Dk. Alex Malasusa: Ataka Chokochoko za kidini zikomeshwe.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeiomba serikali kukomesha chokochoko za dini ikiwamo kupiga marufuku mihadhara yote ya dini inayotumika kukashifu dini nyingine ili kuepusha machafuko yanayoweza kutokea nchini.

Ombi hilo alilitoa jana na Mkuu wake, Dk. Alex Malasusa, katika Mkutano  Mkuu wa 31 wa Kanisa  hilo Dayosisi ya Mashariki na Pwani uliofanyika mjini Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Dk. Malasusa ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alisema ni kosa kubwa kwa serikali kuachia mihadhara ya kukashifu dini nyingine iendelee.

  Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
“Kwa kuwa serikali kupitia Wizara yake ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inahusika moja kwa moja na usajili wa dini hizi, basi ni makosa makubwa kwa serikali yetu na vyombo vyake vya dola kuachia mihadhara ya kukashifu dini nyingine iendelee, iwe ni kwa njia ya kawaida au  kupitia vyombo vya habari,” alisema Askofu Malasusa katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo.

“Kwangu mimi ninaona ni sawa na kumwacha mtu anayefikiriwa kuwa hana akili timamu, akaleta kuni na kuanza kuwasha moto kwenye kituo cha petroli, ambacho mapipa yake hayakufunikwa na  ilihali kimezungukwa na makazi ya watu na kufikiria kuwa moto hautawaka na hata kama utawaka hakuna madhara yoyote yatakayotokea,” alisema kiongozi huyo.

Dk. Malasusa alisema kuwa dini ina uwezo wa kufanya jambo la kawaida likafanyika kuwa la kufa au kupona, hivyo kuna umuhimu wa serikali na taasisi za kidini kushirikiana kikamilifu kudumisha umoja na amani katika taifa.

“Nchi yetu tuliyozoea kuiita kisiwa cha amani,  lakini hivi karibuni  tumeshuhudia uvunjifu wa amani  hiyo, hasa kwa makanisa kushambuliwa na watu wanaosemekana eti ni Waislamu wenye siasa kali, jambo hili limeniogopesha sana hasa nikiangalia kwa upande wa pili wa kulipiza kisasi na athari zinazoweza kujitokeza,” alisema na kuongeza kuwa:

“Ukweli ni kwamba hakuna taifa lolote lililoruhusu vita vya kidini likakaa salama,  dini siku zote zina uwezo wa kufanya jambo la kawaida likawa la kufa au kupona.”

Dk. Malasusa alisema bado anaamini kwamba mamlaka iliyonayo serikali itayatumia katika kukomesha kabisa chokochoko hizo za kidini, ambazo kimsingi, hazitokani na Watanzania.

“Japokuwa Wakristo tumejifunza kwamba kushindana kwetu sio juu ya damu na nyama,  lakini  bado sina uhakika kama unaweza kutoka na Biblia au na silaha, endapo mtu anakuja ndani  kwako kukushambulia na silaha,” alisema na kusisitiza kuwa:

“Watanzania ni wamoja kwa asili, wanapendana, wanashirikiana, na kwa ujumla wao wanasikitishwa sana na vikundi vinavyochochea chuki na uhasama katikati yao,  taifa letu halitaendelea kama mafarakano yatapewa nafasi kushamiri katika nchi yetu.”

Askofu Malasusa alisema: “Ninaomba Serikali ipige marufuku vikundi hivi, hatutaki viendelee wala kupewa nafasi ya kushamiri hata kama ni ndani ya Kanisa ninaloliongoza, kwani yaliyotokea Rwanda,  Burundi na Kenya hatutaki yatokee na hapa kwetu.”

Aidha, Dk. Malasusa aliliomba Kanisa kukemea vitendo hatarishi na viovu  vinavyoweza kuathiri mwenendo na mwelekeo katika jamaii.

Katiba Mpya
Pia, Askofu Malasusa alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika zoezi linaloendelea hivi sasa la maoni ya katiba, ili kutoa maoni yao na kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya.

Alisema kuna matatizo mengi katika nchi hususani rushwa, ukosefu wa ajira, ajali za barabarani na umaskini, hivyo kama wananchi watajitokeza kutoa maoni, matatizo hayo yanaweza kupata ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment