Moto wa Mahakama ya Kadhi

Moto  wa kudai mahakama ya Kadhi inayogharamiwa na kusimamiwa na serikali umeibuka upya, lakini safari hii harakati zinafanyika msikitini na CD zimefyatuliwa na kuingizwa mitaani huku zikiwa na hotuba kali za wanazuoni na wanasiasa pia.

Miongoni mwa wanasiasa walioshiriki kwenye mkanda wa CD hiyo inayoitwa Waislamu Tujipange, ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahimu Haruna Lipumba, ambaye picha yake imewekwa kwenye jalada la juu ya CD hiyo.

Miongoni mwa hoja nzito za Prof. Lipumba, ni kuwa Mahakama ya kadhi isiyoendeshwa na kugharamiwa na serikali haiwezekani, kwa kuwa hicho ni chombo cha dola na hakiwezi kufanya hukumu kikiwa kinaendeshwa nje ya dola.

Akiwa ndani ya Msikiti wa Idrisa Kariakoo jijini Dar es Salaam siku chache zimepita, Profesa Lipumba alitolea mfano majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria ambayo yalianza kuongozwa na sheria tangu yakiwa chini ya ukoloni wa Waingereza.
Profesa Ibrahimu Lipumba
Profesa Lipumba ambaye ni mchumi aliyewahi kuwa mshauri wa Rais kwa masuala ya uchumi, alionya kuwa ikiwa suala la mahakama hiyo litaachwa  mikononi mwa Waislamu wenyewe kama serikali inavyotaka linaweza kuangukia  mikononi mwa waislamu wenye siasa kali na siku moja wanaweza kudai hata dola ya kiislamu.

Kiongozi huyo wa kisiasa alieleza mshtuko wake aliposikia Rais Jakaya kikwete akisema kuwa Waislamu  wenyewe, jambo ambalo haliwezekani.

Katika mkanda huo Profesa Lipumba anaonekana akiwahamasisha Waislamu kujipanga ili kudai haki yao ya kutambuliwa kama rais wa daraja la  kwanza.

Mkanda huo umewashtua baadhi ya watu kutokana na ukweli kuwa, Profesa Lipumba ni kiongozi wa kisiasa anayepaswa kutetea watu wa dini zote, maneno “Waislam Tujipange” yanaweza kutafsiriwa kama kuelemea upande mmoja wa dini.

Alitumia nafasi hiyo kuzungumzia, historia ya Mahakama za Kadhi Tanzania, Kenya na Nigeria, huku akisisitiza kuwa, Waislamu wanapaswa kujipanga kutetea haki zao.

Katika CD, hiyo Sheikh Basaleh ambaye ndiye aliyemkaribisha Prof. Lipumba anasema kuwa, amemuita kiongozi  huyo kwa kuwa ni kiongozi na ni muislamu na hata  viongozi  wengine wa kisiasa wamekuwa wanaingia katika nyumba za ibada na kutoa hotuba.

“Nilipokuwa nikitangaza jana kuna mtu aliniuliza wewe Basaleh ulitutangazia kuwa atakuja Prof. Lipumba na utampa nafasi, yeye ni mwenyekiti wa CUF, je akija wa CCM utampa nafasi? nikasema yeye ametupa taarifa hata huyo wa CCM akitupa taarifa tutampa nafasi kwa kuwa kwanza huyo ndiye Rais wa nchi hii.  Karibu Profesa Lipumba…Rais mtarajiwa …karibu  uje uzungumze na  Waislamu katika nchi hii, lakini nakuomba uzungumzie hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2015, karibu,” alisema Sheikh Basaleh.

Katika mkanda huo, Sheikh Said Ricco, anamalizia kwa kusema: “Mwaka 2010 kulifanyika juhudi kubwa sana kumsaidia bwana mkubwa vinginevyo asingekuwepo. Lakini mzee kapigwa wala hakumsaidia……Lipumba kasema nitakuja kuulizwa mimi wewe Lipumba nimekupa kisomo  umewasaidia nini Waislamu wenzio….hayo ni mashtaka sio mashtaka mbele za mwenyezi Mungu?”

Kisha anaendelea: “Atajibu hawa niliowaendea kwenye majukwaa ya kisiasa hawakunielewa nikawafuata hata misikini ndugu zangu hawa  walala hoi  hawakunielewa sasa tusichokielewa nini? Tutaenda kumjibu nini mwenyezi Mungu, kwa sababu kaja msikitini. Wewe unadhani ni mtu wa kutafuta kazi,  wanamtaka finland, china japani tena kwa pesa nyingi mno.

Ni kwa nini wewe unadhani anakuja msikitini anakuja kwa sababu anataka watanzania wenzie hasa sisi  tunaitwa walala hoi ambao ni Waislam. Ukiangalia huko mitaani wafagizi wote ni Waislamu , wakezetu ndio wanaotembea na mabeseni ya kuuza mihogo, jioni akirudi miguu  imepasuka akiingia kwenye neti ananasa.

Wanawake wa Kikristo hawafanyi hiyo biashara, sasa mimi nilichosimama hapa nakuombeni na sisi tuwe na majibu ya kumjibu Allah subiana uwataalah……….Imam ndani ya hotuba amezungumza wazi kwamba huu ni mwezi wa Rajab, mwezi Mtukufu mwezi ambao  hatutakiwi kudhulumu. Sasa je tuko tayari, tunamuahidi mwenyezi Mungu ndani ya mwezi wa Rajab, katika msikiti mkubwa wa Ali Jumaa, hatutabadilika tena kwenda kuwapigia kura wale; tuko tayari? mnaahidi mbele ya viongozi maana yeke hapa kuna Amir, sheikh Basaleh, maana yeye ndio kiongozi wetu. Je mnaahidi kuwa yeyote atakayebadilika mwenyezi Mungu amtie kansa ya damu?”

Tatizo lenu ni kupewa kapelo na fulana, kwanini mwanaume mwenzenu anakupa kapelo na fulana kwanini asikupe suruali………Ibrahimu yuko mbingu ya saba sasa wewe umkatae Ibrahimu wewe nani? ,” alimalizia sheikh huyo na kumkabidhi sheikh Basaleh ambaye alisema kazi ya mwaka 2015 imeshaanza na wasizubae wakapigwa bao la kisigino.

Kwa sasa Waislamu tayari wana mahakama ya Kadhi, na Kadhi Mkuu, lakini hagharamikiwi na serikali isipokuwa na waislamu wenyewe.

No comments:

Post a Comment