Mapadre wa Tanzania matatani

Wakati Umoja wa Mataifa (UN), ukilikalia kooni Kanisa Katoliki kwa kile ulichodai kuwa halijafanya bidii kuwashughulikia makasisi wake wanaotuhumiwa kwa kashfa ya kudhulumu watoto kingono, imebainika kuwa makasisi wawili wa Tanzania waliotuhumiwa kupokea misaada kutoka kundi la kishetani la Freemasons wametimuliwa bila huruma.

Wiki iliyopita, ripoti ya Umoja wa mataifa ilitolewa hadharani ikiyalaumu makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican, kwa kupuuzia au kuwalinda makasisi wake wenye kashfa ya kudhulumu watoto kingono, likataka hatua za haraka kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kufichuliwa kwa mafaili yenye kashfa hiyo.

Wakati hali ikiwa hivyo, chanzo cha habari hii kililifanya mahojiano na mmoja wa wataalamu wa Kanisa hilo (Kasisi mashuhuri) ambaye alinza kwa kusema:
“Umoja wa mataifa hauwezi kulazimisha mabadiliko yoyote ndani ya Kanisa Katoliki, ni kweli kuwa kashfa hizi zipo, lakini haziwezi kulifanya kanisa libadili kanuni zake, likifanya hivyo litakuwa sio kanisa tena.”

Kisha aliongeza: “Kanisa Katoliki haliwezi kuongozwa na UN, linasheria zake kali, ni kwa sababu tu watu hawajui, mfumo wake wa ndani ni mkali na hauchukuliani na uovu, kuna makasisi wawili wametimuliwa nchini kwa kutuhumiwa kupokea pesa na misaada kutoka kundi la Freemasons.”

Akiongea kwa kujiamini  Kasisi huyo, alisema makasisi waliotimuliwa ni kutoka Wilaya ya Same na Arusha  na mwingine  wa Mwanza alienda baa na baada ya kulewa alizua tafrani na kupigana, na kutokana na hali hiyo kanisa limeshamfukuza mara moja.

“Nakuambia Askofu wa Jimbo la Mwanza alipopata habari hizo alitoka na barua mkononi na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwake na kumsimamisha kazi. Huu ni ushahidi kuwa kanisa letu lipo makini, ingawa wengi wenu hamjui,” alisema mtoa habari wetu.

Akifafanua kuhusu tukio la kutimuliwa kwa makasisi waliopokea misaada ya kundi la Freemasons, alisema kuwa,  zamani makanisa  ya Katoliki yalikuwa yakipokea msaada kutoka Vatican, lakini utaratibu huo haupo kwa wakati huu na makanisa yanajitegemea kwa kuanzisha miradi yao, na hapo ndipo wengine walipopokea fedha  kutoka kwenye makundi  kama Freemasons.

Alisema kuwa baada ya kanisa kubaini taarifa hizo lilichunguza na kuwabaini mapadre kutoka Arusha na Same, kisha kuwasimamisha kazi wakisubiri uamuzi mgumu kutoka kwa Papa huko vatikani.
Kulingana na Taratibu za Kanisa Katoliki Padre anaweza kusimamishwa kazi na Askofu wake kwa mujibu wa taratibu na sheria za ndani ya kanisa (Canon Law) lakini hawezi kuvuliwa upadri kwani mwenye mamlaka hayo ni Baba Mtakatifu yaani Papa aliyeko madarakani.
Kisha chanzo cha habari yetu kiliendelea:

“Mfano miongoni mwa hoja nne za Umoja wa mataifa ni ukali wa wasimamizi wa shule za Katoliki, na ni kweli shule zina misimamo mikali sana. Kanisa limekataa kukubali kusikia kutoka nje kwa kuwa litapoteza ubora wa mafundisho yake, alisema na kuongeza:

“Unajua hapa kuna shinikizo la kuwataka mapadre waoe, lakini, si rahisi kukubalika. Misimamo ya mapadre imegawanyika kati ya Mashariki na Magharibi, mapadre wa Mashariki katika mataifa kama ya Urusi na Ukraine kabla ya kusimikwa wanaulizwa iwapo wanataka kuoa au laa, lakini wa Magharibi wanashikilia msimamo wa kutooa na hao ndio ninaowaunga mkono.”

“Ukiwa Padre ni lazima ujikane na ujitoe sadaka; sasa ukiwa na mke na familia si lazima utaipendelea kuliko wito wa kazi ya Mungu? Mimi kama kanisa litapitisha sheria ya kuoa nitaachana na ukasisi kwa kuwa sitaweza kutimiza wito wangu.”

Hata hivyo akaonya kuwa wale wote waliowahi kula kiapo cha ukasisi, hata wakiacha kamwe hawawezi kuishi vyema na wanawake wala kupata Baraka za Mungu.

“Angalia hata huyu Dk….(jina tunalihifadhi) aliacha upadre na kuamua kuoa lakini amekaa  na mke wa pili sasa na bado  hajafanikiwa  hata cheo anachotaka hawezi kukipata kwa kuwa aliacha kiapo chake, na  kuingia kwenye siasa,” alisema.

Alisema kuwa hata yeye amekuwa akitegwa na akina dada, lakini ameshinda majaribu kwa kuwa muwazi kutangaza hadharani wale wanaomjaribu ikiwa ni pamoja na kuwataja mimbarani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bi. Kirsten Sandberg, kiongozi wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya kutetea haki za watoto (CRC) alionya kuwa ukimya  wa Vatican kuhusu matukio ya kunyanyaswa  watoto kingono ni hatari  na lazima uvunjwe mara moja, wahusika watolewe ndani ya wigo mzito wa Roma na kuachiwa vyombo vya sheria.

Kisha aliongeza: “UN inaitaka Vatican kuwaondoa kwa haraka makasisi wote waliowahi kupata kashfa ya ngono na kashfa zote zinazojulikana lazima zichukuliwe hatua haraka.”

 Taasisi hiyo inayochunguza haki za watoto iliitaka mamlaka ya kiti kitakatifu cha Roma “Holy See” kubadili sera zake ambazo zinaonekana kuwa kichocheo cha makasisi wake kumalizia haja zao za kingono kwa watoto.

 “UN inaitaka Vatican kubadili msimamo wake mkali kuhusu utoaji wa mimba, matumizi ya vidonge au mbinu za kuzuia mimba ambayo imepitwa na wakati na haiwezi kutekelezeka katika nyakati hizi.
 Vaticani katika majibu yake ilisema kuwa itaichunguza ripoti yenyewe pamoja na waandaaji wake kabla ya kutoa msimamo wake. Hata hivyo kundi la makasisi waliosaidia kufichua vitendo hivyo Marekani limeikaribisha ripoti hiyo kwa mikono miwili. Wakati Vaticani ikidai kuchunguza riporti hiyo tayari baadhi ya yale yaliyotajwa na Umoja wa mataifa imeshayatupilia mbali ikisema ni  maovu na yasiyopaswa kujadiliwa na kanisa hilo kulingana na utamaduni wake.

Wachambuzi wanasema kuwa kwa kawaida kanisa hushikilia sheria zake zijulikanazo kama Canon Law, kuwa zinapaswa kutangulizwa mbele kabla ya sheria za kawaida za kijamii “criminal law” katika kushughulikia masuala yanayojitokeza ndani na ya kanisa

No comments:

Post a Comment