‘Nilimwona aliyenimwagia tindikali’ Padre Mwang'amba

 Padri wa Parokia ya Mpendae ya Kanisa Katoliki Zanzibar, Anselmo Mwang’amba amesema kuwa alimwona mtu aliyemwagia tindikali na kumsababishia majeraha na kueleza kuwa anashangaa kuona polisi hawajamkamata hadi sasa.

Akizungumza jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwenye Wodi namba 16, Kibasila alipolazwa, Padri Mwang’amba alisema baada ya kumwagiwa tindikali, alimwona mtu huyo akikimbia kuelekea katika nyumba moja jirani.

“Kwa kuwa mimi nilikuwa na taharuki na maumivu, sikuweza kuendelea kumfuatilia, ila dereva aliyenikimbilia kunipa msaada aliniambia kwamba alimwona mhusika akikatiza kwenye uchochoro hadi alipoingia kujificha kwenye nyumba iliyopo jirani na eneo hilo,” alisema.
Paroko wa Parokia  ya Roho Mtakatifu Cheju Zanzibar, akisaidiwa na Frateri, Richard Haki kupumzika kitandani baada ya kuzungumza na waandishi katika katika Wodi ya Kibasila iliyopo katika Hosipitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijni Dar es Salaam jana.

Alisema majeraha aliyoyapata wakati akitokea katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao la Shine Shine saa 10.15 jioni, ambayo yanamsababishia maumivu makali, hayawezi kumfanya aikimbie Zanzibar, kwa kuwa hata Yesu Kristo wakati alipokuwa katika kazi za utumishi duniani alipata mateso makali kuliko yake.

“Nilisomea upadri nikiwa Zanzibar kuanzia mwaka 1976 hadi mwaka 1981 nilipopata upadrisho kamili. Niko huko kwa kazi ya Mungu wala si mwanadamu, kwa hiyo nikitoka hapa narejea hukohuko, siogopi, ingawa miaka hiyo nilipokuwa naanza kazi hii hakukuwa na mambo kama haya,” alisema.

Aliwataka Wakristo wanaoishi Zanzibar kuendelea kuwa na umoja na upendo pamoja na kuwa makini kwa usalama wao licha ya matukio magumu yanayowakuta ikiwamo vitisho na kuchomwa moto kwa makanisa.

Pia aliunga mkono shinikizo la kutimuliwa kazi kwa Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa kutokana na kushindwa kuwakamata watu wanaomwagia watu tindikali.

“Huyu bwana alishindwa hata kunijulia hali wakati nikiwa hospitali huko Zanzibar, tofauti na nilipokuja Bara ambako Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova walifika kunijulia hali na kuzungumza nami hospitali.

“Kwa hali hii, naona kwamba tukio langu ni la kupangwa na litazungumzwa sana lakini baada ya muda halitashughulikiwa. Atajeruhiwa mwingine tena lakini hatua za dhati za kudhibiti ukatili huu usiendelee hazijachukuliwa. Mimi ni padri wa tatu kufanyiwa ukatili,” alisema.

Mapadri wengine ni Ambros Mkenda aliyepigwa risasi na kujeruhiwa wakati Padri Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi.

Al-Shabaab wanaswa Zenji

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Zanzibar limewakamata watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab cha Somalia.

Source:mwananchi

No comments:

Post a Comment