Kanisa Katoliki Zanzibar latoa tamko

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Mhashamu Augustino Shao
Kufuatia kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya nchini, Kanisa Katoliki jimbo la Zanzibar, limesema wafanyabishara wakubwa wanaoingiza biashara hiyo na kuuza visiwani humo wanajulikana.

Kanisa hilo, limesema wakati umefika kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwakamata wafanyabiashara hao badala ya kuwashughulikia watumiaji wadogo.

Askofu wa kanisa hilo, jimbo la Zanzibar, Mhashamu Augustine Shao, alisema hayo siku chache zimepita katika misa ya Krismasi iliyofanyika katika kanisa la Minara Miwili Shangani katikati ya mji Mkongwe.

Mhashamu Shao alisema wimbi la vijana kutumia dawa za kulevya Zanzibar litapungua kama SMZ itachukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wakubwa.

Alisema kuendelea kwa biashara hiyo kunasababisha madhara kwa vijana na watu wazima.

“Tuache kukimbizana na waathirika waliojikuta wakitumia dawa za kulevya kwa matatizo yao ya umasikini,” alisema.

Hata hivyo, alisema jamii inapaswa kuwasaidia waathirika wa dawa hizo badala ya kuwanyanyapaa kwa sababu kama watapata ushauri nasaha, wana nafasi ya kuacha kuzitumia.

Mhashamu Shao, alisema vijana visiwani Zanzibar wanaishi katika mazingira magumu, kutokana na matatizo kama ukosefu wa ajira, dawa za kulevya na maambuziki ya virusi vya ukimwi.

Ushauri wa Mhashamu Shao, umekuja huku takwimu zikionyesha asilimia 20 ya wagonjwa wa akili katika hospitali ya Kidongochekundu ni waathirika wa dawa hizo.

Kuhusu vurugu za Mei na Oktoba mwaka huu zilizotokea Zanzibar, alisema zimechangiwa na baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini ambao wameamua kutumia vijana wasiokua na kazi kufanikisha malengo yao binafsi.

“Ghasia na uchomaji wa makanisa zilizofanyika chini ya mwamvuli wa Muungano ni dhana nyemelezi ya wenye madaraka nje na ndani katika kutumia umasikini wa vijana wetu kutimiza malengo yao binafsi,” alisisitiza.

Alisema watu hao wameamua kutumia migongo ya masikini kwa manufaa yao binafsi na kuhatarisha amani na umoja wa kitaifa.

“Kataeni kutumiwa kwa misingi ya dini, itikadi za siasa na uchumi kwa manufaa ya watu binafsi au kuneemesha watu wachache,” alionya Mhashamu Shao.

AZUNGUMZIA KATIBA MPYA

Akizungumzia mabadiliko ya Katiba, Mhashamu Shao , aliwataka wananchi kutoa maoni ambayo yatasaidia kupata katiba yenye manufaa kwa maslahi ya Taifa na wananchi wa pande mbili za Muungano.

Hata hivyo alisema wakati huu wa mjadala wa Katiba mpya, ni muhimu wananchi wakazingatia umuhimu wa kulinda misingi ya amani na umoja wa kitaifa.

No comments:

Post a Comment