Aliyegoma kupachikwa No. 666 akimbilia kortini


Mwanafunzi wa masomo ya Sayansi, Andrea Hernandez, (15) amezua kizaa zaa katika shule ya  John Jay High School, baada ya kugoma kupachikwa chip maalumu ya utambuzi, inayowawezesha walimu na viongozi wa shule kumuona na kumfuatilia kwa kila kitu anachofanya, akidai kuwa kifaa hicho ni alama ya mnyama au nambari ya Mpinga Kristo iliyotajwa katika Biblia kwenye kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura ya 13.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, uongozi wa wilaya ilipo shule hiyo, huko Texas nchini Marekani, umepitisha sheria ya wanafunzi wote kupachikwa chip hizo ili kukabiliana na tatizo la utoro madarasani, lakini kijana huyo akiungwa mkono na wazazi wake walikataa kukubaliana na sheria hiyo kwa madai kuwa kifaa hicho kinachorusha mawimbi ya sauti (RFID) kinaumiza hisia za imani yake ya dini.

Wote Andrea na baba yake, Bw. Steven Hernandez, waliueleza uongozi wa shule kuwa hawana shaka hata kidogo kuwa kifaa hicho ni cha Mpinga Kristo na kwa kuwa kina maelezo ya utendaji ule ule wa Mpinga Kristo, kama ilivyoelezwa katika Ufunuo wa Yohana.

Msichana huyo na  mzazi wake walipokataliwa na uongozi wa shule na ule wa wilaya waliamua kwenda Mahakama ya Mwanzo kufungua shauri  na kesi ikaendeshwa haraka haraka, lakini wakashindwa.

Hata hivyo hawakukata tamaa waliamua kukata rufaa katika mahakama ya juu na uamuzi ulitarajiwa kutolewa wiki chache zilizopita, ingawa warufani waliahidi kuendelea mbele ikiwa Jaji asingetoa hukumu upande wao.

Mradi wa kuwapachika chip wanafunzi wote unajulikana kama  “Student Locator Project,”  unalenga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaotulia shuleni na vyuoni badala ya kuzurura mitaani.
Mradi huo unalenga kuhudumia wanafunzi  4,200  katika shule za John Jay High School na Jones Middle School, ambao wanapaswa kuvaa  “SmartID” ambayo imepachikwa kadi ya mawimbi ya  RFID.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la  San Antonio Express, mzazi wa binti huyo,  Bw. Hernandez alipoulizwa na waandishi wa habari mpinga Kristo ni nani alijibu: “Katika shauri hili wasimamizi wa wilaya hii ndio wamegeuka mpinga Kristo.

Katika mahojiano mengine na shirika la  NPR, Bw. Steven Hernandez alisema kuwa binti yake alikwishasema kuwa kamwe hawezi kuvaa kifaa hicho kwa kuwa kina athiri imani yake ya dini.
Mbele ya waandishi wa habari binti huyo alikaririwa akimweleza baba yake: “ ‘Daddy, I’m not going to do this.’ (baba sitafanya hivyo) aliendelea kudai kuwa kilichopo kwenye kifaa hicho ni kile kilichoonywa kwenye Biblia kuhusu Ujio wa mpinga Kristo na yeye hawezi kuwa sehemu ya ushetani huo.

“Nasema kweli niliyoipata katika Biblia, Ufunuo wa Yohana 13:17  unaeleza wazi kuwa wakati unakuja ambao hakutakuwa na uhuru wa kuuza wala kununu isipokuwa uwe umepachikwa alama ya mnyama ambaye jina lake ni namba.”

Mwanasheria anaye mtetea binti huyo alidai kuwa uongozi wa shule umeamua kumuadhibu  Andrea , kinyume na sheria ya jimbo la  Texas’  inayohusu uhuru wa dini, na hata katiba ya Marekani.

 “Wakati tunapohangaika kuhakikisha shule zetu zinakuwa salama, hasa katika wakati huu ambao tumekumbwa na majanga makubwa ya ufyatuaji wa risasi na mauaji; hatuamini kuwa utumiaji wa vifaa hivi utakuwa msaada, nadhani wauaji wanaweza kufanya vibaya zaidi kama watatumia vifaa hivi kuulia,” alisema  John W. Whitehead, rais wa taasisi ya  Rutherford.

Uongozi wa shule unadai kuwa kufungwa kwa vifaa hivyo kutapunguza idadi ya wanafunzi watoro na kuongeza makusanyo ya ziada kiasi cha Dola za marekani Milioni 1.7, kutoka kwa uongozi wa jimbo wakati wa ufungaji wa vifaa hivyo  katika wilaya nzima yenye shule  112 .

No comments:

Post a Comment