Askofu wa EAGT apotea, hofu yatanda

Askofu wa Kanisa la Evangelism Assemblies of God Tanzania (EAGT) anayeishi mjini Makambako katika Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe, Lomanus Lukosi (60), amepotea katika mazingira ambayo yamezua utata kutoka kwa wananchi wakiwamo waumini wa kanisa hilo.

Tukio hilo limetokea wakati ambao kuna hofu juu ya usalama wa viongozi wa dini kufuatia matukio ya kushambuliwa kwao na wengine kuuawa Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo chanzo cha habari hii kimezipata kutoka Makambako na kuthibitishwa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo, askofu huyo ambaye anasimamia makanisa hayo yaliyopo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, alipotea tangu Alhamisi wiki iliyopita.
Askofu Mkuu Msaafu wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Moses Kulola, alipotafutwa na chanzo cha habari hii jana kuelezea tukio hilo, simu yake ilipokelewa na mtu ambaye alikataa kumpelekea huku akisema kuwa askofu huyo hawezi kuzungumzia suala hilo.

“Suala la kupotea askofu wa Makambako Askafo Mkuu hawezi kulizungumzia kwa sababu yeye yupo Dar es Salaam na tukio limetokea Makambako,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Nganyani, alipoulizwa, alithibitishwa kuwapo kwa taarifa za kupotea kwa Askofu Lukosi ambazo alisema ziliripotiwa katika kituo cha polisi Makambako.

Kamanda Ngonyani alisema kuwa Alhamisi iliyopita, askofu huyo aliondoka nyumbani kwake akiwa peke yake bila kuwasiliana na familia yake mahali alipokuwa anakwenda.

Alisema pamoja na kutokumuaga yeyote, mke wake hakuwa na wasiwasi kwa sababu alifahamu huenda alikwenda kanisani kusali.

Kamanda hiyo aliongeza kuwa mke wa askofu huyo alianza kupata wasiwasi baada ya mumewe kutorejea nyumbani siku hiyo na ndipo alipokwenda kutoa taarifa polisi.

Kamanda Ngonyani alisema baadaye uchunguzi ulipoanza kufanywa na polisi, mmoja wa waumini wa kanisa hilo alitoa taarifa kuwa amepigiwa simu na askofu huyo kuwa yupo katika maombi ya kufunga kwa ajili ya kuliombea kanisa hilo.

Alisema juzi (Jumamosi), askofu huyo alimtumia ujumbe mfupi wa maneno mke wake akimweleza kuwa asiwe na wasiwasi kuna sehemu amejificha kwa ajili ya maombi.

Kamanda Ngonyani alisema kutokana na utata huo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na wataalam wa simu za mkononi ili kufahamu alikojificha askofu huyo.

“Tumejaribu kumpigia simu, lakini hadi jana askofu huyo simu yake ilikuwa haipatikani, kwa hiyo tunasaidiana na wataalam wa simu kujua aliko,” alisema Kamanda Ngonyani.

Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linaamini kuwa askofu Lukosi hajapotea bali amejificha sehemu anayoijua yeye kwa ajili ya maombi na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika.

Hivi karibuni, yalitokea matukio ya kushambuliwa kwa viongozi kadhaa wa dini.

Moja ya matukio hayo ni kuuawa kwa kupigwa risasi Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Minara Miwili, visiwani Zanzibar.

Mbali na Padri Mushi, viongozi wengine wa dini waliouawa ni Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Mathayo Kachila, mkoani Geita na Imamu wa Msikiti wa Mwakaje, eneo la Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Sheikh Ali Khamis Ali.

Wapo pia waliojeruhiwa akiwamo Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar, aliyejeruhiwa kwa risasi na Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, aliyemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Mbali na mashambulizi hayo dhidi ya viongozi wa dini, makanisa zaidi ya 25 yamekwisha kuchomwa moto katika kipindi cha mwaka mmoja nchini kote.

 Source: Nipashe