Ugeni wa Papa wa Othodox Afrika kukutana na JK


Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Othodox Afrika, Papa Beatitude Theodoros II anatarajia kukutana na Rais Jakaya Kikwete.

Kiongozi huyo aliyewasili nchini siku chache zimepita, alisema anatarajia kuwa na mazungumzo na Rais Kikwete na miongoni mwa mazungumzo yao ni jinsi ya kanisa hilo litawaletea maendeleo Watanzania.

“Nitazungumza naye juu ya mipango niliyonayo ya maendeleo Tanzania na kuomba ushirikiano zaidi,” alisema Papa Theodoros II.
Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Othodox Afrika, Papa Beatitude Theodoros II
Alisema Kanisa la Othodox limekuwa likiendesha miradi mbalimbali kusaidia Watanzania ikiwapo hospitali itakayogharimu Sh17 bilioni, inayojengwa Nyegenzi, mkoani Mwanza.

Miradi mingine ambayo kanisa hilo linatarajia kuanzisha nchini  ni kujenga vituo vya watoto yatima, vituo vya ushauri na kutoa matibabu kwa waathirika wa virusi vya Ukimwi (VVU) na ujenzi wa shule.

“Nina mpango wa kukutana pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ili kuweka mikakakti jinsi ya kuendeleza elimu nchini,” alisema Papa Theodoros II.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodox, Jimbo Kuu la Mwanza, Jeronmos Muzeyi alisema ujio wa Papa Theodoros II nchini ni kuandika historia ya pekee kwa sababu ni mara ya kwanza.

Alisema Papa huyo amefurahia mazingira na ukarimu wa Watanzania na kwamba, atakuwa akifanya ziara za mara kwa mara  ikiwa ni sehemu ya kuzidi kujenga uhusiano.

Alisema lengo kuu la kanisa hilo ni kuendeleza amani, upendo na mshikamano kwa Watanzania wote na kuhakikisha wanapiga hatua zaidi za maendeleo.

No comments:

Post a Comment