Mokiwa abwagwa Uaskofu Mkuu wa Anglikana

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosia la ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa ameshindwa kutetea nafasi yake ya uskofu mkuu wa kanisa hilo Tanzania baada ya kushindwa na Dk Jacobo Chimeledya (56) wa Jimbo la Mpwapwa.

Askofu Chimeledya ambaye anakuwa kiongozi wa sita kushika wadhifa huo nchini, aliibuka mshindi baada ya jina lake kupenya katika hatua tatu za kura.

Akitangaza matokeo hayo juzi jioni, Katibu Mkuu wa Anglikana, Dk Dickson Chilongani alisema kanisa hilo halina utaratibu wa kutangaza kura zilizopigwa lakini akathibitisha kuwa Askofu Chimeledya ndiye mshindi.

Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,Dk Valentino Mokiwa.
Dk Chilongani alisema kuchaguliwa kwa Askofu Chimeledya ni utaratibu wa kanisa hilo ambalo hufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

Uchaguzi huo ulianza kwa ibada iliyoongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, Godfrey Mhogolo na baada ya hapo, Msajili wa kanisa hilo, Profesa Palamagamba Kabudi alitangaza utaratibu wa uchaguzi.

Chilongani alisema wajumbe 129 walihudhuria mkutano huo kati ya wajumbe 140 waliotarajiwa.

“Kwa kawaida katika uchaguzi, askofu yeyote mwenye umri chini ya miaka 60 huwa anaweza kuwa mgombea na katika uchaguzi huo, maaskofu 21 walikuwa na sifa za kugombea,” alisema.
.
Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment