Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani awa mchungaji Anglikana.



Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani
 Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani ametawazwa kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar na kusema ameshangazwa na mashambulizi ya tindikali dhidi ya viongozi wa dini Visiwani humo.

Akizungumza na waaandishi wa habari mara baada ya kutawazwa ndani ya Kanisa la Anglikana la Minara Miwili Mjini Unguja, Jaji Ramadhan amesema vitendo vya hujuma vinavyofanywa dhidi ya viongozi wa dini na Serikali ni kinyume na utamaduni wa Zanzibar.

Alisema Wakristo na Waislamu Zanzibar kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kama ndugu bila ya kubaguana kwa sababu za itikadi ya dini licha ya Waislamu kuwa asilimia 95.

Hata hivyo, alikumbusha kuwa wakristo wana mchango katika harakati za ukombozi wa Zanzibar, ambapo idadi kubwa ya waumini wake walianzisha Chama cha African Association mwaka 1935, ambapo rais wake wa kwanza alikuwa hayati, Mzee Augustino Ramadhan na baadaye akafuata hayati  Mzee Abeid Amani Karume.

“Vitendo vya watu kumwagiwa tindikali vinanishangaza, sababu halisi siifahamu, najiuliza haya yametokea wapi, siyo jambo jema wala siyo sifa ya Zanzibar tokea enzi na enzi,” alisema.

Alisema wakati umefika na kuwataka viongozi kuwa mstari wa mbele kukemea matukio ya hujuma za tindikali na uhalifu mwingine ikiwemo mashambulizi ya kutumia silaha za moto na watu kupotezewa maisha.

Jaji Augustino amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na Tanzania, Brigedia Jenerali wa JWTZ pia amewahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mahakama ya Afrika Mashariki, ambapo amesema kazi ya sheria hazitofautiani na kazi za kiroho kwa vile zote zinahitaji utende haki na kutimiza wajibu upasavyo. 

Kwa upande wake Askofu Philip Baji wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha Dodoma, alisema huu ni wakati mwafaka kwa Serikali kuwalinda viongozi wa dini bila ya kujali tofauti ya madhehebu yao kutokana na kukithiri kwa vitendo vya hujuma.

Source:Mwanachi

No comments:

Post a Comment