Makanisa matatu yavamiwa Kilimanjaro

Watu wasiojulikana wamevamia makanisa matatu mkoani Kilimanjaro na kuvunja milango, kuharibu mali mbalimbali zikiwemo kompyuta na samani za kanisa na kuiba fedha.

Tukio hilo limetokea katika jimbo la Kilimanjaro Mashariki, Dayosisi ya Kaskazini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Winford Mosha, alisema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana.

Mosha aliyataja makanisa yaliyovunjwa kuwa ni usharika wa Kimbowo, Mseroe  na Mrienyi na kwamba watu hao walivunja kwa lengo la kutafuta fedha.

Mchungaji Mosha, alisema katika usharika wa Mseroe watu hao waliiba shilingi laki mbili na katika sharika nyingine waliharibu mali za kanisa na kuondoka baada ya kukosa vitu vya kuiba.

Hata hivyo, Mosha alisema tukio hilo ni mfululizo wa matukio ya wizi yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi huu katika jimbo hilo ambapo makanisa mengine matatu yalivunjwa na mali zake kuharibiwa vibaya.

Aliongeza kuwa makanisa ambayo yaliyovunjwa ni Msae, Kiruweni na Ashira, hata hivyo katika matukio hayo, pia wezi hao walifanya  uharibifu wa mali mbalimbali za makanisa na kuiba fedha.

Kufuatia tukio hilo, mchungaji huyo aliwataka wakristo pamoja na wachungaji kusimama imara katika maombi ili kuimarisha ulinzi katika maeneo ya makanisa katika kipindi hiki cha sikukuu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema watu hao waliovunja makanisa hayo walikuwa na lengo la kuiba na si vinginevyo.

Maaskofu waijia juu Serikali

Wakristo wamesema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeshindwa kuwasaidia ili waishi kwa amani na utulivu katika nchi yao.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu, wakati akisoma tamko la Maaskofu wa madhehebu ya Kikristo Tanzania katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa lililopo eneo la Jamatini.
Katika tamko hilo alilolisoma kwa niaba ya Maaskofu wote, Kinyunyu alisema kuwa umefika wakati ambao Wakristo wamechoka na vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya waumini wa dini zingine.

“Tatizo ni kuwa Serikali inashindwa kuchukua hatua mapema, makanisa yanachomwa, migogoro inazidi, lakini hakuna hatua zozote ambazo Serikali inachukua katika kunusuru hali hiyo, tumechoka,” alisema.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu 
“ Serikali imeshindwa kuchukua hatua kwa muda mwafaka kwa kila jambo ambalo linatokea kwa Wakristo na hata inapoonyesha kuwa imechukua hatua haionyeshi sana kujali juu ya yale wanayofanyiwa Wakristo. Askofu huyo alisema kuwa matokeo yanayotokea Zanzibar mathalan, Wakristo wanaoishi huko yamewasababishia hofu hivyo wengi kuanza kuvikimbia visiwa hivyo na kukimbilia Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Askofu Kinyunyu, suala la uchomaji wa makanisa hadi sasa limeshindwa kupatiwa ufumbuzi na kila kukicha bado makanisa yanaendelea kuchomwa moto akahoji Serikali kukaa kimya maana yake nini.
Aidha, tamko hilo limeitaka Serikali kuweka utaratibu mzuri na ufafanuzi wa kina kuhusu uchinjaji wa nyama ambao umekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini. “Hapa litolewe tamko kila mtu kwa imani yake achinje mwenyewe siyo kuanza kulaumiana au kumpa haki mmoja akachinja na mwingine akaachwa. Tunaomba sana ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo ili kuondoa mgogoro baina yetu na wenzetu.”
wamekuwa wakifanyiwa, lakini akasisitiza kuwa wanatakiwa kupigana kwa maombi na ndiyo silaha kubwa ya ushindi.

Katika hatua nyingine, wakati Wakristo wakiwa na hofu ya kusherehekea Sikukuu ya Pasaka watu wasiofahamika wamevamia makanisa matatu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini na kuvunja ofisi za wachungaji na wainjilisti.

Watu 40 wahofiwa kufukiwa baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Dar

Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.

Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.
Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege, kweli walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50 ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya ghorofa hilo kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.

Source.mwananchi

Kwaya ya Ambassadors of Christ kutua leo Dar es salaam

Kundi la muziki wa kiroho la Ambassadors of Christ ‘Kwetu Pazuri’ la Kigali, Rwanda linatarajia kutua Dar es Salaam leo kwa ajili ya Tamasha la Pasaka kesho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa kundi hilo pamoja na mambo mengine litazindua albamu yao iitwayo Kaeni Macho katika tamasha hilo litakalofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Tayari mambo yetu yanaenda vizuri na Kwetu Pazuri watawasili Jumamosi wakiwa wamepania kufanya mambo makubwa kwenye tamasha letu,” alisema Msama na kuzitaja nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo kuwa ni Kaeni Macho, Mungu Wangu, Tugireurukundo, Ewe Ndugu, Tuombeane, Umwamini Yesu, Msalaba, Twawona, Okuswala na Huruma.

Alisema kundi hilo limefurahi sana kuja hapa Tanzania na ndiyo sababu wakaipa heshima Tanzania kuzindua albamu yao wakiwa na imani mashabiki wataipenda na kwamba hivi sasa wanatamba na albamu ya Mtegemee Yesu na wamemhakikishia watang’arisha tamasha la mwaka huu.

Alibamu yao hiyo ina nyimbo nane ambazo ni JY’ Ushima Uwite, Mtegemee Yesu, Ndifuza Kugerayo, Iyana Iby’ Isi, Yesu Niwe Mungeri, Parapanda, Abasaruzi na Nenda.

Licha ya kundi hilo, wasanii wengine wa nje ya Tanzania watakaotumbuiza tamasha hilo ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya.

Wasanii wa Tanzania waliothibitisha hadi sasa ni Rose Muhando, Upendo Nkone,  Bonny Mwaitege, Upendo Kilahiro, John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam kesho na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Gosple Festival in South Afrika


TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU SIKUKUU YA PASAKA

KATIKA KUELEKEA SIKUKUU YA PASAKA, INAYOTARAJIWA KUWAADHIMISHWA KUANZIA TAREHE 29 MACHI  HADI  TAREHE 1 APRILI, 2013.  JESHI LA POLISI LINAPENDA KUWAONDOA HOFU WANANCHI WOTE KUWA LIMEJIPANGA KIKAMILIFU KATIKA KUIMARISHA USALAMA WA RAIA NA MALI ZAO KWA KIPINDI CHOTE CHA SIKUKUU NA BAADA YA SIKUKUU, HIVYO WANANCHI WASHEREKEA SIKUKUU  KWA AMANI  NA UTULIVU, PASIPO VITENDO AMA VIASHIRIA VYOVYOTE VYA UVUNJIFU WA AMANI.

2. IKUMBUKWE KUWA, WANANCHI WENYE IMANI YA KIKRISTO NA HATA MADHEHEBU MENGINE HUTUMIA MUDA HUO KWENDA KUABUDU PAMOJA NA MUENDELEZO WA SHEREHE HIZO KWENYE MAENEO MBALIMBALI YA STAREHE. UZOEFU UNAONYESHA KUWA BAADHI YA WATU HUTUMIA KIPINDI HICHO CHA SIKUKUU KUFANYA MATUKIO YA UHALIFU KUTOKANA NA MIKUSANYIKO HIYO YA WATU KATIKA MAENEO MBALIMBALI.

3.JESHI LA POLISI LINAPENDA KUWAONDOA HOFU WANANCHI NA WAUMINI  WOTE KUWA,  ULINZI UMEIMARISHWA KWENYE MAENEO YOTE YA KUABUDIA, FUKWE ZA BAHARI, SEHEMU ZA STAREHE NA MAENEO MENGINE YOTE AMBAYO YATAKUWA NA MIKUSANYIKO MIKUBWA YA WATU.AIDHA, TUNAPENDA KUWATAHADHARISHA WALE WOTE AMBAO WATAKUWA WAKITUMIA BARABARA, KUWA MAKINI KWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI NA HASA KWA MADEREVA KUEPUKA KWENDA MWENDO KASI NA KUTUMIA VILEVI WAWAPO KAZINI.

4 VILEVILE, JESHI LA POLISI LINAWATAKA WANANCHI KUONDOA HOFU NA KUWAPUUZA  WATU WACHACHE AMA KIKUNDI CHA WATU WANAOTUMIA KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU KUWATIA HOFU KWA KUSAMBAZA MESEJI ZA VITISHO KWA WATU MBALIMBALI KWA LENGO LA KUVURUGA AMANI NA UTULIVU KATIKA KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU. KITENDO HICHO CHA KUSAMBAZA MESEJI ZA VITISHO KWA WANANCHI NI UHALIFU KAMA UHALIFU MWINGINE NA WAKIBAINIKA HATUA ZA KISHERIA ZITACHUKULIWA DHIDI YAO.

5. KATIKA KUHAKIKISHA USALAMA KWENYE KUMBI ZA STAREHE, WAMILIKI WA KUMBI HIZO WAZINGATIE UHALALI NA MATUMIZI YA KUMBI ZAO KATIKA UINGIZAJI WA WATU KULINGANA NA UWEZO WA KUMBI HIZO, BADALA YA KUENDEKEZA TAMAA YA FEDHA KWA KUJAZA WATU KUPITA KIASI. VILEVILE, WAZAZI WAWE MAKINI NA WATOTO WAO NA HASA DISKO TOTO, ILI KUEPUKA AJALI NA MATUKIO MENGINE YANAYOWEZA KUSABABISHA MADHARA JUU YAO.

6. JESHI LA POLISI LINATOA TAHADHARI KWA WANANCHI WOTE KWAMBA, WATOKAPO KWENYE MAKAZI YAO WASIACHE NYUMBA WAZI AMA BILA MTU NA WATOE TAARIFA KWA MAJIRANI ZAO, NA PALE WANAPOWATILIA MASHAKA WATU WASIOWAFAHAMU WASIKAE KIMYA BALI WATOE TAARIFA KWA JESHI LA POLISI AU VIONGOZI WAO WA SERIKALI YA MTAA, SHEHIA, KIJIJI AU KITONGOJI ILI HATUA ZA HARAKA ZIWEZE KUCHUKULIWA.

7. MWISHO, NAPENDA KUWAHAKIKISHIA WANANCHI KWAMBA, JESHI LA POLISI LINATEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA KUZINGATIA SHERIA ZA NCHI NA HIVYO HALITAWAJIBIKA KUMWONEA HURUMA AMA UPENDELEO MTU YEYOTE ATAKAYEENDA KINYUME NA SHERIA ZA NCHI.

NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE PASAKA NJEMA.
   
        

      IMETOLEWA NA:
      ADVERA SENSO

MSEMAJI WA JESHI LA POLISI

Askofu Kulola ampa tuzo ya heshima Alex Msama

Kanisa la EAGT hivi karibuni lilimtunuku tuzo Mkurugenzi wa makampuni ya Msama Promotions kwa kutambua mchango wake katika uchangiaji wa maendeleo ya jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhi  tuzo hiyo, juzi Askofu Philemon Phiri wa jimbo la Mikocheni akimwakilisha Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Moses Kulola alisema tuzo hiyo kwa Msama ni utambuzi wa anayoyafanya katika kusaidia jamii.

Askofu Phiri alitumia fursa hiyo kumpongeza Msama kwa  uandaaji wake bora wa matamasha ya Pasaka na kueleza kuwa Mungu amempa ufunuo ambao ni endelevu, naye Msama alishukuru tuzo hiyo na kueleza kwamba tamasha la Pasaka litaendelea kila leo tena kimataifa zaidi hadi duniani.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Moses Kulola
Katika hatua nyingine mwimbaji nguli wa muziki wa Injili wa Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi nchini Kenya, amesema atatumia tamasha la pasaka kutambulisha wimbo wake  wa Kiti Chako uliopo kwenye albamu yake mpya ya Sifa za Mungu.

Akizungumza na Pata Habari, baada ya kuwasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kuhudhuria tamasha la pasaka linalotarajiwa kufanyika Jumapili hii katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam alisema, atautambulisha wimbo huo ambao una ujumbe mzito wa neno la Mungu.

Kwa mujibu wa Solomoni Mukubwa albamu yake hiyo ni zaidi ya nyingine alizowahi kurekodi hii kwa sababu ameimba ushuhuda wa maisha yake  baada ya kupata matatizo ya kukatwa  mkono  wake.
“Nashukuru  kupata  tena  nafasi  ya kuwa mmoja wa waimbaji kwenye tamasha la mwaka huu, nimejiandaa vya kutosha mashabiki wafike kwa wingi kupata ujumbe mzito wa neno la Mungu pia nitatambulisha wimbo wangu mpya siku hiyo” alisema Mkukubwa.

Alisema albamu yake hiyo inanyimbo saba, ambazo ni Kiti chako, Shukrani ya punda, Nitaishi wakitazama, Habari njema, raha yangu, sijafika, Sifa za mungu, Nimewasamehe wote.

Kwa upande wa Faraja Ntaboba, alisema kauli mbiu ya tamasha la pasaka la mwaka huu inayosema kuwa ‘Amani na Upendo’ imempa moyo sana,  inagusa Afrika nzima kwa kuwa  kuna watu wanalia  kwa kupoteza  amani.

Aidha  mwimbaji  huyo  alitoa  wito  kwa  mashabiki  wa tamasha hilo linalotarajia kufanyika mikoa mitano, kuwa wasisherehekea tu bali waje wakijua amani inatafutwa,  aliahidi kufanya mambo makubwa siku ya Jumapili.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 Uwanja wa Samora mkoani Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Source:Fullshangwe

Pengo: Polisi nchini wanafuga uhalifu

 Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kadhalika kiongozi huyo alihoji ulipofikia upepelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita huku akisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”

Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Pasaka.

“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao, viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na kuongeza:

“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”

Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”


Aliongeza: “Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu yeyote anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama mambo yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko la amani.”

Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa chimbuko la kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za Wakristu na Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili ambayo yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.

Alisema pande zote mbili watu wakitaka kujadiliana ni lazima kila upande uwe tayari kujadiliana na kupokea ukweli sambamba na kusema ukweli na siyo kupotosha ukweli kwa masilahi binafsi.

“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande wa pili una nia njema, lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande wa pili una nia njema, lakini kinyume na hapo itakuwa bure na kudanganyana na mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna watu watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina jukumu la kuhakikisha raia wanakuwa salama.

“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya Padri Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli ikatokea Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama nitaambiwa nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.

Polisi wanena

Msemaji Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo cha Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo jukumu lao kujua chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie wanaohusika ili kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza kinachoendelea upelelezi utakapokamilika,” alisema Senso.

Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo, watupe ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.

Pia Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Mwanakwerekwe.

Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa katika ugomvi wa kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita walijeruhiwa vibaya kwa mapanga.

Source:Mwananchi

Waimbaji wa Muziki wa Injili kutoka Nchi jirani kwa ajili ya Tamasha la Pasaka waanza kuingia Nchini


Mwimbaji wa nyimbo za injili, Solomon Mukubwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi yake katika tamasha la Pasaka 2013.


Mwimbaji wa nyimbo za injili, Faraja Ntaboba akiimba kwa hisia moja ya nyimbo zake mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu inayoratibu Tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya tamasha hilo.

Mapato ya Tamasha la Pasaka kujenga kituo cha yatima Dar

Waratibu wa tamasha la Pasaka litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam hapo Machi 31, wamepanga kautumia sehemu ya mapato ya kiingilio kujenga kituo cha watoto yatima kama ishara ya shukrani kwa jamii.Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamatimaalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, alisema kituo hicho kitakachokuwa chini ya kampuni ya
Msama Promotions kitajengwa eneo la Pugu.Alisema uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kuwapa faraja watoto yatima ambao nao wana haki ya kupatiwa matunzo na mahitaji muhimu katika makuzi yao ikiwemo elimu katika kujenga taifa bora la kesho.
 
 Mwenyekiti wa Maandalizi ya Tamasha la Pasaka Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu maandalizi ya tamasha hilo lenye kauli
mbiu ya Amani na Upendo. Kulia ni Mdau wa muziki wa Injili, Mcharo Mrutu.
“Tangu kuasisiwa kwa tamasha la Pasaka mwaka 2000, tumekuwa tukirejesha sehemu ya mapato ya viingilio kwa jamii kwa njia ya misaada kwa yatima, wajane na walemavu, lakini safari hii tumeona twende zaidi ya hapo kwa kujenga kituo cha watoto,” alisema.Alisema lengo ni kujenga kituo hicho cha kisasa ambapo kama mipango itakwenda vizuri, kitakamilika kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwani wangependa ndiye akizindue kwa kutambua mchango wake kwa tamasha hilo.
 
“Mwaka 2011, Rais Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi wa tamasha letu pale Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.“Kitendo cha Rais kuacha kazi nyingi na kuja kutuunga mkono kwenye shughuli hii ya kiroho, kwetu ni jambo kubwa sana ambalo kamwe hatutalisahau, hivyo tumeona tumpe heshima hiyo ya kuzindua kituo hicho akiwa bado madarakani,” alisisitiza.
 
 
 Msama ametoa wito kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za kampuni yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo kueneza injili ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.Kuhusu waimbaji, Msama alisema wale wa nje wataanza kuwasili wiki hii na kuongeza kuwa hadi kufikia Ijumaa, waimbaji wote  watakuwa wamefika tayari kwa tukio hilo mbalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Aliongeza kuwa idadi ya waimbaji imeongezeka baada ya kujitokeza kwa mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ntutuma kutoka nchini Kenya.Baada ya kishindo cha tamasha hilokutikisa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, itakuwa zamu ya Dodoma,

Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya mashambulizi kuhimishwa mkoani Mara.