KKKT yazindua mtambo kuzalisha nishati mbadala

Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), limeanza kupambana na uharibifu wa mazingira kwa kuzindua mtambo wa kuzalisha nishati mbadala ya kinyesi cha wanyama wilayani Serengeti mkoani Mara.

Akizungumza baada ya kuzindua mtambo huo, Askofu wa dayosisi ya Mara, Maiko Adam, alisema mtambo huo, utawasaidia wananchi kuyatunza mazingira kwaajili ya kuepuka uharibifu unaoendelea katika sehemu nyingi hususani katika hifadhi ya wanyama pori nchini.

Askofu Adam alisema Serengeti imepewa kipaumbele kwaajili ya kutunza hifadhi ya wanyama na mazingira ili kuleta ustawi wa vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema kufanya hivyo ni moja ya kuzuia uharibifu wa mazingira unaoendelea katika sehemu mbalimbali  nchini, ambao unaweza kuleta athari kubwa ya kutokea kwa ukame na kupoteza rasilimali zilizopo kama wanyama.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wilaya ya Serengeti, Guddy Pamba, alisema kuzinduliwa kwa mradi huo kutasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaleta uharibifu wa mazingira na kusababisha ukame.
Aliwataka wakazi wa eneo hilo kutunza mradi huo ili kuhifadhi mazingira.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment