Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali,Roho ya Mpinga Kristo imeingia Tanzania

Kanisa la Tanzania limeitwa kusimama imara na kuchagua njia salama ya kuelekea, wakati huu ambao roho ya Mpinga Kristo imeingia nchini na kusababisha mateso makali, na hata mauaji ya watu wasio na hatia.

Katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Idara ya Maandiko na Uanafunzi, ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Barnabas Mtokambali alisema kuwa, kwa sasa roho ya Mpinga Kristo inatenda kazi nchini na ndiyo iliyosababisha Watanzania kuingia katika orodha ya wale wanaoteswa duniani.

“Hii si mara ya kwanza, kanisa la kwanza liliwahi kuingia katika mateso makali na maangamizi, ukisoma Biblia katika kitabu cha Matendo ya Mitume, unaona hatua kadhaa za kanisa lilipopitia katika mateso na hatua ambazo lilichukua hata kuishinda,” alisema kiongozi huyo.

Akichukua tahadhari kubwa, Dk. Mtokambali alisema kuwa, roho ya mpinga Kristo ilishaangamiza Ukristo katika mataifa kadhaa ambayo awali yalikuwa ni ya Kikristo kwa asilimia 80 hadi tisini lakini sasa umefutika.

Alitaja baadhi ya mataifa ambayo Ukristo umemalizwa kuwa ni pamoja na Misri, Tunisia na Lebanon, ambayo sasa asilimia 80 ya watu wake sio Wakristo tena.

Huku akinukuu maandiko ya Biblia kutoka katika vitabu vya Matendo ya mitume na Yohana, alisema kuwa kanisa la kwanza lilipoingia katika mateso kama lilivyo kanisa la Tanzania, halikukimbilia siasa wala harakati, bali lilipiga magoti na kumuabudu Mungu wa mbinguni.

“Naliita Kanisa la Tanzania kuachana na siasa, kuachana na mambo ya harakati lichukue hatua ile ambayo kanisa la kwanza, lilichukua. Kanisa lidumu katika maombi kwa kuwa masuala haya ni ya rohoni, hatuwezi kuyashinda kwa njia nyingine yoyote,” alisema Askofu na kuongeza:

“Mateso ya kanisa hayawezi kupata suluhu kutoka kwa mawanadamu, hatuwezi kupata msaada kutoka kwa Mbunge, chama cha siasa au mabadiliko ya uongozi…..msaada wetu watoka mbinguni tu. Kwa kutambua hilo nimeagiza maombi ya mwaka mzima ili kukabiliana na roho hii ambayo inataka kuufuta Ukristo kabisa kwenye sura ya nchi.”
Alisema, swali kubwa analojiuliza ni hatua gani Kanisa la Tanzania linachukua baada ya kuwa sasa limeingia katika mateso?
“Ikiwa Kanisa la Tanzania litachukua hatua zilizochukuliwa na kanisa la kwanza, ninahabari njema kwao kuwa Mungu atalitetea kama alivyowatetea mitume waliokuwa kwenye mateso,” alisema kiongozi huyo.

Alinukuu maandiko kutoka Matendo ya Mitume 12:12, huku ujumbe wake ukiwa na kichwa; Utendaji wa Mungu kutuokoa.

Kiongozi huyo alisema kuwa, wanasiasa wanamtazamo wao, wanaharakati wana mtazamo wao, lakini kanisa linapaswa kuwa na mtazamo wa kiroho katika kipindi chote cha mateso yake.

Alisema kuwa, historia inaonesha kuwa wakati wote ambao kanisa liliiingia katika mateso likamgeukia kristo ulitokea uamsho mkubwa, hivyo hata wakati huu ambao kanisa la Tanzania linateswa, ni vyema likachukua hiyo kama fursa ya kuamka na kuhubiri Injili kwa nguvu zote.

“Nasema tena, usalama wa Tanzania upo kanisani tu, kanisa likilala amani haitakuwepo, usalama hautakuwepo, naliita kanisa liamke na kuingia katika maombi marefu bila kuchoka,” alisema.

No comments:

Post a Comment