Edward Lowassa aomba makanisa kusaidia vijana kupata ajira


Waziri  Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameyaomba makanisa nchini kuwasaidia vijana kupata mashamba ili kukabiliana na matatizo la ajira.

Lowassa alitoa ombi hilo jana wakati akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa DVD na harambee ya ununuzi wa basi la kwaya ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Msasani jijini Dar es Salaam.

Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli (CCM), alisema kwa kufanya hivyo makanisa yatasadia juhudi za serikali kukabiliana na tatizo kubwa la ajira kwa vijana nchini.

Lowassa ambaye amekuwa msemaji mkubwa wa tatizo la ajira nchini na mara kadhaa, amelifananisha na bomu linalosubiri kulipuka.

Hata hivyo,  amekuwa akisisitiza kuwa nia yake siyo kumlaumu mtu au serikali, isipokuwa jukumu la kuwaokoa vijana na janga hilo ni la kila Mtanzania.

Moja ya changamoto ambazo zilizoainishwa na Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, ni kuwepo kwa tatizo hilo la ajira kwa vijana.

Kwa mujibu wa Lowassa, wakati umefika sasa kwa makanisa nchini kushiriki katika harakati hizo kama yanavyofanya katika sekta za elimu, afya na nyinginezo, ili kupunguza tatizo la ajira.

“Nayaomba makanisa nchini yasaidie kuwatafutia vijana mashamba na kujiingiza katika shughuli za kilimo,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa sekta hiyo ambayo kwa sasa inapewa msukumo mkubwa na serikali kupitia mpango wake wa Kilimo Kwanza, inaweza kutatua kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

“Kilimo kinaweza kabisa kusaidia tatizo hili la ajira, ni jukumu letu kuwasaidia vijana kuweza kujiingiza katika sekta hii, na makanisa ni moja ya taasisi zinazoweza kutoa msaada mkubwa kuwawezesha vijana kuapata mashamba,” alisema Lowassa.

Mwishoni mwa wiki akizungumza na timu za mpira wa miguu na mikono za Bunge la Tanzania, nyumbani kwake Monduli, Lowassa aliwataka wabunge hao kuchangiza kuundwa kwa sheria ya kuwepo kwa shule za michezo nchini (sports Academy) ambazo kwa kiasi vijana watakuwa wanamichezo mahiri na kuweza kupata ajira katika sekta hiyo kama ilivyo katika nchi nyingine.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mchungaji wa Usharika wa Msasani, Eliguard Muro, alimshukuru Lowassa kwa mchango wake katika jamii pamoja na kushiriki katika harambee mbalimbali za makanisa.

Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh. milioni 100 zilitolewa, ikiwa ni ahadi na fedha taslimu. Malengo ya harambee hiyo yalikuwa Shilingi milioni 100.

Lowassa ambaye aliongozana na familia yake yote, alichangia Sh.milioni 5.

Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment