Makanisa matatu yavamiwa Kilimanjaro

Watu wasiojulikana wamevamia makanisa matatu mkoani Kilimanjaro na kuvunja milango, kuharibu mali mbalimbali zikiwemo kompyuta na samani za kanisa na kuiba fedha.

Tukio hilo limetokea katika jimbo la Kilimanjaro Mashariki, Dayosisi ya Kaskazini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Winford Mosha, alisema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana.

Mosha aliyataja makanisa yaliyovunjwa kuwa ni usharika wa Kimbowo, Mseroe  na Mrienyi na kwamba watu hao walivunja kwa lengo la kutafuta fedha.

Mchungaji Mosha, alisema katika usharika wa Mseroe watu hao waliiba shilingi laki mbili na katika sharika nyingine waliharibu mali za kanisa na kuondoka baada ya kukosa vitu vya kuiba.

Hata hivyo, Mosha alisema tukio hilo ni mfululizo wa matukio ya wizi yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi huu katika jimbo hilo ambapo makanisa mengine matatu yalivunjwa na mali zake kuharibiwa vibaya.

Aliongeza kuwa makanisa ambayo yaliyovunjwa ni Msae, Kiruweni na Ashira, hata hivyo katika matukio hayo, pia wezi hao walifanya  uharibifu wa mali mbalimbali za makanisa na kuiba fedha.

Kufuatia tukio hilo, mchungaji huyo aliwataka wakristo pamoja na wachungaji kusimama imara katika maombi ili kuimarisha ulinzi katika maeneo ya makanisa katika kipindi hiki cha sikukuu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema watu hao waliovunja makanisa hayo walikuwa na lengo la kuiba na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment