Abdulrahman Kinana ataka amani idumishwe.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema amekerwa na chokochoko za kidini zilizoanza kujipenyeza  na kuomba madhehebu ya dini na taasisi zake nchini,kuendelea kuhubiri amani na  kuliombea taifa, ili wananchi waendelee kujivunia amani.

Kinana alitoka kauli hiyo jijini Arusha katika sherehe za Hussein Day, ambazo ni maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mtume wa dini ya kiislamu, Muhammad inayoandaliwa na tasisi ya kidini ya Khoja Shia.


Kinana alisema upo umuhimu kwa viongozi wa dini na taasisi zake kuendelea kuienzi amani kwa kuhubiri suala la kudumisha amani na kuonya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua za haraka dhidi ya mtu ama kikundi chochote cha dini kitakachojihusisha na uvunjifu wa amani.

Alisema pamoja na changamoto zinazojitokeza hivi sasa kwa baadhi ya dini kukashifu dini zingine, serikali iko macho kuhakikisha inadhibiti hali yoyote ya ukiukwaji wa maadili ya kidini na kusisitiza kwamba dini zote nchini ziendeshe shughuli zake kwa kuheshimiana.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya  Khoja Shia, Gulam Hussen, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuendelea kukumbuka mazuri yote aliyokuwa akiyafanya mtume  Mohamad,  kwa lengo la kukumbushana na kuyaenzi.

No comments:

Post a Comment