Elimu ya mashirika ya Dini ni mkombozi kwa serikali

Elimu ya vituo ya ufundi inayotolewa na mashirika mbalimbali ya dini  kwa vijana wanaohitimu mafunzo yao, imekuwa mkombozi mkubwa kwa upande wa serikali na jamii katika uboreshaji wa maisha pindi wanapomaliza na kuanza safari ya kujitegemea.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwasisi wa Chuo cha Ufundi kinachomilikiwa na Ushirika wa akina mama wa Kikristo (UMAKI) cha Kanisa la Anglikana Tanzania, Bi.  Beatrice Kasembe, wakati akitoa nasaha kwa wahitimu siku chache zimepita kwenye mahafali ya 22 yaliyofanyika mkoani Dodoma.

Mwasisi huyo alibainisha kuwa, elimu ya ufundi inayotolewa kwenye vituo mbalimbali vya ufundi inawajenga vijana katika msingi wa kujitegemea na kujiajiri, jambo linalowafanya kutotangatanga na kujiingiza kwenye shughuli zinazohatarisha maisha yao.

Bi. Beatrice ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo hicho, akizidi kuweka wazi kwenye mahafali hayo, alitanabaisha kuwa vituo vya vyuo vya ufundi vinavyomilikiwa na mashirika hayo ya dini, vimesaidia vijana wengi waliohitimu kujiajiri wenyewe na baadhi kuingia kwenye taasisi za kiserikali.

Kwa namna nyingine akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa kozi ya ushonaji na uhazili wapatao 22, aliwashauri kuimarisha ujuzi walioupata kwa kujiendeleza zaidi, badala ya kuridhika katika eneo walilofikia, ikizingatiwa kuwa miaka ya hivi sasa dunia imetawaliwa na utandawazi unaoruhusu wataalamu kutoka nje wa nchi.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Bi. Neema Mwendi alichanganua kuwa, tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha mafunzo ya wasichana na wanawake na kuweza kujiajiri na kuajiliwa katika ofisi mbalimbali mkoani Dodoma na hata nje ya Mkoa.

Bi. Neema alisema Chuo hicho cha ufundi kilianzishwa mwaka 1990 kwa lengo la kupiga vita umaskini kwa kuwawezesha wasichana kujiajiri ama kuajiriwa ambapo mpaka sasa mwaka 2012 waliohitimu ni 1959 na wamefanikiwa kujikwamua kimapato katika maisha yao ya kila siku.

No comments:

Post a Comment