Waziri Mkuu mstaafu Lowassa aendelea kulia na kiwango duni cha elimu

Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ameelezea kusikitishwa kwake na kiwango duni cha elimu katika shule za sekondari za kata na katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia mfuko wa elimu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa kijitonyama jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema, kiwango cha elimu katika shule hizo kinamsikitisha kwani ni cha chini.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM) allisema: ”Napenda niseme wazi kuwa kiwango cha elimu katika shule zile za kata na baadhi ya vyuo vikuu kwa kweli ni vya chini, hili mimi linanisikitisha sana kwa sababu elimu bora ni mkombozi kwa mtoto wa Kitanzania.

” Hata hivyo alipongeza kanisa kwa kusaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha na kuboresha elimu na kusababisha shule nyingi za kanisa kuwa na kiwango bora cha elimu.

Lowassa alisema baadhi ya watu wamekuwa wakisema mambo mbalimbali kutokana na kusindikizwa na marafiki zake katika harambee kadhaa na kumuunga mkono kwa kuchangia. Alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa marafiki zake ambaye ni wakili maarufu, Sadock Magai, kuwasilisha michango ya marafiki wa Lowassa katika harambee hiyo ambao walichangia Sh. milioni 50.

Miongoni mwa marafiki zake waliomchangia ni Lawrance Masha, Innocent Macha, Bashir Awale, Hamis Kindoroko na  Lemmy Bathelemew.

Aidha, walikuwapo Mbunge wa Segerea ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga aliyechangia Sh. millioni tatu na Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan, aliyechangia Sh. millioni mbili.

Lowassa alimpongeza Azan kwa kuchangia bila kujali Imani yake ya kidini. ”Nampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Idd Azan kwa kuja kwake kunisindikiza na kuchangia, hii ndiyo Tanzania ninayoijua, isiyo na dini, watu wa dini zote mnashirikiana,” alisema Lowassa.

Katika Harambee hiyo, jumla ya Sh. millioni 615 zikiwa ni fedha tasilimu pamoja na ahadi zilipatikana na kuvuka lengo ambalo lilikuwa Sh. milioni 250.

Source: NIPASHE

No comments:

Post a Comment