Kanisa lililopigwa bomu Arusha lazinduliwa chini ya ulinzi mkali

Balozi wa Papa, Askofu  Padilla, akikata utepe wa kuzindua Kanisa la Mtakatifu Joseph Arusha jana.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Hatimaye  Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti, jijini Arusha, lililopigwa bomu Mei 5, mwaka huu na kuahirishwa uzinduzi wake, limezinduliwa jana na Balozi wa Papa na Mwakilishi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Fransisco Padilla.

Kabla ya uzinduzi huo, ibada hiyo ilianza kwa kubariki makaburi matatu ya Regina Laizer (50), James Kessy (16) na Patricia Assey (10), ambao wote waliuawa katika tukio hilo.

Uzinduzi huo ulikuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi waliokuwa wametanda kuzunguka kanisa na wengine wakiwa juu ya paa.

Akizungumza wakati wa mahubiri Askofu Padilla alisema mara baada ya tukio hilo alikwenda kwa Papa, ambaye alimwamuru arudi Tanzania kuwapa pole waumini wote waliofikwa na tukio hilo.

“Sasa nawapa pole sana na amenituma nije kupatakasa mahali hapa, pawe patakatifu kwa ajili ya utoaji wa huduma za kimungu,” alisema.

Aliwaasa waumini kuwa na umoja na mshikamano katika kujenga kanisa, ili kuwe na matunda mazuri kwa kanisa.

“Nasema hivi sababu nitafurahi kuja kuona watoto wenu wametoka hapa kuwa watawa, masisita na mapadre,  wa kiongoza ibada hapa, nitafurahi sana,” alisema.

Alisema kuwa kanisa hilo baada ya kuzinduliwa litumike kuwa msingi wa kusaidia wasio na uwezo na siyo kulitumia jengo hilo kwa njia isiyofaa wala kuleta matunda kwa kanisa.

Alisema wanapopata majaribu ya shetani, wasikate tamaa, kwani hawana budi kuimarisha imani zao, kwa kuwa shetani hana mamlaka ya kuangusha nguvu za Mungu.

Alitaka kanisa hilo litumike katika kuibua vipaji vya miito na kuwahubiria wengine juu ya wokovu ili nao waokoke.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu, aliyekuwa mwenyeji wa Balozi huyo, alisema kuwa ni vema waumini wakajua kuwa mipango ya Mungu, haiwezi kuangamizwa na shetani, hivyo walishindwa kuzindua kwa wakati ule uliopangwa kwa sababu ya vikwazo vya shetani na sasa wamemshinda shetani na wamezindua kanisa hilo.

“Mjuwe wazi mpango wa Mungu hauwezi kuangamizwa na mtu yeyote na ndio sababu leo tupo hapa tukiweka wakfu katika kanisa letu na kubariki makaburi ya waumini wetu waliofia imani yao ya katoliki,” alisema.

Alisema hata katika Biblia inasema wakati ule Mfalme Herode alipanga angamiza watoto wote wa kiume ili amwangamize Yesu, lakini alishindwa na ndivyo hata leo shetani atajiinua na atashindwa.

Askodu Lebulu alisema waliofariki kwa kupigwa na bomu kanisani hapo, walifariki, lakini waliobaki wamepata uponyaji na nguvu ya maombi zaidi ya hapo mwanzo kabla ya tukio hilo.

Askofu Lebulu aliongozana na Askofu wa Jimbo la Mahenge, Agapite Ndorobo na Askofu Padilla, kwenda kwenye makaburi yaliopo mbele ya kanisa hilo na kuyanyunyuzia maji kama njia ya kuyabariki.

Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Jubilei ya Jimbo la Arusha, ambayo kilele chake, kinatarajia kufanyika leo katika kanisa la mtakatifu  Theresia wa Mtoto Yesu na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na Maaskofu na Mapadre mbalimbali toka ndani na nje nchi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment