Uwepo wa Mungu Bila Neno la Mungu hauwezi kufanya Lolote katika Maisha yako

 
Pastor Carlos Kirimbai Manna Tabernacle Bible Church
Moja ya vitu ambavyo watu wa Mungu tunasahau sana kuhusu Mungu wetu ni kwamba Mungu hafanyi vitu kwa uwepo Wake bali Mungu anafanya vitu kwa neno Lake.

Iko kama tunasahau hili andiko hapa:

Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. (YN. 1:1-3 SUV).

Tunaona kwenye hiyo mistari hapo juu kuwa vyote vilifanyika kwa neno wala pasipo neno hakuna kilichofanyika ambacho kilifanyika. Kama vyote vinafanyika kwa neno na kama hakuna kilichofanyika ambacho hakikufanyika kwa neno ina maana hakuna kilichobaki ambacho kilifanywa na uwepo wa Mungu. Vyote vilifanywa na neno la Mungu.

Uwepo wa Mungu ni wa muhimu sana maana ndo nguvu inayofanya neno la Mungu liweze kufanya kazi lakini kitendea kazi cha Mungu kikuu ni neno Lake.

Mara nyingi tukiwa kwenye wakati wetu binafsi na Mungu labda katika kuomba au kuabudu au vinginevyo, au tunapokuwa kwenye ibada au faragha zetu za pamoja kama watu wa Mungu, uwepo wa Mungu unaweza kujidhihirisha alafu tukaishia kuuitikia huo uwepo kihisia tu kwa machozi, kulia kwingi, na haleluyah nyingi bila ya kutambua kuwa wakati wowote uwepo wa Mungu unapojidhihirisha, unajidhihirisha kwa kusudi fulani na huo uwepo ili utimize hilo kusudi unadai neno la Mungu lisemwe ili kusudi la Mungu liweze kuachiliwa.

Nataka uone mfano halisia hapa:

Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. (MWA. 1:1, 2 SUV).

Maandiko yanasema nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Cha ajabu pamoja na giza, ukiwa na utupu, Roho wa Mungu alikuwepo lakini alikuwa ametulia juu ya uso wa maji.

Fikiria kama kitabu cha mwanzo kingeishia hapo. Mpaka leo hivi unavyosoma maneno haya kungekuwa na giza, ukiwa na utupu japo uwepo wa Mungu upo. Kuwepo kwa uwepo wa Mungu mahali au hata wewe kuuhisi uwepo wa Mungu sio guarantee ya badiliko lolote kutokea maishani mwako. Uwepo unaweza ukawepo, ukawa unausikia kabisa upako lakini bado ikawa giza, ukiwa na utupu maishani mwako. Mungu yupo, uwepo Wake upo, upako Wake upo lakini umetulia, haufanyi chochote na kwa kuwa umetulia haufanyi chochote kila kitu kitabaki vile vile kama kilivyokuwa. Kinachofanya uwepo wa mungu uingie kazini ni Neno la Mungu tena lililotamkwa.

Lakini ukiendelea kusoma kuanzia mstari wa tatu Mungu akaanza kusema na hapo ndipo mambo yalipoanza kubadilika.

Uwepo wa Mungu bila neno la Mungu hauwezi kubadilisha kitu chochote. Uwepo wa Mungu unadai matamko ya neno la Mungu ili mabadiliko yaweze kutokea. Ni kosa kubwa sana uwepo wa Mungu kujidhihirsha mahali alafu kitu cha pekee ambacho tunafanya ni kubaki tu kuuitikia kihisia kwa kulia, kutokwa tu machozi, kupiga magoti, kusujudu, kulala kifudifudi, kuabudu, kusifu, kucheza na vitu kama hivyo ambavyo watoto wa Mungu hua tunafanya. Uwepo wa Mungu unadai neno la Mungu litamkwe. Hata katika maombi uwepo ukijidhihirisha unadai neno litamkwe ili ufanye kazi. Ni kazi ya Roho Mtakatifu kuhuisha ndani yetu neno la kutamka au maneno ya kutamka toka katika neno la Mungu kila uwepo wa Mungu unapojidhihirisha. Ataweka ndani yako andiko au maandiko na atataka uyatamke au katika maombi au katika kutabiri na kutangaza ili sasa aweze kuingia kazini kulitimiza ulisemalo kwa kuvuviwa Naye.

Nikuonyeshe mfano mwingine:

Mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya BWANA, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la BWANA. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake. Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi. Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno. (EZE. 37:1-10 SUV).

Nataka uone kuwa uwepo wa Mungu ambao hapa unaitwa mkono wa Mungu ulikuwa umemfunika Ezekieli. Nataka pia uone alipelekwa na Mungu mpaka kwenye lile bonde la mifupa mikavu. Nataka pia uone kuwa kwenye lile bonde hakuwa Ezekieli peke yake. Alikuwa pamoja na Mungu pale. Lakini pamoja na uwepo wa Mungu kuwepo ili mifupa iliendelea kuwa mikavu vile vile. Mungu akamwuliza Ezekieli mifupa hii yaweza kuishi, Ezekieli akshindwa kutoa jibu akasema wewe wajua. Mungu akamwelekeza neno la kutamka pale kwenye lile bonde akatamka ili mifupa ikaunga mfupa kwa mfupa mwenzake ikabeba nyama na misuli na ngozi. Sijui unaona kuwa sio uwepo wa Mungu peke yake uliyofanya haya. Ni uwepo wa Mungu na neno la Mungu kwa pamoja ndo viliyafanya haya na neno la Mungu lililosababisha mabadiliko lilitoka katika kinywa cha binadamu. Cha muhimu tu kuona hapa mwanadamu huyu hakusema ayatakayo yeye, alipewa na Mungu ya kutamka. Uwepo wa Mungu ukijidhihirisha mahali popote hapa duniani unadai neno la Mungu toka kwenye kinywa cha mwanadamu ili uweze kufanya kitu. Baadaye lile bonde la mifupa liligeuka kuwa bonde la watu lakini wasio na uhai. Bado Mungu akampa neno pa kuutabiria upepo akautabiria ukaja ukawapulizia hao waliojaa kwenye hilo bonde likainuka jeshi kubwa.

Tunaona wazi Uwepo wa Mungu + Neno la Mungu= Matokeo yanayokusudiwa.

Kumbuka ni mara ngapi maishani mwako uwepo wa Mungu umejidhihirisha alafu hukujua cha kufanya nao kwa hiyo ukapita tu bila kuacha kitu chochote.

Nikuonyeshe tena mfano mwingine:

Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na roho ya BWANA itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. (1 SAM. 10:5-7 SUV).

Sijui unaona ninachoona. Sauli alitakiwa atakapokutana na manabii ajue kuwa Roho wa Mungu atamjilia kwa nguvu lakini sio kule kujiliwa kwa nguvu ndiko kutakako mbadilisha kuwa mtu mwingine ni kile asemacho baada ya kujiliwa kwa nguvu na Roho wa Mungu. Tena anaambiwa ishara hizo zitamthibitishia kuwa Mungu yupo na yeye ila asipofanya kitu hataona matokeo hata kama Mungu yupo. Ndo maana akaambiwa akiona ishara hizo zote afanye aonavyo vema maana Mungu yupo pamoja naye. Usichezee tu uwepo wa Mungu Fanya kitu, sema kitu utaona matokeo.

Moja ya maandiko ambayo watu wa Mungu wanayanukuu vibaya sana inapokuja kwenye maswala ya uwepo ni andiko lifuatalo:

hata ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja ya kumsifu na kumshukuru BWANA nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na vinanda, wakimsifu BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya BWANA, hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa BWANA. (2 NYA. 5:13, 14 SUV).

Tunasema kuwa uwepo wa Mungu unajidhihirsha mpaka mtumishi ameshindwa kulihudumu neno. Ila hawa makuhani hapa hawakuwa wanalihudumu neno. Wao walikuwa wanafanya ibada za utoaji sadaka na dhabihu na kuihudumia madhabahu. Tunatafsiri kuwa uwepo wa Mungu unatosha hatuhitaji neno. How wrong we are. Nimekuonyesha kuwa uwepo wa Mungu bila neno la Mungu hauwezi kufanya lolote. Matokeo yake uwepo unakuja tunabaki kulia, kusujudu, kulala kifudi fudi alafu ukishapita hamna kitu umefanya. Kwanini? Hatukujua tufanye nini na uwepo wa Mungu.

Ona huu mfano wa mwisho:

Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. (LK. 9:32, 33 SUV).

Uwepo wa Mungu ulipojidhihirisha hapa Petro alizungumza maneno huku hajielewi.

Mara ngapi uwepo unajidhihirisha ama katika muda wetu binafsi wa kuomba, kuabudu au vinginevyo au tunapokuwa tumekusanyika kwa pamoja alafu hatujui tufanyaje sie. Naamini baada ya somo hili fupi utakuwa makini zaidi na uwepo wa Mungu unapojidhihirisha.

Asomaye afahamu.

No comments:

Post a Comment