CPCT kuwasha moto Desemba

Baraza la Makanisa ya Kipentekost Tanzania (CPCT) nchini linatarajia kuwasha moto wa maombi ya kufunga mapema mwezi Desemba mosi hadi 23, 2012 ili Mungu akomeshe vurugu dhidi ya adui shetani ambaye hutumia watu kuharibu amani nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo,  Askofu David Batenzi wakati akiongea na chanzo kimoja cha habari kwenye semina ya viongozi wa ngazi ya maaskofu na makatibu wa makanisa ya kipentekosti Tanzania, iliyofanyika Dodoma, kwenye kanisa la  Phidelphia Gospel Assembly.

Askofu Batenzi, alisema imewalazimu kukimbilia magotini mwa Mungu kufanya maombi ya siku 23 ili kujiweka imara mbele za Bwana Yesu, ambaye wanaamini wakimlilia vita ya shetani dhidi ya kanisa itakoma kama ilivyokuwa nyakati za ukuta wa Yeriko.

Mtumishi huyo alisema, kutokana na ukosefu wa nidhamu alionao shetani na wafuasi wake, kikao kimeamua kwa pamoja Maaskofu wote kuwashirikisha waumini wote wa makanisa ya kipentekosti, ili maombi hayo yafanyike kwa ajili ya mahitaji watakayoyaomba.

Alisema kuwa katika siku hizo za maombi pamoja na kuombea amani na utulivu wa nchi, pia wataomba maombi ya kukomesha vurugu zinazofanywa dhidi ya wakristo, vinavyotendwa vya kuhatarisha amani.

Mbali na kuombea amani na ulinzi katika majengo ya ibada, pia wataomba kwa ajili ya viongozi wa serikali ili Mungu awape kusimamia haki ambayo hivi sasa imeingia dosari kutokana na baadhi ya waumini kuleta machafuko yasiyo na msingi ndani ya nchi hii ambayo Mungu amewabarikia watu wake.

Awali Askofu Batenzi aliongelea juu ya kusudi la semina hiyo, alisema ni kukumbushana kwa viongozi wa CPCT kuhusu changamoto wanazokutana nazo kwenye makanisa ya Kipentekosti, na jinsi watakavyokabiliana  pamoja na kuangalia maazimio kupitia katiba ya CPCT

Batenzi aliongeza kuwa, pamoja na hayo kikao hicho cha siku mbili ambacho kilikuwa na mada mbalimbali kutoka kwa watumishi wa Mungu, pia lengo lingine ilikuwa ni kunoana kiroho viongozi wenyewe kwa wenyewe na kuhimiza  waumini kuongeza kasi ya utendaji wa kiroho ambao utafanikisha kuwahubiria wanaovuruga amani.

Aidha alisema suala lingine lililoangaliwa kwa makini ni juu ya kuimarisha umoja wa makanisa, kuanzia watumishi hadi waumini na kupeana taarifa mbalimbali zitakazoweka wazi kama kuna tatizo lolote dhidi ya makanisa.

Hata hivyo,  Askofu huyo aliwakumbusha juu ya utekelezaji wa maazimio magumu, ambayo yamekuwa yakisuasua katika umoja wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekosti Tanzania.

Mapema kabla ya kikao hicho ulifanyika uchaguzi wa baraza hilo mkoani Dodoma , ambapo Makamu Askofu wa TAG, Jimbo la Dodoma Mchungaji  Willbarforce  Mongi, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na nafasi ya makamu ilienda kwa Mchungaji Charles Kanyika.

Kwa upande wa Katibu wa Baraza hilo, Mkoa wa Dodoma alichanguliwa Mchungaji Baraka Kihoza ambapo wajumbe waliochaguliwa ni pamoja na Askofu Silvester Thadey, Askofu Julias Bundala na aliyekuwa Mwenyekiti wa kipindi cha nyuma Askofu Donard Mhango.

No comments:

Post a Comment