Tamasha la Pasaka kuhamasisha Amani na Upendo

Waandaaji wa Tamasha la Pasaka mwaka 2013 wameibuka na kauli mbiu inayohamasisha amani na upendo kwa jamii.Akizungumza na chanzo kimoja cha habari,Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo Alex Msama alisema wanashukuru kwamba sasa wamepata kibali cha kufanya tamasha hilo kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Alex Msama

Alisema tamasha la mwaka huu litakuwa zaidi katika kuhubiri amani kwa jamii na kusisitiza kuwa dhamira yao ni kuhakikisha Watanzania wanazidisha upendo na mshikamano uliokuwepo.
Alisema tamasha hilo litafanyika Machi 31 katika ukumbi ambao utatangazwa hivi karibuni na kuwa wana matumaini mambo yatakuwa mazuri kuliko tamasha la mwaka jana lililofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


 “Hatua ya Basata kutupatia kibali inamaanisha tumepata baraka, hivyo tuendelee na mambo mengine ya maandalizi, nasi tunasema mambo mwaka huu yatakuwa mazuri zaidi,” alisema Msama.
Alisema wamepanga siku yenyewe ya Pasaka tamasha lifanyike Dar es Salaam na siku inayofuata bado wanaangalia wafanye wapi kwani mikoa mbalimbali imeomba ipewe uenyeji.

Tamasha la mwaka jana baadhi ya waimbaji mahiri waliokuwepo ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Atosha Kissava,na kundi la Glorious Celebration.

Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival, Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilikuwa miongoni mwa burudani zilizokuwepo siku hiyo.

No comments:

Post a Comment