Dk. Malasusa awataka Viongozi wa dini kuwa mfano

Viongozi wa dini wametakiwa kuwa mfano katika maeneo wanayoyaongoza ili kuendelea kudumisha amani  kwa ajili ya ustawi wa nchi.
Rai hiyo ilitolewa  na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, alipokuwa akihubiri katika  ibada ya kumweka wakfu, Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu.

Dk. Malasusa alisema Serikali imetoa uhuru wa kuabudu hivyo viongozi wasiposimamia amani iliyopo watahatarisha uhuru uliopo wa kuabudu.

 “Kwa sasa hivi tunaona vurugu zinazosababisha kufyatuliwa kwa mabomu ya machozi, hatupendi kuona risasi za moto zinatumika kwa kuwa wakati huo itakuwa ni vigumu kupata muda wa kuabudu,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, ambaye aliiwakilisha serikali, alisema  viongozi wa dini wasibadilike, wahubiri amani na sio vurugu.

Dk. Rehema Nchimbi alisema serikali haina dini ila imetoa uhuru wa kila mwananchi kuabudu dini anayoitaka bila kuingiliwa uhuru wa mtu mwingine.

Aliwataka viongozi wa dini kumwogopa  Mungu aliyewaweka katika nafasi hizo na kuwasaidia katika kufanya mema.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa      







Kwa upande wake, Askofu Kinyunyu aliwaomba waumuni wa Kanisa hilo kujikita katika kuendeleza mema yaliyoanzishwa na Askofu aliyemaliza muda wake, Festo Ngowo.

Alisema Askofu Ngowo alianzisha ujenzi wa ofisi za Dayosisi hiyo, ujenzi wa shule ya sekondari na miradi mingine mbalimbali ya Kanisa hilo.

Askofu Kinyunyu alichaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya Askofu Ngowo kuugua kwa zaidi ya miaka miwili.

 Kwa mujibu wa taratibu za KKKT, inapotokea askofu akaugua zaidi ya muda huo, askofu mwingine huchaguliwa kuchukua nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment