Serikali: Uhamaji ‘Analojia’ kwenda ‘Dijitali’ ufanyike kwa awamu

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
Serikali  imeitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha kuwa zoezi la uhamaji wa mfumo wa matangazo ya analojia kwenda dijitali unafanyika kwa awamu   ili kuondoa hofu ya wananchi ya kukosa matangazo ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wakuu wa TCRA, ambao waliwasilisha taarifa ya mabadiliko ya mfumo huo ofisini kwake.

Aidha, waziri huyo aliusisitizia uongozi huo kuendelea kutoa elimu sahihi kwa umma   kwa kuzingatia ratiba ya uzimaji wa mitambo hiyo iliyotolewa.

Mkurugenzi wa Utangazaji TCRA, Habi Gunze, akiwasilisha taarifa hiyo kwa waziri mwenye dhamana alisema uzimaji wa matangazo hayo utafanywa kwa awamu tano.

Alisema kwa Kanda ya Dar es Salaam, mitambo ya analojia itazimwa Desemba 31, mwaka huu, saa sita usiku na maeneo husika ni jiji la Dar es Salaam, miji ya Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe na Mkuranga.

Vituo vitakavyohusika ni TBC1, ITV, EATV, Channel Ten, Star tv, DTV na Capital TV.

Vituo vingine ni pamoja na Tumaini TV, ATN, Mlimani TV, C2C, CTN, Clouds TV na Efatha.

Kwa Kanda ya Dodoma na Tanga, mitambo hiyo itazimwa Januari 30, 2013, maeneo husika yakiwa ni Manispaa ya Dodoma Kibaigwa, Mvumi, Mtera, Miyuji na Hombolo. Maeneo mengine ni pamoja na Muheza, Mkanyageni, Nguvu-Mali, Mabokweni na Mkinga.


Vituo vitakavyohusika ni TBC1, ITV, EATV, Channel ten, Star tv, TV ya Manispaa ya Tanga na ATN.

Kanda ya Mwanza, mitambo itazimwa Februari 28, mwaka 2013 na maeneo yatakayohusika ni jiji la Mwanza, Sengerema, visiwa vya Ukerewe na Kisesa. Vituo vitakavyohusika ni TBC1, ITV, EATV, Channel ten, Star tv na ATN.


Kanda ya Kaskazini Moshi na Arusha, mitambo hiyo itazimwa Machi 31, 2013 maeneo husika yakiwa ni jiji la Arusha, Usa River na Tengeru.

Maeneo mengine ni Manispaa ya Moshi, Mweka, TPC Gate, Mabungo, Himo, Mwika, Marangu Mtoni, Chekereni, Bombang’ombe na Machame.

Kanda ya Mbeya, mitambo hiyo itazimwa Aprili 30, 2013, maeneo husika yakiwa ni jiji la Mbeya, Mbarali, Igulusi, Igawa, Rujewa na Chimala, vituo vitakavyohusika ni TBC1, Star tv, TV ya jiji la Mbeya na ATN.

Dk. Mukangara alisema wananchi wanaoishi katika maeneo, ambayo hayakutajwa katika ratiba hiyo wataendelea kupata matangazo kupitia mfumo wa matangazo ya televisheni kama ilivyo sasa hadi hapo mitambo ya kupokea mfumo wa matangazo ya dijitali itakapokamilika kwenye maeneo yao.

Alizitaka kampuni zinazoweka mitambo ya dijitali kuongeza kasi ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo inakamilika nchi kote kabla ya mwaka 2015.

Source:Nipashe

No comments:

Post a Comment