‘Tumegoma kupokea misaada ya waabudu shetani’

Mmiliki na mwanzilishi wa kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na yatima cha Hananasif Orphanage Centre (HOC) Bw. Hezekia Mwalugaja, amesema kituo chake kimekataa baadhi ya misaada yenye masharti ya kishetani, inayolenga kuwaunganisha na madhabahu ya kisheni.

Akiongea na moja la Kikristo katika Mahojiano maalumu, mara baada ya kupokea msaada wa vyakula wenye thamani ya Shilingi 700,000 iliyotolewa na kanisa la EAGT City Centre, linaloongozwa na Mchungaji Flarian Katunzi, Bw. Mwalugaja, alisema kuwa  anamshukuru Mungu kuwainua watakatifu kujitolea kufanya kazi pamoja na kituo hicho katika mazingira safi na yenye kumpa Mungu utukufu.



Alisema kuwa kituo hicho kina zaidi ya watoto 100, 98 miongoni mwao wakiwa wanafunzi wa Sekondari ambao wanatunzwa na kusomeshwa na kituo, huku wanafunzi wanne wakiwa katika shule za msingi.

Awali akishukuru mbele ya maelfu ya waumini wa kanisa hilo waliochanga fedha kwa ajili ya kununulia chakula cha msaada kwa watoto hao, alisema kuwa kwake huo ni muujiza kwani Mungu alisema na Mtumishi wake, Mch. Katunzi na wauminini wake wakachanga chakula hicho kwa ajili ya watoto yatima kwa wakati huu ambao wamekataa misaada mingi ya wafadhili kutoka Magharibi.

Akifafanua alisema: “Wafadhili tuliowakatalia kupokea mamilioni ya misaada yao walitupa masharti magumu, ikiwa ni pamoja na kuacha kuendesha ibada na maombi, kituoni hapo na kufanya mambo mengine ambayo ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Ni mambo ya kishetani kabisa.”

Kisha aliendelea: “Miongoni mwa mambo ambayo wafadhili hawataki ufundishe kinyume chao ni pamoja na ndoa za jinsi moja, kuwa ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na ni dhambi. Wanataka ufundishe mafundisho ya mseto ya dini zote. Kwetu tulikataa kwa kuwa hiyo sio imani yetu.”

“Mkazo mkubwa kwenye kituo chetu ni kuwafunzisha watoto wale jinsi ya kumtegemea Mungu na kuishi maisha matakatifu, tunawaandaa kuwa vyombo vya kumtumainia Mungu, lakini wafadhili wa kimagharaibi hawataki kabisa mafundisho ya dini kituoni na hilo ndilo sharti kubwa la kupokea misaada yao.”

Alisema kuwa wamefikia mahali pa kuamua kumtumainia Mungu na kuwaambia misaada ya masharti ya kufundisha watoto ndoa za jinsia moja na dini za mseto baina ya madhehebu yote, ni  ibada ya Mungu mwingine na wao hawako tayari kuifanya.

Akikabidhi misaada hiyo muda mfupi kabla ya ibada kuanza, Mchungaji Katunzi alisema kuwa kanisa lake lina program ya kuigusa jamii kwa Neno na tendo, hivyo waliamua kujitoa, ili kuwasaidia watoto hao waliopoteza wazazi na walezi.

Kiongozi huyo alisema kuwa michango hiyo ilitolewa na waumini wa kanisa hilo kwa ajili ya kuwasaidia wenzao. Aliwashukuru wana EAGT City Centre, kwa moyo wao wa huruma walionyesha kuwa kujitoa kusaidia watoto hao.

No comments:

Post a Comment