Viongozi wa Dini wateta na JK kuhusu kulegalega kwa amani nchini.

Rais Jakaya Kikwete, ameelezea kuogopeshwa na kulegalega kwa amani, utulivu na usalama wa nchi hasa katika kipindi cha mwaka jana.

“Nimeogopeshwa sana na hali ya kulegalega kwa hali ya amani, utulivu na usalama wa nchi yetu, hususani kipindi cha mwaka jana na naomba hali hiyo isitokee tena mwaka huu wa 2013,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

"Maana hata nilipolazimika kutumia vyombo vya dola vyenye dhamana ya kutuliza ghasia, bado hali ilikuwa ngumu…lakini naamini kupitia misikiti na makanisa mkiendelea kuwahubiria waumini wenu, hali itakuwa shwari,” alisema wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)- Dayosisi Kati-Singida, Mchungaji Dk. Alex Mkumbo, iliyofanyika makao makuu ya kanisa hilo, Usharika wa Imanuel, mjini hapa jana.
Rais Jakaya Kikwete
Kwa msingi huo, Rais Kikwete, ameyataka madhehebu ya dini kurejesha utaratibu wa zamani wa kukutana pamoja mara kwa mara kujadili mahusiano baina yao ili kuepukana na uhasama wa kidini unaoweza kusababisha machafuko makubwa nchini.

Alisema masuala ya udini siku za nyuma hayakuwapo hapa nchini kutokana na viongozi wa madhehebu ya dini kukutana na kumaliza tofauti zao mapema.

Hata hivyo, alisema hivi sasa utamaduni huo umetoweka hali inayoweza kuchangia kutokea kwa machafuko ya udini nchini.

Aidha, Rais Kikwete aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwahubiria waumini wao kujiepusha na vurugu za udini, matumizi mabaya ya dawa za kulevya, uvivu, biashara ya ukahaba na kupiga vita vitendo vya kuomba na kupokea rushwa ili washiriki vema kujiletea maendeleo yao.

“Dini na serikali wote tunafanya kazi ile ile ya maendeleo na wananchi wanahimizwa kujiletea maendeleo na dini pia inahimiza waumini wake kupata maendeleo. Kwa hiyo nawaomba tuendelee kushirikiana pamoja, serikali yangu inaahidi kushirikiana na madhehebu ya dini,” alisema.

Alisema utaratibu wa zamani wa viongozi wa dini waliokuwa wanautumia kukaa na kujadili masuala mbalimbali, ulisaidia kutuliza ghadhabu, kuonya na kufundisha, hali aliyotaka ufufuliwe na kuhuishwa upya ili kuimarisha amani na utulivu nchini.

Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)- Dayosisi Kati-Singida, Mchungaji Dk. Alex Mkumbo mbele, na kwanyuma ni yake ni Askofu Mkuu wa KKKT, Alex Malasusa 

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT, Alex Malasusa, alimshukuru Rais Kikwete, kwa kutoa kauli hiyo inayowahakikishia waumini wa madhehebu yote uhuru wa kuabudu kila mtu na dini yake pasipo kuingiliwa.

Dk. Malasusa alimweleza Rais Kikwete kuwa Kanisa litakuwa bega kwa bega na serikali kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu nchini, licha ya wachache kutaka kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.

Mapema baada ya kuwekwa wakfu, katika risala yake, Dk. Alex Mkumbo, alimwomba Rais kurejesha Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruruma iliyopo wilaya Iramba, kutokana na eneo hilo kuwa kitovu cha madhehebu ya Lutherani, kwenye dayosisi hiyo.

Dk. Mkumbo alimweleza Rais Kikwete kuwa shule hiyo ilichukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na yeye ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Kanisa linaiomba shule hiyo ili kuweka mambo mengi muhimu ya ukumbusho wa KKKT Dayosisi ya Kati.

Hata hivyo, katika majibu yake, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa kanisa hilo kukutana na wenzao viongozi wa ngazi ya mkoa wa Singida ili kumaliza kabisa tatizo hilo.

Katika sherehe hizo, wageni mbalimbali walihudhuria wakiwamo Maaskofu wa kanisa hilo kutoka ndani na nje ya nchi kama Norway, Ujerumani, Afrika Kusini na Marekani.

Source:Nipashe

No comments:

Post a Comment