Makamba apotoa Biblia!

•    Ni kumlinganisha Kikwete  na  Yesu•    Wachungaji, maaskofu wamjia juu•    Alikuwa akijihami na kura za maruhani

Katibu Mkuu mstaafu wa chama cha Mapinduzi CCM, Luteni mstaafu Yusufu Makamba, siku chache zilizopita katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika mjini Dodoma alikaliliwa kutumia muda mwingi kutoa ufafanuzi wa vifungu vya Biblia kwa lengo la kumwombea kura Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete huku akimfananisha mgombea huyo na Yesu Kristo, jambo ambalo limepingwa vikali na watumishi wa Mungu.

Katika mkutano Mkuu wa CCM, uliofanyika maeneo ya Kizota mjini Dodoma, Makamba alianza kwa kusema kuwa, ameshalemaa kwa kutumia vifungu vya Biblia, kila anapohutubia, licha ya kuzaliwa katika familia ya kiislamu, na kukulia katika uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).    


Katibu Mkuu mstaafu wa CCM,  Yusufu Makamba
Makamba kabla ya kusema maneno hayo yaliyowaudhi baadhi ya wachungaji na maaskofu, alijihami kwa kuwaomba radhi masheikh, akidai kuwa lengo lake la kutumia Biblia jukwaani si kutangaza dini, bali anatumia vifungu vya Biblia kumwombea kura Kikwete ili aweze kuendelea kushika nafasi ya uenyekiti kwa kipindi kijacho.

Baadhi ya wale walioguswa na kauli nzito ya  Makamba, ya kumfananisha Rais Kikwete na Yesu ni; Askofu wa Kanisa la TAG, Zanzibar, Dickson Kaganga ambaye alikuwa na haya ya kusema:

“Luteni Makamba kwa kauli yake hiyo, mimi namuangalia kama mtu asiyejua maana ya Biblia na kuleta tafsiri mbaya katika ulimwengu wa kawaida,” alisema na kuongeza:

“Hata kama ni kumpigia kampeni, lakini mfano huo ni mkubwa sana hakutakiwa kuutumia katika mambo ya dunia.”

Naye Mtumishi mwingine wa Kanisa la EAGT, Geita, Mchungaji Obed Kyando, alisema, alichokifanya Makamba ni upuuzi ambao ni dhihaka na ni kufuru mbele za Mungu.

“Huwezi kumfananisha Yesu na Kikwete, ni kweli Mungu huchagua kiongozi au humtumia mtu yoyote, lakini hili ni kufuru,” alisema.

Mwenyekiti wa CPCT Dodoma, Wilberforce Mongi aliongea kwa njia ya simu kutoka mkoani humo, alisema Makamba si mtu anayejua Neno la Mungu, au mafundisho yake kwa usahihi, ingawa kwa maelezo yake anaeleza kuwahi kuwepo  KKKT.
“Mtu asiyemjua Kristo anaweza kusema lolote, najua hana analolijua kwa habari ya Yesu na Ukristo kwa ujumla,  hakuwa akieleza jambo la maana,” alisema.
Akizidi kuongea kwenye mkutano huo, Makamba alisema, anawakemea baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kupanga mbinu ya kutaka kumpigia kura za maruhani Kikwete, jambo ambalo ni uendawazimu.

Makamba ambaye mara nyingi hurukia Biblia na kunukuu vifungu kadhaa wakati wa hotuba yake alinukuliwa akisema:
“Nasema wale wote ambao wanawaza kumpigia JK kura za maruhani washindwe kwa Jina la Yesu, mnampigia kura za maruhani ili iweje kuna watu hapa ambao kazi moja imewashinda, lakini wanataka Jakaya apunguziwe kazi ni kazi gani hiyo imemshinda……” alisema na kuongeza:

“Tena mtu huyo ambaye anasema tumpunguzie JK kazi hasemi tumpe nani, hapa kazi ni moja tu, kumtafuta Mwenyekiti na Mwenyekiti wetu ni Jakaya, hafanyi kazi kwa makusudi yake binafsi, bali anafanya kazi kwa makusudi ya Mungu.”

Alisema Jakaya anafananishwa na Yesu katika kitabu kitakatifu ndani ya Biblia, kwani Mungu wakati anataka kupeleka mkombozi duniani, alianza kuuliza amtume nani na Yesu akasema: “Niko hapa nitume mimi.”
Hata hivyo alisema, anawashangaa baadhi ya wanachama ndani ya CCM ambao kwa sasa wanafikiria juu ya Ikulu, na kuongeza kuwa; kura za urais zitapatikana kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano mkuu, kama uliomalizika, jambo ambalo ni ukombozi kwa wana CCM na kwa taifa zima.

Alisema, wakati akifanya kazi alijikuta katika wakati mgumu kutokana na kuchukiwa na wanachama wengi kutokana na kufanya kazi katika mazingira ya kuwa muwazi na mkweli, hivyo kumtaka Jakaya Kikwete kuhakikisha anakuwa ngangari bila kuwa na hofu.
Makamba alisema katika kuongoza jahazi ndani ya CCM, Jakaya bado anafaa kushika nafasi hiyo ili kuongoza mashambulizi makubwa kwa wapinzani na wala hakuna sababu ya kuwepo kwa kura za maruhani.

Kura za Maruhani ni mfumo ulioanzishwa huko Zanzibar, na wanachama wa chama cha Wananchi CUF, waliokuwa wakishindana na wenzao wa CCM. Wakati mgombea waliyemtaka alipokosa nafasi ya kugombea kwa sababu fulani waliamua kuandika kura zao kuwa wamepigia maruhani. Hata hivyo maruhani ni mapepo au kwa lugha nyingine hujulikana kama mashetani.

Hata hivyo wachambuzi wa Biblia wanaelezea upotoaji wa kimaandiko alioutumia Makamba kwa kudhani kwamba aliyesema maneno hayo aliyotumia alikuwa ni Bwana Yesu, jambo ambalo ni potofu. Ukweli wenyewe ni kwamba, andiko hilo ambalo liko kwenye Isaya 6:8 likisomeka:

“Kisha nikasikia sauti ya Bwana, akisema, nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo nikasema, mimi hapa, nitume mimi.”

Kulingana na ushahidi wa kimaandiko, neno ‘Bwana’ katika mfumo huo linamaanisha  Yesu, hivyo isingewezekana ajiulize na kujituma mwenyewe. Hii inaonesha kuwa aliyekuwa akijibu ni Nabii Isaya na sio Yesu kama mpotoaji alivyosema.


Source :Jibu la Maisha

No comments:

Post a Comment