Papa Benedict XVI aachia madalaka rasmi.

Kanisa Katoliki Ulimwenguni kwa sasa halina Papa. Hii ni baada ya ya kiongozi wake, Baba Mtakatifu Benedict XVI, jana kung’atuka rasmi na kuwaaga makardinali mjini Vatican.

Papa Benedict XVI, aliwaaga makardinali baada ya ibada yake ya juzi ya kuwaaga maelfu ya waumini wa kanisa hilo katika viwanja vya Mtakatifu Petro na kuzungumzia uongozi wake huku akieleza kwamba ulikuwa na nyakati za dhoruba na furaha.

Papa Benedict XVI aliwahutubia maelfu ya Wakatoliki katika mkesha wa kihistoria wa kustaafu kwake kama kiongozi wa Wakatoliki bilioni 1.2 kote ulimwenguni.

Mbele ya umati wa watu, Papa Benedict XVI, alizungumzia nyakati za mapambano na pia za furaha wakati wa hotuba yake ya mwisho ya umma katika viwanja vya Mtakatifu Petro.


Katika ujumbe wake binafsi usio wa kawaida, alisema: "Kumekuwa siku nyingi za nuru, lakini pia nyakati za dhoruba kali.”

Jana, Papa alizungumza na makardinali na kuwaaga kwa kuwakumbatia mmoja mmoja, kisha kuondoka kwenye gari dogo kuelekea kwenye chopa.

Papa alizunguka anga la Vatican kwa takribani dakika 25 akiwaaga Wakatoliki akiwa kwenye chopa iliyoandikwa Republica Italiana kabla ya kwenda kuishi katika makao yake mapya katika kasri ya Gandolfo.

Kuondoka kwa Papa kumeacha kiti cha Petro wazi na hivyo Wakatoliki duniani kote wanasubiri kwa hamu kiongozi mpya ambaye atakuwa na majukumu mazito kama kushughulikia kashfa ya unajisi wa watoto pamoja na ya rushwa inayolikabili kanisa hilo.

Wakati watu nje ya kanisa wakitazama utaifa na ukabila wa Papa ajaye, makardinali wa ngazi ya juu kabisa wa Kanisa Katoliki wanatazama mtu mwenye maono makubwa ya kimataifa na Kanisa.

Hivi sasa makardinali walio na umri wa chini ya miaka 80 ambao ndiyo wenye sifa za kupiga kura huitwa kwa ajili ya mkutano wa makardinali na hupiga kura za siri kila mmoja.

Makardinali 118 kutoka duniani kote ambao wana sifa za kumchagua Papa ajaye wamewasili Vatican. Takwimu za Vatican zinaonyesha kwamba zaidi ya nusu yao wanatoka mataifa ya Ulaya. Hata hivyo, watu wengi wanatazamia kwamba Papa ajaye atoke Afrika au Amerika Kusini.

Makardinali 118 wanaopiga kura, 28 kati yao wanatoka Italia, 34 wanatoka kwingineko Ulaya, 19 wanatoka Latin Amerika, 14 wanatoka Marekani na Canada, 11 kutoka Asia, 11 kutoka Afrika na mmoja wa Australia.
Msemaji wa Vatican, Padre Federico Lombardi, alisema Papa mpya atapatikana kabla ya Sikukuu ya Pasaka.

Wakiwa Vatican, makardinali hawaruhusiwi kuondoka wala kuzungumza na mtu yeyote nje ya mkutano huo hadi jukumu la kumchagua Papa mpya litakapokamilika.

Viongozi hao hupiga kura na ikiwa mshindi hakupatikana, watarudia tena na tena. Kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Hayati Papa John Paul II, makardinali wanaweza kupiga kura hata mara nne kwa siku ya pili na ya tatu.

Kwa siku ya tatu, kama bado Papa atakuwa hajapatikana, makardinali hupumzika kwa siku moja kwa ajili ya sala, majadiliano na maonyo kutoka Kardinali mwandamizi. Siku hiyo hutoa ahueni kwa makardinali.

Papa John Paul II aliamua kurahisisha zoezi hilo kama itafikia hatua hiyo, alieleza kwamba kura zipigwe kwa kuzingatia kardinali anayekuwa amepata kura nyingi na mshindi atapatikana kwa kupata asilimia 51 ya kura zote. Hapo mchuano utakuwa baina ya makardinali wawili wanaokuwa wamepata kura nyingi zaidi hapo awali.

NINI NAFASI YA AFRIKA,  AMERIKA KUSINI?
Pamoja na kwamba waumini wa Kikatoliki wameongezeka sana barani Afrika na hata Amerika Kusini, hiyo haiwezi kuwa hoja ya kufanikiwa kutoa Papa.

Ikiwa takwimu zitazingatiwa, basi Kanisa Katoliki halina cha kuhofia barani Afrika, kwani katika mwaka 2011 idadi ya waumini wa kanisa hilo kote barani humo ilionekana kuongezeka kwa zaidi ya milioni sita na kufikia watu milioni 18.

Taarifa zinaonyesha kwamba mafunzo ya upadre kwa kizazi kipya yanaonekana kuongezeka bila kikomo wakati nchi zinazokabiliwa na mizozo kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) au Sudan Kusini, mara nyingi mapdri wakikatoliki wanajikuta wakiwa na sauti kuliko wajumbe wa serikali.

Hata hivyo, hali ni tofauti barani Ulaya, ambako idadi ya viongozi wa kidini katika kanisa hilo imekuwa ikipungua kiasi kwamba Kanisa Katoliki barani Afrika linabidi kuchangia kutoa mapdri kuwapeleka barani Ulaya.
Baadhi ya mapadri wanasema kwamba idadi kubwa ya waumini siyo hoja, hoja ni ubora wa mafunzo ya dini hiyo.

Papa Benedict  XVI aliwahi kukiri juu ya ukweli kuhusu hoja hiyo pale alipoitisha mkutano mkubwa kabisa wa Maaskofu wa Kikatoliki kutoka barani Afrika mjini Roma mwaka 2009. Maaskofu 197 walishiriki mkutano huo uliojadili dhima ya kanisa hilo barani Afrika.

Mkutano huo ulikuwa wa pili wa aina yake katika historia ya kanisa hilo baada ya uliotangulia ulioongozwa na Papa John Paul II.

Papa Benedict XVI, aliwaasa zaidi viongozi hao wa kidini barani Afrika kuchukua jitihada kama Kanisa kuyatatua matatizo mengi ya bara la Afrika kuanzia umaskini hadi mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, lakini alishindwa kutoa majibu juu ya vipi hilo lifanyike badala yake alihimiza zaidi juu ya Kanisa kuchukua jukumu la kuuelimisha umma.

Hata hivyo, Padri Pete Henriot ambaye amefanya kazi barani Afrika kwa takriban miaka 25, anasema sura ya Kanisa Katoliki duniani inakaribia kabisa kubadilika na kuwa ya Kiafrika.

Kanisa Katoliki barani Afrika kwa upande mwingine linakabiliwa na changamoto chungu nzima, hivyo kazi kubwa inamsubiri kiongozi mpya wa kanisa hilo duniani.

Aidha, changamoto nyingine inayolikabili kanisa hilo barani Afrika ni ushindani kutoka makanisa mengine ya kiinjili ambayo yanaongoza pia katika kutoa huduma za afya na elimu.

Suala la matumizi ya kondomu ambalo baadhi katika kanisa hilo wanapendekeza Papa ajaye achukue hatua za kuunga mkono hatua ya kushajilisha mtengamano miongoni mwa tamaduni mbalimbali.

Waangalizi wengi wa masuala ya kidini barani Afrika na nje, wanatarajia kwamba suala la matumizi ya mipira hiyo pamoja na njia za kupanga uzazi, Papa mpya hatatofuata na nyayo za Papa Benedict XVI.

Source:Nipashe

No comments:

Post a Comment