Tapeli wa simu alisumbua kanisa Jijini Dar es salaam!

Mtu mmoja  aliyejulikana kwa jina la Grace Ngailo, amekuwa kero kubwa kwa watumishi wa Mungu jijini Dar es Salaam, akijaribu mara kadhaa kuwatapeli kwa kutumia majina yao anayoyakuta kwenye matangazo hasa yale yanayochapwa kwenye magazeti.

Bila haya mhalifu huyo ambaye mara kwa mara amekuwa akibadili simu na kusajili zingine kwa majina tofauti lakini kwa lengo la kutumia simu hizo kwa utapeli, amekuwa akiomba fedha kiasi kidogo akijipachika jina la mtu mwingine na kudai yuko mkutanoni aazimwe fedha atarudisha baadaye.

Kwa Mfano, wiki iliyopita, tapeli huyo alijifanya Mhariri wa Gazeti la Jibu la Maisha, kisha akatuma ukumbe kwa Mchungaji Ray Seng’enge wa Kanisa la Dar es Salaam, International Church, akidai eti Mhariri yuko mkutanoni simu yake ina matatizo hivyo atumiwe kiasi cha Shilingi 50, 000.

Jumbe za aina hiyo zimekuwa zikitumwa kutoka katika jina la mtumishi mmoja kwenda kwa wengine na kwa mara chache tapeli huyo amefanikiwa kujipatia fedha kwa wale wasiojua mchezo huo mchafu unaofanywa na tapeli huyo.

Wiki kadhaa zilizopita akitumia jina la Mhariri huyo tapeli hilo liliweza kujipatia shilingi 30,000 kutoka kwa Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na haki za Binadamu Bi. Flaviana Charles. Mwanasheria huyo alipowasiliana naye, alimjibu kwa kiburi kuwa yeye angekula wapi anasumbuliwa na njaa tu.

 Habari kutoka kwa wachungaji mbali mbali jijini Dar es Salaam, zinasema kuwa tapeli huyo amekuwa akitumia majina yao kujaribu kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha usumbufu mkubwa.
Inadaiwa kuwa tapeli huyo pia husikiliza  mahubiri kwenye radio za dini na kusoma matangazo kwenye vyombo vya habari za kikristo ambapo hujipachika cheo cha Mhariri Mkuu na afisa yeyote kuwaomba wahusika kiasi cha shilingi elfu 50 na 30 akidai ana matatizo .

Baada ya matukio hayo kushamiri, uongozi wa Gazeti la Jibu la Maisha liliwahi kutoa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi cha Urafiki ambapo mpaka hivi leo watu wanaendelea kutapeliwa na hakuna juhudi zozote ambazo zimefanyika kumkamata tapeli huyo, licha ya kufuatilia kituoni hapo kwa zaidi ya mara kumi na kuahidiwa kuwa wapelelezi wanafuatilia barua kutoka kwa mkuu wa upelelezi, ilikuomba ushirikiano wa makampuni ya simu, kwa lengo la kumfuatilia.

Wananchi wanateswa na tapeli huyo wamestaajabu ni vipi polisi wanashindwa kumkamata mhalifu huyu wakati simu zote zimesajiliwa. Aidha wamemuomba Kamanda wa Polisi wa mkoa wa kipolisi wa wa Mkoa wa kipolisi wa Kinondo Charles  Kenyela, kuingilia kati kuzuia uhalifu huo.

Mwandishi wa Jibu la Maisha alipowasiliana na Kamanda kenyela kwa simu yake ya mkononi alisema, hana taarifa na anaomba yeyote ambaye ametapeliwa kufika kwake na kuandikisha maelezo pamoja na vielelezo vya ushahidi wa jumbe ili mhusika asakwe.

No comments:

Post a Comment