Ishara na miujiza yatikisa jijini Dar es salaam.

Jumapili iliyopita ilikuwa ya kipekee kwa jiji la Dar es Salaam, wakati  umati wa watu kutoka maeneo mbali mbali ya jiji la Dare s Salaam, waliposhuhudia ishara na maajabu isivyo kawaida ikitendeka mbele ya macho yao  katika kanisa la TAG, Majumba sita, Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Katika Ibada hiyo ya kipekee iliyoongozwa na Mchungaji kiongozi, Mchungaji Moses Magembe, huku ikirushwa moja kwa moja (Live) kupitia kituo cha Radio WAPO FM, katika jiji la Dar es Salaam, na  mikoa ya jirani matukio ya uponyaji yasiyo ya kawaida yalishuhudiwa.

Takwimu za mtandao zinaonesha kuwa ibada hiyo pia ilikuwa ikifuatiliwa na watu zaidi ya 54 elfu, kutoka maeneo mbalimbali ya nje ya Tanzania kupitia mtandao wa Internet, wakiwepo kutoka Kanada na mataifa yasiyo na ruhusa ya kuhubiri Injili kwa uhuru.

Akifundisha somo lenye kichwa; “Utendaji wa Mungu juu ya miujiza,” huku akinukuu maandiko kutoka katika Biblia kitabu cha Matendo ya Mitume 1:8,  Mchungaji Magembe alionya wale wanaochanganya imani halisi na vitu kama vile; mafuta yanayoitwa ya upako, chumvi na maji ya baraka, pamoja na kubinafsisha maeneo yao kuwa vituo maalumu vya maombezi.

“Huduma ya kuombea watu kwa jina la Yesu inapaswa kufanywa na kila aliyempokea Bwana Yesu, haina haja ya kubinafsishwa kwa wachache tu. Askofu ambaye kwake  hakuna watu wanaoombewa na kupona basi arudishe Biblia dukani tuchukue sisi,” alisema kiongozi huyo.

Kisha aliongeza: “Tatizo hapa sio waumini, bali ni baadhi ya viongozi wamekufa na kuganda kabisa, wana majina ya Kikristo lakini hawako hai. Sasa tunamtaka BWANA  atende miujiza sio propaganda, tunataka Bwana afanye…”


Huku akinukuu maandiko matakatifu kutoka katika Biblia vitabu vya; Waebrania 9: 14, Luka 1:31, Waebrania 13: 8 na 1Wakornto 2: 14, aliwaasa Wakristo kuwa macho na watu wanaolitumia vibaya jina la Yesu kwa kuwanywesha watu vitu vya ajabu ikiwa ni pamoja na mafuta na kuwapa vitambaa na maji ya Baraka  kuacha kwa kuwa  kufanya hivyo ni kinyume na Neno la Mungu.

“Kinachoponya ni kuliamini Neno la Mungu na kuishi maisha matakatifu, sio maji ya upako wala vitambaa. Acha mara moja ……mtazame Kristo  aokoaye….” alisema Mchungaji Magembe, huku akihubiri katika mtindo wa kiinjilisti.

Mchungaji Magembe ambaye kwa kupitia huduma ya Gospel Campaign Centre, ameendesha harakati kubwa za umisheni huko, Msumbiji, Malawi, Zambia  na sehemu zingine duniani, alionya kuwa wale wanaosafiri hadi mataifa ya Nigeria kusaka upako sio wa Mungu wa Wakristo.

“Mungu wa vitambaa, chumvi, kukata viuno madhabahuni, sio Mungu wetu. Mungu wetu Wakristo anafanyakazi na Biblia na sio vinginevyo, nitaonya na kukemea mpaka Tanzania ipone,” alisema Mchungaji Magembe.
 
Miongoni mwa shuhuda za kustaajabisha katika ibada hiyo ni Leah Eliasi ambaye alishuhudia jinsi alivyonyweshwa mafuta na maji za upako alipokwenda kuombewa katika Huduma moja iliyopo jijini Dar es Salaam, (jina tunalihifadhi) lakini hakupata nafuu yoyote.

Akiwa na Mumewe Bw. Joseph Eliasi, mbele ya maelfu ya watu waliohudhuria ibada hiyo na wale waliokuwa wakifuatilia kupitia radioni na mitandaoni, alisema kuwa alikuwa akiugua mwili mzima. Karibu kila kiungo kilikuwa kikimsumbua na alikwenda hospitali mbalimbali bila msaada, mwisho akaamua kwenda kwa waganga, lakini hali ilizidi kuwa mbaya.

Ndipo alipoamua kwenda kuombewa katika huduma na makanisa mbalimbali lakini akakutana na maajabu katika kanisa moja ambapo alikorogewa mafuta ya upako, asali mbichi na maji ya Baraka na kuambiwa aogee kwa siku saba mfululizo, lakini  hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Alipofika mahali pa kukata tama ndipo alipofika Majumba sita, ambapo aliombewa kwa jina la Yesu bila maji, kitambaa wala mafuta na akapokea uponyaji wake na sasa ni mzima kabisa.

Bi. Annamaria Kimbila, akishuhudia jinsi Bwana alivyomuokoa, alisema kuwa mjukuu wake aitwaye Lilian Emmanuel alipotea jijini Dar es Salaam, na kanisa likaingia kwenye maombi na katika hali ya kustaajabisha alipatikana huko Muleba Bukoba akiwa hai na mzima wa afya.

No comments:

Post a Comment