Wana bunduki na majeshi, lakini mimi nina Jina la Yesu!

Hatimaye mjane wa aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa kituo cha Luninga cha Channel TEN, aliyefariki dunia akiwa mikononi mwa Polisi katika mazingira ya kutatanisha, Bi. Itika Mwangosi, ametoa ya uvunguni mwa moyo wake akisema; amechoka kuhangaishwa sasa anamwachia Bwana Yesu Kristo ampiganie.

Katika mahojiano maalumu na chanzo kimoja cha habari nyumbani kwake, Iringa Bi.Itika alisema: “Nimechoka kuhangaishwa, najua kuwa serikali ina majeshi na silaha kali kama zile walizotumia kumuua mume wangu, lakini mimi nina Jina la Yesu na majeshi ya mbinguni, lazima haki itapatikana siku moja.”

Akionekana kutoamini mchakato wa kiuchunguzi unaoendelea, mama huyo ambaye bado amefunga kitambaa cheusi kichwani kama ishara ya maombolezo alisema: “Uchunguzi gani unaoendelea muda wote huo, jambo hili lilitendeka hadharani kila mtu aliona; kuna haja gani ya uchunguzi wa muda mrefu kiasi hicho kweli? acha tumtwishe Bwana Yesu fadhaa zetu.”

Chanzo hicho kilipotembelea nyumbani kwake Jumanne iliyopita, na kumkuta shambani akipanda mahindi, alisema kifo cha mumewe kimemsababishia mateso mengi kwani mwanaye amemaliza kidato cha Nne lakini hana tumaini la kufanya vyema katika mtihani wake kwa kuwa aliumia sana, tena wakati wa maandalizi ya mitihani.

Alipoulizwa iwapo amekwishafungua kesi mahakamani kudai haki ya mumewe alisema: “Kwenda Kortini…labda niambiwe mwisho wa kesi mume wangu atafufuka, vinginevyo sitaenda kortini. Sihangaiki nimechoka acha tu nimuachie Yesu, yeye ana majeshi mengi ya mbinguni na anaweza kupambana na majeshi ya hawa watu…..”

Aliendelea: “Mimi tegemeo langu ni Kristo kwa sasa bado sijaanza kujishughulisha na kitu zaidi ya hichi kilimo, nasubiri Mungu anataniambia nifanye nini, ila kwa kweli nimeumia sana.”
Mwandishi huyo chipukizi aliuawa katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa Polisi, Septemba mbili mwaka huu na askari mmoja aliyedaiwa kuhusika na tukio hilo amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za mauaji.

Hata hivyo, bado taarifa ya tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, kuchunguza mkasa huo haijatoa majibu yoyote na taarifa ya awali ilipingwa na wadau; kwa kile kilichoelezwa kuwa ilificha mambo mengi.

Baadhi ya asasi za kijamii, kikiwepo kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini, viliahidi kulipeleka suala la kuuawa kwa mwandishi huyo mbele ya Mahakama ya Jinai ya kimataifa huko The Hague Uholanzi ili haki itendeke.
Baadhi ya wadai na wakereketwa wa haki za binadamu wamehoji ukimya wa suala hilo, na Jibu la Maisha likiwa nyumbani kwa marehemu pamoja na mambo mengine kujionea maisha ya mjane huyo na watoto wake na jinsi ambavyo wale waliotoa ahadi ya kusaidia familia hiyo wanavyotekeleza ahadi zao.

Ingawa mke wa Mwangosi alionekana kukata tamaa au kutokuwa uhakika wa kupata haki ya mumewe, lakini anaonekana mwenye kumtumaini Bwana Yesu zaidi kwani kila baada ya maneno machache alilitaja jina la Yesu kama mfariji wake.

Pia anaonekana kuwa karibu na ndugu wa marehemu wa mumewe kwani, kila anapoulizwa swali anajibu na kisha kuomba shemeji yake naye aulizwe kwa kuwa ana ufafanuzi zaidi.

Baadhi ya wakazi wa Iringa waliohojiwa na Jibu la Maisha, kuhusu suala la Mwangosi linavyoshughulikiwa walieleza wasi wasi wao kutokana na ukmya mwingi wa serikali wakati suala lenyewe lilitokea hadharani na wauaji wanaonekana tu.

“Kwa kweli kama Mungu anaingilia kati watu wanaotendwa uovu basi ataingilia hili. Yeye ni mume wa wajane atapigana upande wa mjane huyu kwa kuwa anakandamizwa kwa makusudi,” alisema mmoja wa majirani wa marehemu Mwangosi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mmoja wa wanasheria mashuhuri nchini, Dk. Daniel Mjema, aliliambia Jibu la Maisha kuwa, yeye na baadhi ya wanasheria wenzake wako tayari kusaidia mjane huyo kufungua mashtaka ya madai mahakamani ili kudai fidia ya kifo cha mumewe kwa kuwa hiyo ndiyo njia itakayosaidia kupatikana kwa haki ili familia iliyoachwa ipate kusoma na kuendeleza maisha.

“Fikiria Mwangosi ameuawa lakini familia yake ipo pale inatakiwa iendelee kuishi, itaishije kama hawakupata fidia? kama angekuwa amekufa katika mazingira ya kawaida kusinginekuwa na neno, lakini kwa kuwa kifo chake kimetokana na watu; na watu hao wanamilikiwa na mamlaka fulani, basi mamlaka hiyo inapaswa kuagizwa kulipa fidia stahiki,” alisema Dk. Mjema.

No comments:

Post a Comment