Kwaya ya Ambassadors of Christ kutua leo Dar es salaam

Kundi la muziki wa kiroho la Ambassadors of Christ ‘Kwetu Pazuri’ la Kigali, Rwanda linatarajia kutua Dar es Salaam leo kwa ajili ya Tamasha la Pasaka kesho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa kundi hilo pamoja na mambo mengine litazindua albamu yao iitwayo Kaeni Macho katika tamasha hilo litakalofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Tayari mambo yetu yanaenda vizuri na Kwetu Pazuri watawasili Jumamosi wakiwa wamepania kufanya mambo makubwa kwenye tamasha letu,” alisema Msama na kuzitaja nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo kuwa ni Kaeni Macho, Mungu Wangu, Tugireurukundo, Ewe Ndugu, Tuombeane, Umwamini Yesu, Msalaba, Twawona, Okuswala na Huruma.

Alisema kundi hilo limefurahi sana kuja hapa Tanzania na ndiyo sababu wakaipa heshima Tanzania kuzindua albamu yao wakiwa na imani mashabiki wataipenda na kwamba hivi sasa wanatamba na albamu ya Mtegemee Yesu na wamemhakikishia watang’arisha tamasha la mwaka huu.

Alibamu yao hiyo ina nyimbo nane ambazo ni JY’ Ushima Uwite, Mtegemee Yesu, Ndifuza Kugerayo, Iyana Iby’ Isi, Yesu Niwe Mungeri, Parapanda, Abasaruzi na Nenda.

Licha ya kundi hilo, wasanii wengine wa nje ya Tanzania watakaotumbuiza tamasha hilo ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya.

Wasanii wa Tanzania waliothibitisha hadi sasa ni Rose Muhando, Upendo Nkone,  Bonny Mwaitege, Upendo Kilahiro, John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam kesho na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

No comments:

Post a Comment