Papa Francis I akataa vitu vya kifahari

Siku chache baada ya kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewashangaza wengi mengi kwa kukataa kuvaa viatu vya kifahari na msimamo wake kuwekwa wazi kuwa hatavumilia makasisi watakaotenda uovu.

Tayari, Papa Francis ameelezwa kuwa kiongozi asiyetaka makuu, mhafidhina na mtu ambaye hataweza kubadili mengi katika kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2 duniani.

Katika siku mbili za uongozi wake, Papa Francis amelithibitisha hilo kwa kutokea hadharani akiwa amevaa viatu rahisi, vyeusi na kuachana na vyekundu vya kifahari vilivyopendelewa na mtangulizi wake, Benedict VXI.

Katika uongozi wake, siku zote Papa Benedict, alivaa viatu vyekundu vilivyotengenezwa kwa mkono, jambo ambalo Papa Francis anaonekana kuachana nalo.

Watu walio karibu naye Papa Francis, wanaeleza kuwa kabla ya kuondoka Buenos Aires, Argentina kwenda Rome, Kardinali Jorge Mario Bergoglio, kama alivyojulikana awali, alivaa viatu rahisi vya rangi nyeusi, na kuwafanya marafiki zake, wakiwamo mapadri kutaka kumnunulia viatu vingine vipya.

“Siku ile aliyoondoka mjini Buenos Aires kuelekea Rome kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi wa Papa (conclave), marafiki zake walimpa zawadi ya viatu. Yeye, siku zote amekuwa akitokea hadharani akiwa amevaa nguo rahisi, viatu vya kawaida,” walieleza mapadri hao kutoka Amerika Kusini walipozungumza na Kituo cha Redio Vatican.

Juzi Ijumaa alipokutana na makardinali 106, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76, licha ya kuonyesha uso wa furaha na kuwatania aliwaonya makardinali hao kuhusu wajibu wao kama viongozi wa kanisa maeneo mbalimbali duniani akiwataka kutosahau kuwa hawarudi kwenye ujana.

Katika ukumbi wa Sala Clementina, ulioko Vatican Papa Francis pia aliwataka makardinali hao wakiwamo waliomchagua kuwategemea zaidi vijana aliosema ndio nguzo kuu muhimu ya ustawi wa Kanisa Katoliki, huku aliwashauri makardinali kusaka njia sahihi ya kueneza Ukristo pande zote za uso wa dunia katika karne ya 21.

Aidha, alimsifu mtangulizi wake, Papa Benedict kwa uamuzi wa kijasiri wa kustaafu, akieleza kuwa ni uamuzi wa busara, wenye kuonyesha ukomavu na kuwataka wasichoke kuiga matendo mema.

Source Mwananchi

No comments:

Post a Comment