Njia mpya kuteka wasichana yaibuka

Mitandao ya kijamii ukiwemo Facebook, imegeuka mlango wa ibilisi wa kupoteza mabinti wanaorubuniwa  na kutekwa kisha kutendewa unyama wa kustaajabisha. Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa jumla ya mabinti 129, wameshatekwa na kutendwa vibaya baada ya kurubuniwa kupitia mitandao.

Shirika la habari la ‘Associated Press’ linaeleza kwamba tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea wiki kadhaa zilizopita baada ya binti wa miaka 14 kupokea ujumbe kwenye mtandao wake huo wa Facebook, kutoka kwa mtu mmoja ambaye hakuwa akimfahamu kuomba urafiki.

Shirika hilo linasema kuwa binti huyo kwa masihara kukataa ombi la mtu huyo anayesadikiwa kuwa na umri wa baba yake, alikubali kumuorodhesha kuwa miongoni mwa marafiki zake.

Linasema kwamba baada ya kuongezwa kwenye orodha ya marafiki wa binti huyo, mtu huyo aliendelea ‘kuchati’ kwa kasi isiyokuwa ya kawaida huku wakibadilishana namba za simu ili kuwasiliana kwa undani na kwa haraka zaidi, na hapo ndipo mkasa ulipoanzia.

Kitambo kidogo kikapita, Associated Press inaendelea kuweka wazi kuwa, mtu huyo asiyekuwa na soni alimuomba binti huyo wakutane katika maduka makubwa (kwa Tanzania tungesema (Mlimani City jijini Dar).

“Binti huyo baada ya kuonana na mtu huyo alielezea kwamba alikuwa na sifa ya ucheshi sana na mwenye masihara na hilo lilimfanya kuwa na mawasiliano ya karibu tofauti na marafiki wengine aliokuwa nao katika mtandao wake,” lilisema shirika hilo.

Urafiki ulikolea na hivyo baba huyo kuomba wakutane tena kwenye eneo waliloonana awali, lakini kabla ya kuonana naye binti huyo alimuaga mama yake kwamba kabla ya kwenda kwenye mazoezi ya Kwaya kanisani kuna mtu wataenda kukutana naye.

Siku hiyo baada ya kukutana na kuongea kidogo alimchukua na kumpeleka nje ya mji wa Jakarta ambapo walisafiri kwa mwendo mrefu kidogo na kuingia mji wa Bogor Magharibi wa Java.

Walipofika kwenye eneo husika walimuingiza kwenye chumba kidogo ambamo walikuwa wasichana wengine kama watatu waliokuwa na umri kati ya 14 na 17 ambapo walimbaka mfululizo.

Baada ya wiki moja ya mateso wale mabinti wengine waliokuwa pamoja nae mmoja alimueleza kwamba, yeye aliuzwa akitokea Singapore na alinunuliwa na watalii walifika eneo hilo kwa boti.

Alimueleza kuwa, amekuwa akilia na kuwaomba wamrudishe, lakini hawataki kumsikiliza zaidi ya kumpa mateso ya kumpiga na kumwambia anyamaze ama auawe.

Mwezi mmoja baada ya mateso na kubakwa, binti huyo ambaye wazazi wake walikuwa wakimuombea alipatikana kwenye kituo cha mabasi akiwa ametupwa hapo.

Akiongea kwa uchungu huku akiwa amefunika sura yake ili asionekane, binti huyo ambaye ni mwanafunzi alisema:

“Nilikuwa nikiwasiliana na watu mbalimbali na kubadilishana nao namba ya simu, lakini hakukuwahi kutokea shida yoyote, nikiwa huko niliwekwa chini ya ulinzi mkali, kweli mtu huyo namfahamu hata nikimuona sasa, ila namuogopa sana.

Aliniahidi kuninunulia vitu vingi vikiwa ni pamoja na vifaa vya shule, lakini nilikuja kugundua baadaye kwamba hakua mtu mwenye pesa, nina hasira sana sifurahishwi na kile alichonifanyia. Najua kwamba shuleni nitanyanyapaliwa, sitamani tena kwenda shule, kweli nikumbukapo jambo hili nashtuka sana.”

Mtekaji nyara mwenyewe hajapatikana lakini wapo  watu wanaoshikiliwa na Polisi kwa matukio yanayofanana na hayo, wengine wakinaswa na picha za mabinti wakiwa watupu.

Wakati hilo likiendelea, Kamisheni ya taifa ya Indonesia inayojishughulisha na ulinzi wa watoto, (INCCP) imebainisha kwamba ndani ya mwaka huu 2012, watu 27 kati ya 129 waliotekwa walipatikana nchini humo, na wengi waliotekwa wanaeleza kuponzwa na mitandao.

Mwenyekiti wa shirika hilo la kulinda watoto, Merdeka Sirait alieleza kwamba wengine wengi wamepatikana, lakini wakiwa wamekwisha uawa.

Mwingine aliyeongelea suala la utekaji kwa mabinti ambao umekuwa ukishamiri siku za hivi karibuni,  Bw. said Anjan Bose, ambaye ni Afisa  program anayeshughulikia masuala ya watoto, alisema kuwa mitandao imekuwa ikitumiwa na watu wa namna zote pasipokujua hao ni matajiri na masikini.

Indonesia ni nchi yenye watu zaidi ya milioni 50 wanaotumia mtandao wa Facebook duniani ikiongozwa na Marekani ikifuatiwa na Ufaransa. Imeelezwa kwamba asilimia kubwa ya  mabinti wapo hatarini lakini hawajui na hata wazazi wao hawana muamko wa kujua hatari ya kuruhusu mgeni kujua taarifa muhimu za watoto wao kupitia mitandao.

Nchini humo kama ilivyo hata hapa Tanzania, vijana wamekuwa wakiweka bayana picha na maelezo binafsi kama; anuani za majumbani mwao, simu na shule badala ya kuweka kwa  namna ya siri ambayo haitaonwa na kila mtu.

Kwa msingi huo watoto wengine 435 walitekwa mwaka jana na kufanyiwa matendo ya kinyama vikiwemo vya kingono, jeshi limeonekana kushindwa kudhibiti kutokana na mazingira, huku ikiongezwa kwamba makisio yakionesha kuwa  kwa mwaka watu 40, 000 hadi 70,000 wamekuwa wakijiingiza au kuingizwa kwenye masuala ya kingono nchini humo.

Matukio ya udhalilishaji wa ngono yamekuwa kawaida katika mataifa kama Asia  na Philipino ambapo mbali na kutekwa, lakini pia wazazi wamekuwa wakiruhusu watoto wao jinsi ya kujishughulisha na mitandao.

No comments:

Post a Comment