marufuku si taarifa za ukweli, bali ni taarifa za uongo zilizopotosha ukweli wa yaliyo afikiwa.” alisema Dk. Mwakibolwa wakati akisoma tamko hilo.

Dk.Mwakibolwa aliweka wazi kuwa lazima injili ihubiriwe katika taifa la Tanzania ili watu wamgeukie Mungu na kuachana na utu wa kale,waishi maisha ya kumpendeza BWANA.

“Katika mikutano ya injili watu hatari wameokoka na kuachana na vitendo viovu, wezi wameacha wizi, mashoga wameacha kazi hiyo, majambazi wameacha ujambazi na sasa wanamtumikia Mungu hii ni kutokana na injili ya kweli isiyo na uchochezi wa aina yoyote inayohubiriwa na watu kuamua kugeuka,” alisema Mwenyekiti huyo wa PCT.

Hivyo akawataka watumishi wa Mungu,walioko maeneo mbalimbali ya taifa la Tanzania kuendelea kumtumikia Mungu kwa kuhubiri injili yenye lengo la kuwakomboa watanzania wanao potea dhambini.

Sambamba na hilo alisema, hata katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa watumishi wa Mungu kuhubiri injili, pasipo kubugudhiwa na mtu wa aina yoyote.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa ya watumishi wa Mungu kukamatwa hususani maeneo ya mikoani kutokana na kuhubiri mikutano ya injili ambapo Dk.Mwakibolwa alisema kuzuiwa kwa watumishi hao na kuzuiwa kufanya mikutano ni kwenda kinyume na sheria ya nchi.

Askofu David Mwasota ni Katibu wa PCT, akizungumzia suala hilo alisema kuwa, serikali haijazuia mikutano ya hadhara, bali mikutano yenye lengo la kuleta uchochezi ndiyo hairuhusiwi.

Katibu huyo akaongeza kuwa lazima watumishi wa Mungu wafanye kazi ya kuihubiri injili kupitia mikutano ili kuleta ukombozi katika taifa la Tanzania ili watu waachane uovu na kumgeukia Mungu aliye hai.

“Injili ndiyo uhai wa kanisa, sasa sisi tuzuie mikutano ya hadhara tutakuwa tumefanya nini, lazima injili ihubiriwe, injili ikizuiliwa hapo sasa hakuna haja ya kusajili makanisa, lazima tumtangaze Yesu aliye hai kupitia mikutano ya hadhara,” alisema Mwasota.

Mbali na hilo akawataka watumishi wa Mungu kujikita kuifanya kazi ya Mungu kwa bidii, ili kulikomboa taifa la Tanzania, ambalo hivi sasa linakabiliwa na changamoto lukuki, ikiwa ni pamoja na kuliombea.

No comments:

Post a Comment