Mwingira ashauri wagombea wapimwe akili

Kiongozi  wa Kanisa la Efatha nchini, Mtume Josephat Mwingira ametaka kila anayegombea uongozi wa umma sharti apimwe akili.

Hayo aliyaeleza jana asubuhi wakati akihubiri katika ibada ya kwanza kwenye makao makuu ya Kanisa hilo, jijini Dar es Salaam.

”Hali ni mbaya, malalamiko ya wananchi dhidi ya wizi wa rasilimali za Taifa kwenda nje yamekuwa mengi,’’ alisema.
Alisema tabia ya mfumo wa uchumi nchini ya kuthamini wawekezaji kutoka nje ya nchi kuliko wa ndani  siyo nzuri na kwamba ni moja ya vyanzo vya kudorora kwa uchumi wa taifa.


“Mimi nimewahi kuchimba madini ya Tanzanite, ikanipa kipato kizuri tu lakini nilinyang’anywa wakapewa wawekezaji wakubwa, siasa zisizoona tatizo hata kudhulumu wananchi wake ni siasa chafu,” alieleza Mtume na Nabii Mwingira.

Akifafanua juu ya hali ilivyo nchini, alitoa mfano wa familia yenye kumiliki ardhi kubwa lakini isiyoendelezwa akisema, “wanakuja watu kutoka nje kuomba wapatiwe ardhi hiyo ili waiendeleze kwa kilimo na ufugaji na baba wa familia husika ambaye anawaruhusu kwa kusema, ‘tumieni tu hamna taabu’.

Kiongozi huyo mwanzilishi wa Kanisa la Efatha alieleza kuwa wageni hao wanapohoji kuhusu malipo, wanaelezwa na baba wa familia husika kuwa hakuna tatizo waendelee na shughuli zao kwanza, baada ya miaka mitano ndipo wataamua walipe kitu gani.

Alisema wakati wakulima hao wakivuna mazao na kuuza na mengine kuhamishia kwenye nchi zao, wanafamilia inayomiliki mashamba hayo wanakabiliwa na uhaba wa chakula kiasi cha wengine kufa kwa kukosa chakula, hali inayosababisha baba wa familia husika kuchota fedha za familia, kwenda kwenye nchi za wale wanaolima mashamba yake kuomba misaada.

“Hii si sawa, kuna umuhimu kila mtu atakayetaka kuongoza umma wa Watanzania hata kama ni ngazi ya mbunge, akapimwe akili yake kwanza ili kujiridhisha na uwezo wao wa utendaji kiakili,” alieleza Mwingira.

No comments:

Post a Comment