Mwalimu, Mafanikio ya elimu yanaambatana na kuwa karibu na Mungu pia maombi.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ya Bombambili, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Mwl. Simon Lupanga amesema ili mafanikio ya elimu yaweze kupatikana, na kujenga mshikamano wa kuheshimiana kwa wafanyakazi na wanafunzi, ni lazima kumtanguliza Mungu kwanza kwa maombi.

Wito huo aliutoa hivi karibuni katika hafla ya kuagwa baada ya kuiutumikia  shule  hiyo kwa muda mrefu ambapo ilitanguliwa na sherehe za mahafali ya darasa la saba wa shule hiyo.

Alisema kuwa, amefundisha wanafunzi kwa pindi kirefu bila mkwaruzano kutokana na kuwa karibu na Mungu huku akimshirikisha mambo yote yaliyohusu uongozi wake.

“Naomba niwapeni siri niliyokuwa nikiitumia kabla sijaingia katika kipindi cha kufundisha au kufanya kikao na ninyi walimu wenzangu, nilikuwa natanguliza sala kwanza ya kutupatanisha sisi na Mungu ili tujaliwe katika maamuzi ya kikazi,”alisema Mwl. Lupanga.

 Alisema ikiwa mtu anafanya maombi katika kazi aliyonayo, hakika anafanikiwa vizuri zaidi kwa kuwa shetani siku zote halila ila kutaka kuleta mafarakano na matatizo katika umoja huku akieleza kwamba ikiwa mtu ataomba ni wazi kuwa mipango ya shetani hutoweka bila hata muhusika mwenyewe kutambua.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sabasaba, iliyopo mjini Matarawe Raphael Karonga ambaye amechukua nafasi ya Mwl. Mkuu Simon Lupanga alisema kuwa, tangu afike shuleni hapo kuchukua nafasi hiyo amekuta sifa nzuri za mwalimu mkuu aliyemtangulia.

 “Nimepata sifa za uongozi wako katika shule hii, ndio maana nikaungana na walimu wenzangu kufanya maandalizi ya kuweza kufanikisha kukuaga kwa heshima zote zinazo takiwa kama kiongozi hodari wa shule katika nyanza za utoaji elimu kwa vizazi vyetu,”alisema Mwl. Karonga.

Kwa upande wake mwalimu mmoja wa shule ya Sabasaba, Bi. Elizabeth Ndunguru alipopata nafasi ya kutoa Neno la shukurani alisema anamuomba mwalimu mkuu Lupanga akaendeleze msimamo wake kwa manufaa ya jamii na kizazi kijacho.

No comments:

Post a Comment